Thursday, December 30, 2010

Somo la 2: Msaada wa Mungu wa Kukabiliana na Wasiwasi

(Mwanzo 15, Yohana 14, Mathayo 6)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: “Siku moja moja.” “Usijali, furahia,” “Unasema – Mie niwe na wasiwasi?” Ninafikiria hiyo kauli ya kwanza kama bango lililopachikwa kwenye gari, ya pili kama kaulimbiu ya kisiwa fulani hivi, na ya tatu ni nukuu kutoka kwa Alfred E. Neuman kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la uchizi. Je, haya ni maneno ya kuishi kwayo? Au, je, ni fikra za watu wasio na njozi za kuona mbali, wavivu na wenye wazimu/ kwa ujumla, suluhisho langu kwenye wasiwasi ni kufanya kazi kwa bidii, kufanya mazoezi zaidi na kupanga vyema. Mimi ni kichaa? Je, unakabilianaje na wasiwasi? Je, wasiwasi unadhoofisha kabisa maisha yako na kuyafanya yawe na furaha kidogo? Hebu tuzame kwenye Biblia na kuona kile tunachoweza kujifunza kuhusiana na mtazamo wa Mungu juu ya wasiwasi!

I. Ibrahimu na Wasiwasi

A. Soma Mwanzo 15:1. Je, ni aina gani ya vitu ambavyo kwa kawaida huwa unakuwa na wasiwasi navyo? (Kutokewa na kitu kibaya kwako wewe au kwa familia yako?. Kufadhaishwa kwa kutotenda jambo fulani kwa uzuri.)

1. Kama majibu yaliyopendekezwa yanaakisi wasiwasi wako, je, ni kwa jinsi gani Mungu anayazungumzia? (Mungu anasema “mimi ni ngao yako” ambayo inapendekeza kuwa anatukinga kutokana na vitu vibaya. Mungu pia anasema kuwa yeye ni “thawabu yetu kubwa sana,” kitu kinachopendekeza kuwa tutakuwa salama. Tutapewa thawabu.)

B. Soma Mwanzo 15:2-3. Ibrahimu hasemi kuwa ana wasiwasi. Je, unadhani kuwa ana wasiwasi? (Mungu anasema nitakuwa ngao yako na thawabu yako. Ibrahimu anajibu kuwa Mungu hajamkinga kutokana na matatizo ya kifamilia ya kutokuwa na mrithi. Mungu hajamsaidia katika Idara ya thawabu kwa sababu hana mwana wa kuendeleza uzao wake na kurithi fedha zake. Kama hivi ndivyo vitu ambavyo kwa kawaida huwa tunakuwa na wsiwasi navyo, basi Ibrahimu ana wasiwsi.)

1. Je, wewe u kama Ibrahimu: je, unasema, (ahadi za Mungu haziendani na uhalisia?”

2. Je, una wasiwasi kuhusiana na kile unachokisoma kutoka kwenye Biblia? Kwa mfano, Ayubu, mtu mkamilifu, watoto wake wanauawa na anapoteza utajiri wake. Tunasoma vitu kwenye Biblia ambavyo vinapaswa kuwafanya wafuasi wa Mungu kuwa na vitu vingi vya kuwa na wasiwasi navyo (kama vitu hivyo vina mantiki yoyote), sawa?

C. Soma Mwanzo 15:4-6. Je, Mungu anajibuje swali la Ibrahim kuhusiana na pengo lililopo kati ya ahadi za Mungu na uhalisia? (Mungu anaweka ahadi maalum/mahsusi kwa Ibrahim kwamba ataziba pengo hilo siku za usoni – na Ibrahim anamwamini Mungu.)

1. Je, ni kwa namna gani tunapaswa kukitumia kisa hiki kivitendo maishani mwetu? (Ibrahimu aliangalia mbele zaidi ya uhalisia kwenye ahadi ya Mungu. Tunajua kuwa Mungu kwa hakika alitimiza ahadi yake kwa Ibrahim.)

2. Soma Waebrania 11:11&13. Je, ni mustakabali upi unaelezewa hapa kwa ajili ya wasiwasi? (Kuamini ahadi za Mungu hata kama hatuzioni zikitokea tungali hai.)

