Friday, December 18, 2009
Somo la 13: Miji ya Kimbilio
Hesabu: Somo la 13
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.
Utangulizi: Katika sura za mwisho za kitabu cha Hesabu tunaona kwamba kwa hakika Mungu anawaingiza watu wake Kaanani. Sura ya 33 ya kitabu cha Hesabu ina kumbukumbu ya kihistoria ya safari ya kutokea Misri kuelekea Kaanani. Safari sasa inaingia kwenye vitabu vya historia na si tena sehemu ya maisha ya kila siku. Katika sura ya 34 ya kitabu cha Hesabu tunasoma kile ambacho Mungu anakiweka kama mipaka mipya kwa ajili ya Israeli. Katika sura ya 35 ya kitabu hicho hicho Mungu anaelezea mfumo wa haki unaojumuisha sehemu za magereza! Je, ungependa gereza lijengwe upenuni au uani mwa nyumba yako? Je, ulijua kwamba Israeli ilikuwa na magereza? Je, ulijua kwamba watumishi waliishi na walioshitakiwa kwa mauaji? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
I. Watumishi na Wauaji
A. Soma Hesabu 35:1-3. Hapo awali tulijifunza nini kuhusu Walawi? (Walawi walikuwa waaminifu kwa Mungu pale ambapo wana wa Israeli walikuwa wakiabudu sanamu ya ndama kwenye mlima Sinai. Matokeo yake, Mungu aliwaweka kuwa wahudumu hekaluni /madhabahuni yaani kuwa makuhani na kuihudumia jamii.
1. Kama Walawi ni “watu wazuri” kwa nini walipewa miji badala ya vipande vya ardhi (Malipo yao (urithi), kwa mujibu wa Hesabu 18:24, ilikuwa ni kupokea zaka za watu na siyo sehemu yoyote ya ardhi/nchi.)
B. Soma Hesabu 35:4-5. Kwa nini walihitaji sehemu ndogo tu ya malisho? (Kwa sababu zaka ilijumuisha wanyama. Kwa hiyo, wangekuwa nao kwa muda fulani tu kabla hawajawala.)
1. Kwa nini makuhani wasiwe wala mboga pekee? Kama hicho ndicho chakula bora, na Mungu ameweka mfumo, kwa nini basi wasiachwe kula mbogamboga pekee? (Kwa kuwa sadaka ya wanyama ilikuwa ni kuwakumbusha kuhusu Yesu, isingeleta mantiki sana kwa wao kuwa walaji wa mbogamboga tu Uzingatiaji wa kivitendo uliupiku uzingatiaji wa kiafya.)
C. Soma Hesabu 35:6-8. Walawi waliishi na watu walioua watu wengine na waliishi pamoja na watu wa makabila yote. Unadhani kwa nini Mungu alipanga iwe hivyo? Je, kuna lolote la kujifunza hapa kwa ajili ya watumishi wa leo? (Mtu aliyeua au alituhumiwa kwa mauaji ni mhitaji mkubwa wa ushauri wa kiroho. Kwa kuzingatia sehemu ya watu ambao hawakusababisha mauti, Walawi hawakupaswa kuishi kwenye koloni tofauti na wao. Badala yake, miji yao iligawanywa katika Israeli yote. Watumishi wanahitajika kuishi miongoni mwa watu.)
D. Soma Hesabu 35:9-11. Je, hii ndio “miji ya kimbilio” ambayo wauaji wote wanaishi (sambamba na Walawi na familia zao)? (Hapana. Ni kwa ajili ya wale “walioua pasipo kukusudia.”)
E. Unachukulia mauaji gani kuwa yasiyo ya kukusudia? Yanaweza kujumuisha mtu aliyetenda hivyo kwa uzembe? Mtu ambaye alikuwa akiendesha gari kwa mwendokasi wa maili 50 kwa saa kwenye eneo la shule wakati akiwa anasoma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi? (Soma Kumbukumbu la Torati 19:4-6. Msingi ni upungufu wa ile dhamira ya kukusudia. Mauaji hayakuwa ya kudhamiria.
1. Je, uzembe ulihusika kwenye mauaji ya kutumia shoka? Je, mtu mwangalifu angekagua uimara wa shoka, kwenye maungia na mpini wake kabla hajaanza kulitumia wakati kukiwa na watu pembeni yake? (Hilo ndilo suala lililopo kwenye uzembe. Kama jibu ni “ndiyo, mtu mwenye busara atakagua,” mtumia shoka ni mzembe. Kama jibu ni “hapana,” ajali ni ya bahati mbaya kwa hakika. Katika matukio yote mawili, mhusika ana uhalali wa kwenda kwenye mji wa kimbilio.