3. Je, unaweza kuipataje ahadi ya Mungu kwako? (Yumkini Mungu atatujia kama alivyomjia Ibrahim na kuweka ahadi mahsusi. Kwa namna hiyo hiyo, tunahitajika kuichungua Biblia kwa ajili ya ahadi za Mungu kuhusiana na vitu vinavyotutia wasiwasi. Hebu tufanye hivyo katika hatua inayofuata.)

II. Ahadi ya Mungu Kuhusu Mahusiano

A. Soma Yohana 14:1-3. Je, ni kitu gali kilikuwa kinawahangaisha wanafunzi wa Yesu? (Yesu aliwaambia kuwa alikuwa anaondoka.)

1. Je, ni aina gani ya wasiwasi ilisababishwa na hilo? (Wanafunzi wake walikuwa na wasiwasi kuhusiana na “familia zao.” Walikuwa na wasiwasi juu ya hatma ya taaluma yao siku za usoni (angalia Matendo ya Mitume 1:6).)

a. Je, wanafunzi walipaswa kuwa na wasiwasi kuhusiana na vitu hivi? Je, tunajua nini kuhusu siku zao zijazo ambazo wao hawakuzijua? (Ndoto zao za kuwa watawala hapa duniani zilivunjwa matumaini. Yesu hakurudi kuwachukua kwenda nyumbani katika kipindi cha maisha yao.)

2. Je, ni ahadi gani anayowapatia Yesu inayohusika kwetu? (Yesu alisema kuwa angeyafanya haya mambo sawia ambapo angerejea.)

III. Ahadi za Mungu Kuhusiana na Vitu

A. Soma Isaya 33:15-16. Je, Mungu anawaahidi nini waaminifu? (Maji ya kutosha na chakula cha kutosha.)

1. Je, wanafunzi walikuwa na malengo/matarajio makubwa ya kidunia zaidi ya hayo? Je, vipi kuhusu wewe?

a. Je, inawezekana kuwa baadhi ya wasiwasi wetu upo kwa sababu tunaweka matamanio yetu ya kuwa na vitu kuwa ya juu sana? Je, ulafi/uroho ni chanzo cha wasiwasi wetu?

2. Soma Wafilipi 4:11-13. Nini siri ya Paulo ya kuepuka wasiwasi kuhusiana na utajiri wake?

B. Soma Mathayo 6:25. Hii inapendekeza uwekaji wa vipaumbele vyetu kwa ajili ya matamanio yetu. Ni yapi hayo? (Uzima na afya njema ni vya muhimu zaidi ya chakula na mavazi.)

1. Je, huu mpangilio wa umuhimu unahimiliwa na wasiwasi? (Hehu tuendelee kusoma.)

C. Soma Mathayo 6:26. Je, tunapaswa kuhitimishaje kuhusiana na wasiwasi kutoka katika hili fungu? (Ya kwamba Mungu atatupatia chakula kwani anawapatia chakula ndege ambao ni wenye umuhimu mdogo.)

1. Rejea nyuma na uangalie mpangilio wa umuhimu: ya kwamba maisha yetu ni ya muhimu kuliko chakula. Je, Yesu anasema nini kuhusu maisha yetu? (Kama Mungu atatoa chakula, kwa hakika atatoa pia kwa ajili ya uzima wetu.)

2. Je, Yesu anapendekeza kuwa hatuhitajiki kupanda, kuvuna na kuhifadhi?

3. Je, umegundua nini kuhusiana na ndege na chakula: je, wanakaa na kuacha kucharuko (wanyama wadogo) wawalishe? (Kwa hakika ndege wanatafuta chakula. Wanakifanyia kazi chakula chao.)

a. Kwa vile mara zote ndege wanafanyia kazi chakula chao, lakini hawapandi, hawavuni au hawahifadhi, je, tunapaswa kuhitimishaje kuhusiana na Mungu wetu na wasiwasi wetu kuhusu chakula? (Mungu aliwapatia wanadamu mpango wa kupanda, kuvuna na kuhifadhi. Aliwapatia ndege mpango wa siku zote wa kutafuta chakula. Vyovyote iwavyo vile katika mpango wa utekelezaji, wasiwasi sio sehemu ya mpango kwa sababu Mungu ndie chanzo chetu cha mwisho.)

D. Soma Mathayo 6:27. Je, ni ukweli kwamba hatuwezi kuongezea urefu wa maisha yetu? Hivi karibuni rafiki yangu alipatwa na ugonjwa wa kisukari kwa kuwa alikuwa mnene sana. Muda mfupi kabla ya hapo alikuwa akivuta sigara. Mwanangu (ambaye ni daktari wa watu) alisema “Anapaswa kuwa na wasiwasi kuhusiana na urefu wa maisha yake. Atoe miaka kumi kwa ajili ya kisukari na miaka mingine kumi kwa ajili ya uvutaji wa sigara.” Je, rafiki yangu hapaswi kuwa na wasiwasi? (Angalia kwa makini katika kile alichokisema Yesu: wasiwasi hautakufanya uishi maisha marefu. Pia, haitakufanya uwe mrefu zaidi au uwe na mwonekano mzuri. Hata hivyo, rafiki yangu ataishi maisha marefu kama atapungua uzito na kuacha kuvuta sigara.)

E. Soma Mathayo 6:28-30. Je, ni malalamiko gani ambayo unayasikia mara kwa mara kutoka kwa Wakristo wenzako kuhusiana na uvaaji wa watu wengine? (Baini kuwa Yesu hahukumu nguo nzuri. Anahukumu wasiwasi juu ya kuwa na nguo.)

1. Kumbuka mjadala wetu wa kipaumbele. Je, Yesu anasema nini zaidi ya uvaaji? (Kwa kuwa miili yetu ni ya muhimu kuliko nguo (Mathayo 6:25), Yesu anatuambia kuwa hatuhitaji kuwa na wasiwasi kuhusiana na miili yetu pia.)

F. Soma Mathayo 6:31-32. Je, dunia inajishughulishaje na uhitaji wa chakula, vinywaji na mavazi? (Wanavifanyia kazi kwa nguvu sana. Je, hii inakukumbusha jinsi nilivyosema ninajishughulisha na wasiwasi – kuifanyia kazi kwa bidii?)

G. Soma Mathayo 6:33. Je, Wakristo wanapaswa kujishughulishaje kwenye uhitaji wa chakula, vinywaji na mavazi? (Badala ya kukimbilia kutafuta fedha, tunahitajika kukimbilia kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Tunahitajika kuyaweka mbele maisha yenye haki. Hii haimaanishi kuwa hatufanyi kazi kwa bidii, inamaanisha kuwa na bidii yetu katika kuuendeleza ufalme.)

H. Soma Mathayo 6:34. Je, hii ni “mara moja moja?” au, je, hii ni “usipoteze furaha na utendaji mzuri wa siku kwa kuwa na wasiwasi kuhusu kesho?”

1. Tovuti ya Bible.org inatuarifu kutoka kwenye chanzo kisichojulikana kuwa wastani wa wasiwasi wa mtu unajielekeza kwenye: asilimia 40 vitu ambavyo kamwe havitatokea; asilimia 30 vitu ambavyo haviwezi kubadilishwa; asilimia 12 ukosoaji wa kizandiki wa watu wengine; asilimia 10 afya – ambao haitegemezwi na msongo; na asilimia 8 matatizo ya uhakika/ya kweli ambayo lazima yakabiliwe. Je, hii ni kweli kwa uzoefu wako?

a. Kama jibu ni “ndiyo,” je, ni muhimu kiasi gani kugandamiza Mathayo 6:34 kwenye hisia zetu!

I. Rafiki, inaonekana kuwa suluhisho la wasiwasi ni kumwamini Mungu. Anaweza asitatue tatizo katika kipindi cha maisha yetu, anaweza sifanye vitu kwa namna ambayo tungependa afanye, lakini kama tukiamua kuamini maamuzi yake, kama tukifanya kazi kuuendeleza Ufalme wake, hatuhitajiki kudhoofishwa kabisa na wasiwasi. Je, utadhamiria kumwamini Mungu?

IV. Juma Lijalo: Msongo.

Thursday, December 23, 2010

Robo ya Kwanza 2011 - Somo la 1: Hisia

Ndugu msomaji, juma hili tunaanza mfululizo mpya wa mwongozo wetu wa kujifunza Biblia katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2011 (Januari - Machi). Karibuni tuendelee kujifunza sote kwa uongozi wa Roho Mtakatifu.