F. Soma Hesabu 35:12. Je, miji ya kimbilio ilikuwa ndio magereza? Je, ilikuwa ni sehemu ambayo wale waliotuhumiwa kwa mauaji waliishi moja kwa moja (yaani siku zote)? (Ukiangalia Kumbukumbu la Torati 19:6 inamrejea mwenye kulipiza kisasi cha damu akimwandama mwuaji “kwa hasira.” Miji hii iliruhusu wale waliokuwa na hasira kutuliza hasira zao bila mtu yeyote kuuawa katika muda huo.)
1. “Mwenye kulipiza kisasi” ni nani na anahusikaje na mji wa kimbilio? (Soma Mwanzo 9:5-6. Uwezekano mkubwa ni kwamba mlipiza kisasi alikuwa ni mtu kutoka kwenye familia ya marehemu aliyekuwa akifuata kauli ya kitabu cha Mwanzo kuhusu umwagaji damu ya mtu aliyemwaga damu ya mtu mwingine.)
G. Angalia tena Hesabu 35:12. Unadhani mfumo huu wa haki ulifanya kazi kwa namna gani? (Mji wa kimbilio haukuwa tu sehemu ya wenye hasira kupooza hasira zao, ulikuwa ni sehemu ya wale wenye mamlaka kuchanganua/kuainisha mauaji ya kukusudia kutoka kwa wale walioua kwa bahati mbaya au kwa uzembe. Mlipiza kisasi hakupaswa kumwua mtuhumiwa kabla ya shauri kukatwa.
H. Soma Hesabu 35:13-15. Je, ni nani mwenye kustahili kukimbilia kwenye mji wa kimbilio? (Mtu yeyote. Unaweza kufikiria kuwa mgeni hakulindwa na sheria ya Kiebrania. Hao ndio watu ambao walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupitia mateso kutoka kwenye kundi la watu wenye hasira. Mungu anaelekeza kwamba wote wana haki ya hukumu sawa.)
1. Je, uwekwaji wa miji unapendekeza kitu gani? (Ilikuwa ni kwa ajili ya watu wote.)
II. Maarifa ya Sheria ya Mungu
A. Soma Hesabu 35:16-18. Hivi punde tu tumejifunza kuwa “jinai ya dhamira” ndio msingi wa kuwatenganisha wale waliotiwa hatiani kwa mauaji na wale wa bahati mbaya. Je, sasa tumebadili kanuni? Je, chuma, jiwe au kipande cha mti vinahusikaje na chuki/dhamira/kusudi? (Kumshambulia mtu na silaha nzito mkononi mwako hufunua kile kilichomo akilini/mawazoni mwako.)
B. Soma Hesabu 35:20-21. Sasa tumerejea kwenye uovu wa kudhamiria. Je, kumrushia mtu kitu kwa kudhamiria ni sawa na uovu wa kudhamiria? Vipi kuhusu kumpiga mtu konde la kihasama? (Kwa kawaida, uovu wa kudhamiria humaanisha kuwa umepanga kumdhuru mtu. Nadhani sumbwi liumizalo mtu na uvurumishaji wa kudhamiria unapanua ufafanuzi wa mauaji kidogo. Unaonekana kujumuisha maumivu ya hasira.)
C. Soma Hesabu 35:22-23. Je, mifano hii inaashiria uzembe au makusudi? Unadhani tofauti ya msingi ni ipi? (Ni ile “Dhamira ya kudhuru.”)
1. Hebu jifanye kwamba upo kwenye baraza la wazee wa mahakama na mafungu machache ya mwisho ni maelekezo ya wazee wa baraza la mahakama. Je, yapo wazi vya kutosha kwako?
2. Unaweza kujisikia kuwa na ujasiri wa kuhukumu kesi ya mauaji? (Nafikiri maelekezo ya Mungu yapo wazi kabisa.)
3. Sheria za nchini kwako zinafanana na hizi kwa kiasi gani? (Sijajihusisha na sheria za jinai kwa zaidi ya miaka thelathini, lakini kanuni hizi zinaonekana kuakisi sheria za asili za mauaji za Marekani. Hata hivyo, kanuni zetu za “jinai-mauaji” na za “kushiriki kwenye njama” zinatoa wigo mpana kuliko sheria za Mungu.)
D. Nini hutokea kwa wale wanaoua mtu kwa uzembe au kwa bahati mbaya? Je, huachwa huru? (Watu hawa wanaelezewa kwenye kitabu cha Hesabu 35:22-24, ambapo tumesoma hivi punde. Hebu tusome: Hesabu 35:25-28. Hukumu hii ni ya aina gani?