Somo la 1: Hisia
(Wagalatia 5, Wakolosai 3, 2 Samweli 13)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, Biblia inaonekana kuwa mahala pazuri pa kujifunza kuhusu hisia za kibinadamu? Angalia Wagalatia 5:22-23 inayosema kuwa “tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema na kiasi. Je, ni mangapi kati ya hayo matunda aidha ni hisia au yanalinganishwa kwa karibu kabisa na hisia? Mtu yeyote aliyekwishasoma kitabu cha Robert Whitaker kinachoitwa Anatomia (Sayansi ya mwili) ya Magonjwa ya Mlipuko ana mashaka makubwa ya kuirejea sayansi katika kuponya matatizo ya kihisia na ya kiakili. Kitabu chake kinaelezea ukweli kuwa katika nchi ya Marekani tuna ongezeko kubwa la watu wanaodhoofishwa na hisia zililoanzia kwa kuanza kwa matumizi ya dawa katika kuponya matatizo ya kiakili. Hoja yake ni kwamba kutumia dawa za sasa ni kama kutupa mawe/miamba kwenye mitambo ya kisasa. Dawa ni kwamba tu zinafanya tatizo kuwa kubwa zaidi. Ikiwa sayansi yaweza kutoa majibu au la, mimi sina wasifu wa kuzungumzia hilo. Lakini hebu tuzame kwenye mfululizo wetu wa kujifunza ili kuona kuwa ni majibu gani yanapatikana kwenye Biblia!


I. Wajibu Wako Kwenye Hisia Chanya

A. Soma Wagalatia 5:16-17. Je, unateseka na mgogoro/mtafaruku wa kihisia? Je, mara nyingine hisia zako hazidhibitiki au sivyo ambavyo ungetaka ziwe?

1. Je, ni mgogoro gani ambao Paulo anatufundisha ulio uzoefu wa kila mwanadamu? (Paulo anatuambia kuwa asili yetu ya dhambi inataka kufanya jambo moja na Roho Mtakatifu anatutaka tufanye jambo jingine. Mambo haya mawili yapo katika mgogoro kiasi kwamba tunajikuta tukifanya mambo tusiyotaka kuyafanya.)

2. Je, nini kilicho ufunguo cha maisha sahihi? (Kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu.)

B. Soma Wagalatia 5:19-21. Katika orodha hii ambayo Paulo anaiita “matendo ya asili ya dhambi,” je, unaona hisia zozote? (Ndiyo.)

1. Je, mchanganyiko huu unapendekeza nini? (Unapendekeza kuwa hisia hasi ni sehemu ya asili yetu ya asili ya dhambi. Tunazipata bila kuziomba! Pili, inapendekeza kuwa hisia hasi zina aina fulani hivi ya muunganiko na matendo hasi.)

C. Soma Wagalatia 5:22-25. Tumejadili kwenye utangulizi kuwa hizi ni hisia au zinalinganishwa kwa karibu kabisa na hisia. Je, hizi ni hisia chanya, hisia ambazo ungetaka ziwe sehemu ya maisha yako?

1. Je, tunapataje hizi hisia? Au, je, zipo nje kabisa ya uwezo wa uchaguzi? (Uchaguzi ni kigezo. Kwanza, ni kigezo kwenye uchaguzi wetu wa “kuishi kwa mujibu wa Roho.” Pili, Paulo anatuambia kuwa tunaweza “kuisulubisha” asili yetu ya dhambi.)

2. Je, ni wangapi kati yenu mnapata ugumu kuishi kwa mujibu wa/kuendana na Roho na kuzisulubisha asili zenu za dhambi? (Kama wewe uko kama mimi, mkono wako umenyooshwa juu. Sina uhakika kwamba mafanikio ni rahisi, lakini nina uhakika kuwa Biblia inatufundisha kuwa uchaguzi ni kigezo katika hisia zetu za kibinadamu.)

D. Soma Wakolosai 3:5-10. Je, hisia ngapi hasi tunaziona ambazo zimeorodheshwa kwenye haya mafungu? (Kadhaa.)

1. Je, ni ushawishi gani tulionao dhidi ya hizi hisia hasi? (Paulo anatuambia “tujiweke mbali” nazo.)

E. Soma Wakolosai 3:12-14. Tunaona tena hisia chanya na pendekezo kuwa tuna ushawishi dhidi ya hisia zetu. Je, ni matendo gani mahsusi ambayo mafungu haya yanapendekeza ambayo tunaweza kuyafanya? (“Kuchukuliana” na “kusameheana.”)

1. Je, hizi ni chaguzi?

2. Baini kuwa Paulo anasema “upendo” utatufungamanisha kwenye umoja kamili. Je, tunaweza kuchagua kupenda? Au, je, hiyo ni hisia isiyodhibitika?

a. Hebu tuchukulie kuwa humpendi mtu fulani, lakini unataka kujifanya kumpenda. Je, unawezaje kulifanya hilo? (Utakuwa mwema kwa huyo mtu. Utakuwa mkarimu. Utamtendea mtu huyo kama ambavyo ungetaka kutendewa. Hiyo inaonekana kama “kuchukulia” na “kusamehe,” si ndio?)

(1) Je, hii ni tiba ya Kibiblia ya kutibu matatizo ya kihisia? (Kama wewe uko kama mimi, baadhi ya nyakati zangu za furaha sana ni pale ninapomsaidia mtu fulani naye anashukuru/anafurahia. Kuwa mwema na mwenye upendo kwa watu wengine ni kama ndege iliyojazwa mafuta kwa ajili ya hisia chanya. Kuwa mwema na mwenye kujali ni uamuzi. Hakupo nje ya utayari wa uhuru wa uchaguzi.)

II. Mfano wa Kibiblia

A. Soma 2 Samweli 13:1-2. Je, Amnoni anateseka na tatizo la kihisia? (Ndiyo. Ilimfanya augue kimwili.)

1. Soma Mambo ya Walawi 18:11. Je, fungu hili linasema nini kuhusu matamanio ya Amnoni? (Kwamba asingeweza kumwoa Tamari.)

B. Soma 2 Samweli 13:3-6. Je, Amnoni ana uchaguzi wa kufanya hapa kuhusu kuzilisha hisia zake hasi?

1. Je, hapa kuna usawia/ufananisho/uhusiano katika maisha yako? Je, unapambana na hisia hasi unazozilisha kwa chaguzi zako hafifu?

C. Soma 2 Samweli 13:9-11. Hadi kufikia hapa, je, ni chaguzi zipi mbaya ambazo Amnoni amezichagua? (Amedanganya ili kumleta Tamari katika chumba chake. Amemtoa kila mtu nje na sasa wapo yeye na Tamari peke yao. Sasa anaonekana kumlazimisha ili afanye nae ngono{amtenze/ambake}.)

D. Soma 2 Samweli 13:12-14. Je, hii dhambi ni ya bahati mbaya? Je, Amnoni ameonywa kikamilifu kuhusiana na asili ya dhambi yake? (Amnoni amekuwa akikimbilia kwenye aina zote za “taa nyekundu” kuelekea katika hii hatua ya chini. Ameruhusu hisia zake ambazo hakuziangalia kwa makini kuwa tabia mbaya ajabu.)

1. Soma tena Wakolosai 3:5. Je, badala yake Amnoni angetakiwa kufanya nini? (Paulo anasema kuwa hisia zilizosababisha kufikia katika hatua hii zinategemeana na uchaguzi wetu. Tuna uwezo wa “kuzifisha” hizi hisia.)

E. Soma 2 Samweli 13:15. Je, hapa Amnoni anateseka kutokana na matatizo ya kihisia?

1. Je, ni kwa kiasi gani sasa tunaweza kuona kwamba haya matatizo yanafungamanishwa na maamuzi yake mabaya?

F. Soma 2 Samweli 13:17-20. Je, hapa Tamari anateseka kutokana na matatizo ya kihisia?

1. Je, kuna kitu chochote ambacho angeweza kukifanya kwa utofauti ili kuepuka matatizo yake ya sasa ya kihisia? (Hapana.)

a. Je, mistakabali ya Amnoni na Tamari inatufundisha nini kuhusiana na ugumu/matatizo ya kihisia? (Baadhi ni matokeo ya chaguzi zetu hafifu, na baadhi yanakuja pasipo kuwa na kosa lolote tulilolitenda.)

G. Soma 2 Samweli 13:21-22 na 2 Samweli 13:28-29. Je, Absalomu anateseka kutokana na tatizo la kihisia?

1. Je, hili ni kosa lake?

2. Je, Absalomu angeweza kufanya nini ili kuepuka kuacha tatizo lake la kihisia kufikia hatua ya mauaji? (Wagalatia 5:20 inatuambia kuwa chuki/uadui ni sehemu ya asili yetu ya dhambi, na kuishi kwa mujibu wa Roho ni suluhisho la asili yetu ya dhambi.)