1. Unadhani hii ni haki? (Adhabu ni sawia na”kosa.” Kwa bahati mbaya au kwa uzembe mtu kapoteza maisha yake. Adhabu ni ukomo wa maisha ya mwuaji unaopimwa kwa bahati – Kuhani Mkuu ataishi kwa muda gani? Inaonekana bahati inahusishwa kwenye pande zote mbili: kwenye kifo na kwenye adhabu.)
a. Hii inafananishwaje na sheria ya nchini mwako? (Kama kifo kwa hakika ni cha bahati mbaya, hatumwadhibu mwuaji kabisa.)
E. Tumejadili kanuni ya sheria, vithibitisho vinavyohitajika kwenye mauaji ni vipi? Hebu tusome Hesabu 35:30. Katika kiwango hiki, je, mwuaji anaweza kuuawa kutegemeana na kukiri wakati akiwa kwenye kizuizi cha polisi? (Hapana. Shahidi mmoja hatoshi. Mungu ana kanuni dhidi ya mtu kujitia hatiani mwenyewe.)
1. Mashahidi wangapi wanahitajika? (Soma Kumbukumbu la Torati 17:6-7. Wawili au watatu.)
a. Je, hii ni kama kusema kuwa “Nitakuuzia gari langu kwa Dola za Marekani 5,000-6,000” na hiyo imaanishe kuwa bei ni Dola za Marekani 5,000?
b. Je, kanuni ya “Mashahidi kuwa wa kwanza kuua” ina athari gani kwenye ushahidi wa shahidi? (Hii inapendekeza kwamba unahitaji kuwa na angalao mashahidi wawili wa kuaminika. Mtu ambaye hana uhakika hatataka kuwa sehemu ya mauaji. Kama kuna mashahidi wawili dhaifu, hiyo haitoshi.)
c. Je, hii inamaanisha kwamba chini ya kanuni za Mungu baadhi ya wauaji wataachwa huru?
F. Soma Hesabu 35:31-32. Je, matajiri wanajiendesha chini ya kanuni tofauti za haki kwenye mfumo wa Mungu? (Hapana. Huwezi kulipa fedha ili kubadili hukumu.)
G. Soma Hesabu 35:33-34. Sababu ya hizi kanuni ni ipi? (Wanaishi ndani ya uwepo wa Mungu.)
III. Mungu Aking’ara
A. Kanuni hizi za mauaji, na hasa hasa mafungu ya mwisho tuliyosoma, yanatufundisha nini kuhusu Mungu wetu? (Ni Mungu wa haki mwenye kulinda uzima. Tunaona hili kwenye kanuni moja ya sheria kwa ajili ya kesi za haki zote kwenye mfumo wa miji ya kimbilio.)
B. Je, mpango wa wokovu wa mfumo wa Mungu wa “mbadala wa kondoo”, “mbadala wake wa Yesu” unajihusianisha vipi kwenye kanuni ya sheria ambapo zote mbili zinazuia fidia (Waamuzi 35:31) na zinahitaji upatanisho kupitia kifo cha mdhambi (Waamuzi 35:33)? (Vitu viwili. Kwanza, tunazungumzia kuhusu kanuni za maisha hapa duniani, siyo uzima wa milele. Pili, Yesu ni Muumbaji wetu. Siyo tu mtu fulani aliyejitoa kwa ajili ya kufidia maisha yetu. Kafara ya Yesu siyo tu inaonyesha asili ya kutisha ya dhambi, inaonyesha jinsi gani Mungu atatenda kuyaokoa maisha yetu ya umilele.)
C. Rafiki, tunae Mungu wa haki na rehema. Je, utakubali rehema zake ili usikabiliane na haki yake? Kwa nini usiutoe moyo wako kwake sasa hivi?
IV. Juma Lijalo: Tutaanza mfululizo mpya kuhusu “Karama za Rohoni.”
Friday, December 11, 2009
Kizazi cha Pili: Mausia
(Hesabu 26-32)
Hesabu: Somo la 12
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.
Utangulizi: Maisha ya wazazi wako yanaathirije maisha yako? Baadhi ya watoto huwalaumu wazazi wao kwa makosa yao na kurudia kuyafanya makosa ya wazazi wao. Wengine huangalia mazuri na mabaya ya wazazi wao, na kisha hudhamiria kufanya vema zaidi pale ambapo wazazi walitenda mabaya. Musa anasimama kama mzazi kwa kwa vizazi vyote viwili, cha kwanza na cha pili. Waisraeli walifanyaje pale ilipofikia kwenye kizazi cha pili? Musa alifanyaje kukabiliana na makosa yake na makosa yao? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kubaini zaidi!