III. Maoni ya Yesu Juu ya Hisia

A. Soma Yohana 16:20. Kwenye somo letu la Biblia tumeona uhusiano/ulinganifu kati ya hisia njema na kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu. Je, fungu hili linapendekeza nini kuhusu huo uhusiano/ulinganifu? (Ulimwengu, unaodhaniwa kuwa hauishi kwa mujibu wa Roho, unafurahia wakati wale wanaoongozwa na Roho wanahuzunika.)

1. Chungua/changanua muktadha wa Yohana 16:20. Je, unatoa mwanga gani kwenye kauli ya Yesu? (Sababu ya huzuni ni kwamba Yesu atatiwa mbaroni hivi karibuni na kusulubiwa.)

a. Je, hii inapendekeza nini kuhusiana na hisia za Kikristo na kibinadamu? (Kwamba mazingira yaliyo nje ya udhibiti wetu yatatusababishia huzuni – wakati ambapo ulimwengu unafurahia uovu.)

B. Soma Yohana 16:21-22. Je, mwisho wa tumaini la matatizo yetu ya kihisia ni upi? (Ni ya kitambo kidogo. Ni ya msingi katika mwanga/muktadha wa ukweli kuwa Yesu atakuja tena kutupatia furaha!)

C. Soma Mathayo 26:36-38. Je, Yesu anateseka kutokana na hisia ipi?

1. Tunapochukulia kwamba Yesu aliteseka hisia hasi, je, tuhitimisheje kuhusu matatizo ya kihisia na dhambi? (Ugumu/matatizo ya kihisia yanaonekana kufanana na magumu/matatizo mengine. Kwa ujumla, kuishi maisha yanayoongozwa na Roho hutupatia hisia chanya. Kuishi maisha yanayoongozwa na asili yetu ya kibinadamu hutupatia hisia hasi. Hata hivyo, tunaishi kwenye ulimwengu wenye uovu ukiwa na watu waovu – na wanaweza kutusababishia kuteseka kihisia. Ni hadi hapo Yesu atakapokuja tena, ndipo matatizo yetu, yakijumuisha matatizo yetu ya kihisia, yatakapoponywa.)

D. Rafiki, je, utadhamiria hivi leo kuboresha afya yako ya kihisia kwa kumwomba Roho Mtakatifu akuongoze maishani mwako? Kwa nini usimwombe sasa hivi?

IV. Juma Lijalo: Mpango wa Mbingu Kuhusiana na Wasiwasi.

Thursday, December 9, 2010

Somo la 12: Gehazi: Kukosa Shabaha

(2 Kings 5, 5 & 8)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kama ningekuuliza kuwa lengo la maisha yako ni lipi, je, ungejibuje? Je, jibu lako litakuwa kuhusu kutenda wema? Kukuendeleza? Kuuendeleza Ufalme wa Mungu? Kukuendeleza wewe na Mungu? Katika somo letu la kujifunza Biblia juma hili tunawaangalia wale waliotenda wema bila kutarajia zawadi, na wale ambao walitarajia tu zawadi. Hebu tuzame kwenye somo letu!

I. Ukarimu

A. Soma 2 Wafalme 4:8. Hatujui jina la huyu mwanamke, kwa hiyo hebu tumuite “Sheri” Mshunami. Linganisha mustakabali wake na ule wa mjane tuliyejifunza juma lililopita? (Katika mistakabali yote miwili nabii (mara hii Elisha badala ya Eliya) anasimama kwa ajili ya kula. Tofauti ni kuwa Sheri ana mume, fedha na chakula anachokitumia kumbariki nabii.)


B. Soma 2 Wafalme 4:9-10. Kwa nini Sheri anafanya hivi kwa ajili ya Elisha? Anataka kuuendeleza Ufalme wa Mungu.)

1. Je, hii inapendekeza nini kwetu kuhusu kuwalipa watumishi wa Mungu? (Kuwa na kitu cha kujitegemea – kinyume na hisani za zimamoto – ndiko kunastahili.)


C. Soma 2 Wafalme 4:11-13. Unafikiria nini kuhusu nabii kutoa fadhila kutoka Serikalini?

1. Je, Sheri anajibuje kuhusiana na hiyo fadhila? (Hadhi yangu kwa Serikali ni nzuri tu.)

D. Soma 2 Wafalme 4:14. Elisha bado anataka kumtendea Sheri fadhila. Linganisha pendekezo la Gehazi na wazo la awali la Elisha? (Pendekezo la Gehazi linaonekana kuendana zaidi na kazi ya nabii.)

E. Soma 2 Wafalme 4:15-16. Je, tunaweza kuwa na uhusiano kama huo na Mungu kiasi kwamba tunaweza kuweka aina hizi za ahadi kwa watu wengine?

1. Sheri anaonekana kusema, “Hebu usinitanie kuhusu hili!” Je, anatania?

F. Soma 2 Wafalme 4:17. Kama Sheri angejua kuhusu matokeo haya mwanzoni mwa mahusiano yake na Elisha, je, angefikiria matendo yake kwa nabii kuwa ya maana? (Bila shaka. Sheri alikuwa mkarimu bila kutarajia thawabu. Mungu wetu Mkuu wa mbinguni alimbariki sana.)


II. Mgogoro

A. Soma 2 Wafalme 4:18-20. Mvulana huyu inawezekana alikuwa na tatizo alilozaliwa nalo lililojidhihirisha hivi sasa. Kwa nini Mungu anaruhusu jambo hili wakati ambapo Sheri alipewa kijana huyu kama ishara maalum ya shukurani?

1. Je, unadhani kuwa ingekuwa heri Sheri asingempata huyu kijana, kuliko kumpata na kuwa nae kwa miaka michache tu na kisha afariki?

a. Je, kauli yake ya “Usinitanie” inapendekeza jibu?


B. Soma 2 Wafalme 4:21-23. Linganisha mtazamo wa baba na Sheri kuhusu kuwasiliana na Elisha? (Mama alichukulia kuwa ni jambo la dharura – kwa hiyo aliamini kuwa Elisha anaweza kutenda jambo fulani. Baba alifikiria kuwa hii ilikuwa ni safari ya kawaida – hakuwa na matarajio ya msaada.)

1. Linganisha Sheri alivyofanya kufuatia kifo cha mwanae na jinsi ambavyo mjane tuliyemjifunza juma lililopita alivyofanya? (Yule mjane alijilaumu, alimlaumu Mungu na alimlaumu nabii. Sheri anamtafuta nabii kwa ajili ya msaada. Hebu na tuwe kama Sheri!)


C. Soma 2 Wafalme 4:24-26. Je, swali la Elisha linatuambia nini kuhusu jinsi ambavyo Sheri alipomkaribia? (Kujongelea kwake kulimwambia Elisha kuwa kitu fulani hivi kibaya kimetokea.)

1. Kwa nini Sheri anasema kuwa kila kitu kipo sawa?

D. Soma 2 Wafalme 4:27. Linganisha hisia za Elisha na hisia za Gehazi? (Elisha anakuwa makini zaidi. Anaangalia mbele zaidi ya maneno ya Sheri dhidi ya mwonekano wake.)

1. Je, ni mara ngapi unaonyesha hisia kama hizo kwa wale wanaokuzunguka?

E. Soma 2 Wafalme 4:28. Je, sasa Sheri anamlaumu Elisha? (Kwa kiasi fulani. Mtazamo wake ni kwamba hakuomba kwa ajili ya kumpata mwana – angeridhika bila kuwa na mtoto – bali kumpata mwana na kisha afariki angali kijana mdogo ilimuwia ugumu sana.)

1. Je, ni kitu gani chanya unachokiona kwenye matendo na maneno ya Sheri? (Anamgeukia Elisha kwa ajili ya kupata msaada. Sidhani kama Mungu anatutia hatiani kwa kusema aina ya vitu alivyovisema Sheri hapa.)

F. Soma 2 Wafalme 4:29. Je, ni imani kiasi gani aliyonayo Elisha kwa Gehazi?

G. Soma 2 Wafalme 4:30. Je, ni imani kiasi gani aliyonayo Sheri kwa Gehazi? (Anamtaka Elisha aende.)

H. Soma 2 Wafalme 4:31-35. Kwa nini fimbo haikufanya kazi? Kwa nini ilimpasa Elisha kujinyoosha juu ya mwili ya mvulana mara mbili? Je, hatua hizi zimekosewa au ni hatua za muhimu?

1. Hii inaonekana kama ni kurudisha fahamu bila kufikiria – je, hiyo inaweza kusaidia kwa mtu aliyefariki kitambo namna hii? Vipi kama kifo kilisababishwa kwa damu kuvujia kwenye ubongo? (Mimi sio mfizikia, lakini kupanua mapafu, kuchua moyo na kuupasha mwili joto kunaonekana kutotenda jambo lolote zuri katika kuufufua mwili.)

a. Je, hii inatufundisha nini kuhusu asili ya miujiza? (Mungu anatutaka tuwe sehemu ya miujiza yake – hata kama kile tunachokifanya kinaonekana kutokuwa na manufaa yoyote.)