- Kizazi Kipya, Fursa Mpya
- Hesabu 26 inahesabu upya sensa iliyochukuliwa na Musa na Eleazari. Soma Hesabu 26:63-65. Nani hakuhesabiwa? (Wale waliokuwa watu wazima na wale waliokataa kuingia Kaanani mara ya kwanza.)
- Je, hii inauma? Je, tunapata nafasi moja tu maishani kuwa na mafanikio? (Kwa kusema wazi, hapa hatuzungumzii kuhusu wokovu. Hata hivyo, maamuzi ya muhimu ya kimaisha mara nyingi huwa yanafanywa pale tunapokuwa wadogo. Maamuzi haya yanaweza kuathiri mfumo mzima wa maisha yetu.)
- Soma Hesabu 26:51-56. Je, kwa kupigia kura, ndio njia sahihi ya kugawa ardhi? Kwa nini ardhi bora isipewe kwa wapiganaji wazuri? Kwa nini iliyo bora wasipewe walio werevu?
- Unawezaje kuelezea mfumo uliotumika? (Ni ya nadharia ya kivitendo. Inaziweka familia pamoja na kuwaweka mbali watu wanaohitaji ardhi hiyo.)
- Soma Matendo ya Mitume 1:23-26. Unadhani hii ni bahati kwa hakika?
- Soma Yoshua 15:13-17. Je, sehemu ya Kalebu ni matokeo ya bahati? Kalebu alitumia mbinu gani kutia moyo uwerevu? (Kalebu aliahidiwa ardhi/nchi iliyokaliwa na majitu makubwa kwa sababu aliitaka ile ardhi. Alimchagua mkwerima wake kwa ujanja. Utengaji wa ardhi haikuwa kwa bahati tu.)
- Ni fundisho gani la kiroho unaliona kwenye mfumo wa Mungu wa kugawa ardhi? (Katika hali fulani tunaona mfumo wenye kustahili, na katika hali nyingine tunaona mfumo wa nadharia ya kivitendo.)
- Ni kitu gani cha muhimu ambacho uamuzi wa utengaji ardhi huu unachukulia? (Ya kwamba kizazi cha pili kilikuwa kinaelekea kufanikiwa wakati ambapo kizazi cha kwanza hakikufanikiwa.)
- Mungu Mwenye Fursa Sawa
- Soma Hesabu 27:1-4. Jibu la kihistoria la swali lililoulizwa kwenye kitabu cha Hesabu 27:1-4 ni lipi? (Utashangaa. Soma 1 Mambo ya Nyakati 2:34-36. Tunaona hapa kwamba urithi ulipitia kwa binti. Hii ilitokea kabla ya wakati wa Musa. Kwa bahati mbaya, hata katika nyakati hizi za kisasa kuna nchi zinazowakatalia wanawake haki ya kumiliki vitu.)
- Je, hawa walikuwa mawakili wa mwanzo wa ukombozi wa wanawake? Waliyapata wapi mawazo hayo? (Tafsiri ya Biblia ya Wycliffe inatuambia kwamba kule Misri urithi ulipitia kwa akina mama.)
- Soma Hesabu 27:5-7. Jibu la Mungu ni lipi? (Mungu anakubaliana na wanawake. Wanapaswa kurithi ardhi ya baba yao.)
- Soma Hesabu 27:8-11. Ikiwa ni matokeo ya hawa wanawake kusimamia haki ya milki zao, nini kilitokea? (Waliweka mfano! Kuanzia pale, mabinti walirithi kabla ya ndugu yeyote wa mbali.)
- Mwanzo wa Mpito
- Soma Hesabu 27:12-14. Kama wewe ungekuwa Musa ungelichukuliaje suala hili? Mungu anakuonyesha lengo la maisha yako, kisha anasema "Hutaingia kwa sababu ya dhambi yako."
- Ungekuwa na visingizio? Ungebisha ya kwamba Mungu hapaswi kuwa mkali sana?
- Tunapata fundisho gani la kiroho hapa? Je, Mungu anakuwa mkali sana? (Tunajua kwamba Musa alichukuliwa mbinguni (Mathayo 17:3), kwa hiyo Mungu alimtimizia ahadi yake ya juu kabisa ya nchi ya ahadi. Lakini, tusisahau kwamba Mungu ni Baba yetu na Hakimu wetu kwa wakati mmoja. Ana viwango vya juu kwa ajili yetu.)
- Soma Hesabu 27:15-17. Musa ana mrejesho wa aina gani kutokana na suala lililotokea hivi punde? (Anawaangalia tu watu. Kumbuka ya kwamba hawa ni watu wale wale waliomdhihaki na kumsababishia kuingia kwenye dhambi iliyomzuia kuingia kwenye nchi ya ahadi.)
- Musa ni mtu mkuu wa namna gani?
- Soma Hesabu 27:18-20. Kwa nini Yoshua alichaguliwa? ("Mtu mwenye roho ndani yake." Hata katika zama za Agano la Kale, kuwa mwenye kujazwa roho ilikuwa ni muhimu kwa ajili ya uongozi.)
- Soma Hesabu 27:21-23. Je, Yoshua ana hadhi sawa na Musa? Umebaini kuwa utofauti ni nini? (Mungu alizungumza moja kwa moja na Musa. Lakini, Yoshua anapaswa kujifunza mtazamo wa Mungu kupitia kwa Eleazari, Kuhani Mkuu, ambaye atayapokea kutoka kwenye Urimu.)
- "Urimu" ni kitu gani? (Soma Mambo ya Walawi 8:8. Biblia kamwe haituelezei kwa uwazi kuwa Urimu na Thumimu ni vitu gani. Kwa kawaida inaaminika kwamba ni mawe yaliyopo kwenye kifuko cha kifuani mwa Kuhani Mkuu ambayo kwa namna moja yanaashiria uamuzi wa Mungu kwenye jambo fulani. Vyovyote vile walivyofanya, hakuna hata mmoja anayezungumza na Mungu sasa.)
- Viapo
- Soma Hesabu 30:1-2. Ni mara ngapi kiongozi wa kanisa lako alikuomba utoe ahadi ya kitu fulani mbele za Mungu? Umewahi kuambiwa kunyoosha mkono wako au kusimama pamoja na watu wengine?
- Kama ndivyo, ahadi hii ni nzito kiasi gani? Je, inategemeana na jinsi ombi lilivyofanywa? (Nakumbuka mchungaji wetu aliwaomba watu kuweka ahadi kusoma Biblia zao muda wote hadi mwaka ujao. Kama kamwe hujawahi kusoma Biblia, kwa hakika fanya hivyo.)
- Kwa nini mtu fulani anajaribiwa/anashawishika kuvunja nadhiri aliyoweka kwa Mungu? (Mungu hatakufungulia mashtaka? Mara nyingine tunafikiria wajibu wetu kwa Mungu na kanisa kama vitu visivyotuchukulia nafasi kuliko wajibu wetu wa kulipia nyumba pamoja na magari yetu.)
- Bado Unasita?
- Soma Hesabu 32:1-5. Nini kiliwatia hamasa haya makabila mawili kutaka kukaa upande wa jangwani wa mto Yordani? (Ardhi ilikuwa nzuri kwa ufugaji na hawakutaka kuwavusha kwenye mto.)
- Unaweza kufikiria sababu nyingine zozote ambazo hawakutaka kuvuka mto? (Waliwashinda watu kwa upande wao wa Yordani, lakini siyo kwa upande mwingine wa Yordani!)
- Soma Hesabu 32:6-8. Musa alijibu nini kuhusiana na mpango huu?
- Anafikiria nini kihistoria kuhusiana na hili? (Ya kwamba miaka arobaini iliyopita mababu zao hawakutaka kuvuka Yordani na hiyo ilisababisha miaka arobaini ya kutangatanga! Hawapaswi kufanya kosa lile lile tena.)
- Je, hiki kizazi cha pili ni kama kile kilichokataa kuingia Kaanani? (Fafanuzi za Biblia
kadhaa zinasema kwamba hii ni ardhi nzuri sana – nzuri kuliko ya upande wa pili wa Yordani.)
- Soma Hesabu 32:14-15. Je, inaonekana kutokuwa sawasawa ya kwamba Musa alikuwa anawaambia hawa watu, hata kama alifahamu hataingia Kaanani? (Gundua ya kwamba Musa si kwamba anaongelea kuhusiana na mustakabali wao, bali mustakabali wa wote. Kama kiongozi, hilo ni jukumu lake. Hawi mnafiki.)
- Soma Hesabu 32:16-19. Je, counter-offer
hii ni ya msingi? Je, inaponya pingamizi lililowekwa na Musa?- Je, unadhani ya kwamba wana wa Reubeni na wana wa Gadi walikuwa na hili mawazoni mwao pale walipotoa pendekezo la awali? (Nahisi walikuwa wanataraji kuusemea tu upande wao upande wao wa Yordani.)
- Soma Hesabu 32:20-24. Vipi kuhusu uchaguzi wa ardhi kwa kutumia mfumo wa kugawana tulioujadili mwanzoni mwa somo hili? (Kwa dhahiri kabisa, ulikuwa na nafasi ya kufanyiwa maboresho. Musa aliona kwamba walikuwa hawawi waoga, hawakuwa wakimwamini Mungu, na kwamba kwa hakika waliihitaji ardhi hii. Kwa hiyo alikubali kuwaruhusu kutunza ardhi hii, kutegemeana na masharti yaliyowekwa.)
- Baini tena Hesabu 32:21. Ni nani anayepigana? ("Bwana….. amewafukuza maadui zake kutoka mbele zake." Mungu ndiye ambaye anafanya unyanyuaji wa vitu vizito.)
- Soma Hesabu 32:28-30. Ni nini kilicho kitu cha muhimu sana kwenye huduma zetu kwa ajili ya Mungu? (Kujitoa tayari kutumika. Watu wengi sana wanazungumza, lakini siyo wengi kwa hakika wanafanya chochote.)
- Rafiki, vyovyote vile ambavyo wazazi wako waliishi, je, unayachukulia majukumu yako kwa Mungu kwa dhati? Kama hivyo ndivyo, Mungu yupo tayari kukupigania na kukuzawadia kwa ukarimu!
- Juma Lijalo: Miji ya Kimbilio.
Sunday, December 6, 2009
Lesoni ya 11: Uzinzi Mpakani
(Hesabu 25 &31)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sememu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani, Kihispania, Kizulu, nk.
Utangulizi: Miaka mingi iliyopita nilimfahamu bwana mmoja mheshimiwa na mtu muhimu (au: mstahiki) sana ambaye alikuwa rais wa Chuo Kikuu. Alianguka kwenye dhambi ya uzinzi, akapoteza kazi yake, hadhi yake, na nani ajuaye, kingine zaidi alichopoteza! Umewahi kubarikiwa na Mungu, halafu ukatekwa na dhambi fulani ndogo ya kijinga kiasi cha kuipoteza mibaraka ya Mungu? Somo letu juma hili ni mwendelezo wa mada tuliyofungia somo la juma lililopita: jinsi ya kucheza na tunavyojikosesha mibaraka ya Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu na tujifunze ambacho hatupaswi kukifanya!
I. Kunyakua kushundwa toka kinywani mwa ushindi
A. Juma lililopita tulijifunza kwamba Balaki na Balaamu hawakuweza kuilaani Israeli. Sanasana walichoweza kukifanya kilikuwa ni kuibariki. Hata hivyo, Balaam alidhani kwamba angeweza kuizidi mibaraka ya Mungu kwa kuwalaghai/kuwashawishi Waisraeli kutenda dhambi. Balaam shurti alifahamu madhaifu kadhaa ya mwanadamu.
B. Soma Hesabu 22:1. Wakati huu Israeli wako wapi? (Wako tayari kuvuka mpaka kuingia Kaanani. Lengo lililosubiriwa kwa muda mrefu la safari kutoka Misri sasa laelekea ukingoni. Wanahitajika tu kuvuka mto Yordani ili waingie nyumbani.)
C. Soma Hesabu 25:1-3. Waisraeli wapo salama kwa kiwango gani? (Waliyashinda mataifa kadhaa na Wamoabu waliwaogopa. Mungu siyo kwamba tu aliwalinda, alijipanga ili kwamba adui yao awabariki! Wakiwa na mibaraka tele chini ya uangalizi wa Mungu, walikuwa tayari kufikia lengo la maisha yao.)
1. Je, "nyakati nzuri" ni za hatari kiasi gani pale linapokuja suala la dhambi?
2. Je, unapitia "nyakati nzuri" kwa sasa? Nyakati za mbaraka na amani?
3. Je, unaweza kuwa na huruma na sehemu yoyote ya dhambi ya au wana wa Israeli? Je kuna kitu kama hiki katika vyombo vya habari hivi leo? (Kwa kuwa mimi ni mwanaume, siyo vigumu kwangu kufikiria kwa nini wana wa Israeli walijiingiza kwenye masuala ya ngono na wanawake wa Kimoabu. Rejea ya kwamba Ufunuo 2:14 inafunua mpango wa wanawake wa Kimoabu wa kuwalaghai/kuwashawishi wanaume wa Kiebrania. Bila shaka hawa walikuwa wanawake wenye kuvutia na ilikuwa ni mkakati wa serikali yao.)
a. Lakini, kwa nini kuabudu miungu yao? Kivutio cha miungu yao ni nini? (Tafsiri ya Biblia ya Wycliffe inaelezea kwamba sikukuu za majira ya kipupwe)zilisheherekea kukutana kimwili kwa kwa Baal-peori na mungu-mke wa uzazi. Kwa mujibu wa uvumbuzi wa mambo ya kale, ukahaba ulikuwa ni sehemu ya huduma ya ibada.)
b. Fikiria ya kwamba unatafuta kanisa jipya. Katika kanisa A wanachinja wanyama kama sehemu ya ibada. Katika kanisa B, wafanya ngono kama sehemu ya ibada. Unabashiri nini kuhusiana na umashuhuri wa hayo makanisa mawili?
(1) Sina habari kama kuna makanisa yoyote hapa kwenye eneo langu (au hata katika nchi yangu) ambapo ngono ni sehemu ya ibada, lakini je, hili wazo la kuchagua kanisa kutegemeana na kama huduma ya ibada inakupendezea si jambo linalotendeka hivyo hata leo?)
D. Hesabu 25:3 inasema kuwa "hasira za BWANA zikawaka juu ya Israeli." Jiweke kwenye nafasi ya Mungu. Kwa nini amekasirika? (Kile ambacho wana wa Israeli wanakifanya ni makosa katika nyanja nyingi.
Siyo waaminifu kwa Mungu wao, wake zao na familia zao. Haionyeshi utii kwa Mungu ambaye ndiye aliyewafikisha kwenye mpaka wa nchi ya ahadi. Inakiuka kanuni za Mungu kuhusiana na mwenendo wa mahusiano ya kingono. Pia haionyeshi utii kwa taifa lao.)
E. Soma Hesabu 25:4-5. Je, Mungu anajali mienendo yetu?
1. Angalia ya kwamba wale wanaume wasiokua waasi walikuwa na "viongozi." Hilo linatuambia nini? Nilidhani kwamba ilikuwa ni wanaume wachache waliotamani ambao walijipenyeza hadi kwenye kambi ya Wamoabu! Je, hiyo ni kweli? (Kama ilivyo kwa karibu dhambi zote, huwa tunajaribu kuzihalalisha. Huenda wengine walidai kwamba hii ilikuwa njia ya hali ya juu ya ibada ya kumwabudu mungu mkuu. Waliwashawishi wengine kuungana na kundi lao. Hizi zilikuwa ni harakati), sio kupitiwa tu.
F. Soma 25:6. Israeli wanaomboleza mbele za Mungu. Kwa nini? (Chukulia hisia ya hili. Wengine wana marafiki na wanafamilia waliokuwa sehemu ya dhambi ya Wamoabu na sasa wameadhibiwa kifo hadharani. Wengine wamesikitishwa kwa sababu ya kumkosea Mungu. Wengine wanasikitika kuhusu kufa kutokana na tauni. Wengine wanakatishwa tamaa na jinsi mambo yanavyokwenda wakati ambapo wameukaribia kabisa ushindi. Habari njema ni kwamba wote wanamsogelea Mungu kwa ajili ya msaada.)
G. Soma 25:6-9. Punde tu tumejadili kwamba taifa linalia, huyu "mwanaume wa Kiisraeli" anafanya nini? Unaelezeaje mwenendo wake? (Wakati ambapo taifa linatubu, na tauni imepamba moto, mwanaume huyu ni mjasiri sana wala hata hajali dhambi yake kwa kumleta mwanamke Mmidiani kwenye hema lake mbele ya kadamnasi. Hii inaunga mkono hitimisho langu la awali ya kwamba hizi zilikuwa ni harakati, na wala siyo wanaume wachache wakijificha kwa woga gizani.)
1. Je, unafiki umehafifishwa hapa? (Walao wanafiki wanatambua mwenendo mzuri wa tabia. Kwa hakika kutetea uovu na kutenda uovu bora kuliko kuutetea) ukweli na kisha kutenda uovu. Wanafiki wanaonekana wabaya tu, hawana wafuasi.)
2. Unafikiria nini kuhusu matendo ya Finehasi, Kuhani Mkuu mtarajiwa)? Je, hili linaonekana kama jambo jema kufanywa, au hili linaonekana kama jambo la Kitalibani? (Habari inaonyesha kwamba wawili hao walikuwa wanafanya ngono, vinginevyo ingekuwa vigumu sana kuwachoma kwa fumo (mkuki) tumboni mwao wote wawili kwa pamoja. Ujasiri huo wa kutenda dhambi unalinganishwa na ujasiri wa mtumishi wa Mungu kupigana dhidi ya dhambi.)
3. Soma Mambo ya Walawi 20:10. Je, Finehasi anatenda kinyume na sheria? (Hapana. Hili siyo tu tendo la kutisha. Finehasi anatekeleza hukumu inayojulikana na kueleweka sana kwa huyu mtu.)
a. Hebu subiri kidogo. Mwanamke hakujua kuhusu ile sheria, sawa? (Makosa. Kumbuka ya kwamba hii ilikuwa sehemu ya mpango wa Wamoabu kuwashawishi Waisraeli kutokuwa waaminifu kwa Mungu wao. Mwanamke yule alijua kuhusu mpango ule.)
H. Soma Hesabu 25:10-13. Mungu anafikiria nini kuhusiana na nia/hamasa za Finehasi? (Mafungu yanasema kwamba alikuwa na "wivu" kwa ajili ya Mungu.)
1. Baini kwamba Hesabu 25:13 inasema kwamba Finehasi aliwafanyia "upatanisho" wana wa Israeli. Hilo ni kweli kivipi? Nilidhani kwamba upatanisho ulifanywa pale ambapo kuhani alitoa kafara ya mnyama, siyo wanadamu? (Mnyama alikuwa ishara ya Yesu ambaye alipatanisha dhambi zetu. Alikufa kwa ajili yetu. Kama tukimkataa/tukimkana Yesu, tutakufa katikati ya) dhambi zetu kama kwa hakika ambavyo wawili hawa walivyokufa katikati ya dhambi zao.)
2. Soma Zaburi 106:30-31. Tendo hili "linamhesabuje" Finehasi kuwa mwenye haki? Nini kilitokea kwenye haki kwa imani? Je, nafasi ya hili imechukuliwa na haki kwa fumo (mkuki)? (Nadhani ilikuwa ni kusimama thabiti kwa ajili ya Mungu, kumchagua Mungu kwa uthabiti, ambako ndiko kulikomshindia Finehasi kuwa mwenye haki. Hii inakubaliana na pendekezo katika Hesabu 25:11 ya kwamba Finehasi alikuwa akiutetea wivu wa Mungu.)
3. Hatuna haja ya kutizama mbali kuona dhambi ya uzinzi katika tamaduni zetu. Pale inapokuja kwenye matendo yako wewe mwenyewe, je, unasimama kwa uthabiti kwa ajili ya Mungu? Wengine wanakuona vipi pale linapokuja kwenye suala la usafi wa masuala ya kingono?
- Baini kwenye Hesabu 25:8 na Zaburi 106:30 kwamba tauni ilizuilika ikiwa ni matokeo ya uingiliaji kati wa Finehasi. Hebu turukie mbele na kusoma Hesabu 31:22-23. Hii ni rejea ya utekaji nyara uliofanywa kutoka kwa Wamidiani. Hili linapendekeza nini kuhusu chanzo cha tauni? (Hii inapendekeza kwamba Wamidiani walikuwa na magonjwa ambayo Waisraeli hawakuwa na kinga nayo. Watu hawa waliingiza tauni kwenye kambi ya Waisraeli. Mungu alizuia tauni ikiwa ni matokeo ya tendo la haki la Finehasi.)
II. Ulipizaji Kisasi
A. Kitabu ninachokisoma kinatoa maoni kwamba kwa taifa la Wakristo, raia wa Marekani wanapenda kulipiza kisasi sana. Tunaona hili kwenye sinema zetu, vitabu na matendo ya kitaifa. Soma Hesabu 31:1-2. Israeli ilifanyiwa kitu gani kinachostahili ulipizaji kisasi? (Njama za Balaki na Balaamu zilizosababisha tauni.)
1. Unafikiria nini kuhusu tendo la mwisho la Musa kuwa sehemu ya ulipizaji kisasi?
2. Unaamini juu ya ulipizaji kisasi? (Vipi kuhusu sinema ya mwisho, mchezo au kitabu ulichokisoma ambapo ulifurahia mauti ya "mtu mbaya?")
3. Soma Warumi 3:5-6, Warumi 12:19-21 na Waebrania
10:30-31. Je, ulipizaji kisasi ni jambo jema au baya?
a. Je, Finehasi angewapatia kikombe cha maji ya baridi badala ya fumo (mkuki)?
b. Ni nini wajibu wetu kwenye ulipizaji kisasi? (Tunapaswa kuacha ulipizaji kisasi mikononi mwa Mungu. Maelekezo kwa Musa na tendo la Finehasi vinaonyesha kwamba mara nyingine Serikali ni nyenzo za Mungu kwa ajili ya kufanya ulipizaji kisasi.)
B. Rafiki, kumwabudu Mungu ni muhimu. Je, utadhamiria kwa dhati leo kumheshimu Mungu maishani mwako? Je, utakuwa mwaminifu katika eneo la usafi wa mahusiano ya kingono hata kama watu wengine watakufanyia njama dhidi yako?
III. Juma Lijalo: Kizazi cha Pili: Mausia