I. Soma 2 Wafalme 4:36-37. Kazi umekamilika!
J. Soma 2 Wafalme 8:1-3. Je, utii umemtendea Sheri nini? (Umeiokoa familia yake na njaa, lakini nyumba zisizo na mpangilio zimejengwa nyumbani kwake!)

K. Soma 2 Wafalme 8:4-6. Kwa nini mfululizo wa haya matukio ulitokea? Kwa nini Sheri asipokee mbaraka uliofifilishwa? (Sheri na familia yake hawakuokolewa kutoka katika dhiki/taabu. Lakini, tunaweza kuona mkono wa Mungu ukifanya kazi hata katika kipindi cha dhiki. Kama mwana wa Sheri asingekufa na kufufuliwa kimiujiza, yawezekana Mfalme asingefanya vile katika kumtendea Sheri fadhila kuhusiana na shamba lake.)


1. Je, kuna somo gani hapa kwa ajili yetu? (Pambano kati ya wema na uovu linaendelea hapa duniani. Upatie nafasi ufanyaji kazi wa Mungu maishani mwako. Usihafifishe imani kwa sasa.)

III. Naamani

A. Soma 2 Wafalme 5:1-3. Je, nani anayewajibika kwa mafanikio ya Naamani maishani? (Mungu.)

B. Soma 2 Wafalme 5:9-11 na Warumi 13:7. Je, ilimpasa Naamani kuingia kwenye nyumba ya Elisha badala ya kukaa kwenye kibandawazi chake cha kukokotwa na farasi? Je, ilimpasa Elisha kutoka nje na kumsalimia?

1. Je, ulibaini kuwa Elisha hakuongea moja kwa moja na Sheri (2 Wafalme 4:13)? Kwanza alimtuma Gehazi kukabiliana na mwana wa Sheri aliyefariki (2 Wafalme 4:29). Je, hili ni suala la haiba? Je, hii ni kwa sababu Elisha anamwakilisha Mungu?

2. Je, kungekuwa na kosa gani kwa kufanya vitu kwa jinsi ambavyo Naamani alitarajia?

C. Soma 2 Wafalme 5:12. Je, ni kitu gani kingine kina makosa katika maelekezo ya Elisha? (Mantiki. Kama unataka kusafishwa kitu fulani, nenda kwenye mto msafi!)

1. Nini kinatokea kutokana na hili “shambulio” kwenye hadhi ya Naamani na mantiki? (Anaondoka kwa hasira.)

D. Soma 2 Wafalme 5:13-14. Tumekuwa tukiupatia mantiki uvumilivu. Je, ni mantiki gani inayotumiwa na wasaidizi wa Naamani? (Ungeweza kufanya jambo fulani kubwa/gumu, kwa nini sasa usifanye kitu kisichokuwa na mantiki na kisichokuwa na hadhi?)

1. Unadhani ni masomo gani Mungu anamfundisha Naamani? (Muujiza ulikuwa unajihusisha na uwezo wa Mungu. Haikuwa kitu ambacho Elisha alikuwa akikidai kwa mkono wake. Haikuwa kuhusu uthamani wa Naamani. Haikuwa kuhusu mantiki ya kibinadamu.)

2. Je, kuna kitu alichotakiwa kufanya Naamani? (Uaminifu na utii.)

3. Je, huwa unachanganya mantiki na uthamani kwenye maombi yako ya muujiza?

E. Soma 2 Wafalme 5:15-16. Kwa nini sasa Elisha anakutana na Naamani? (Jaribu limekwisha.)

1. Kwa nini Elisha anakataa zawadi? (Elisha hakustahili malipo kwa kazi ya Mungu.)

F. Soma 2 Wafalme 5:17-19. Je, Elisha anaweza kusamehe dhambi? Je, anaweza kuzisamehe kabla hazitatendwa? (Elisha anasema kuwa kwa mtazamo wa Naamani, hii sio dhambi.)

G. Soma 2 Wafalme 5:20-25. Je, Gehazi yupo kwenye kipimo kipi katika uaminifu na uadilifu?

H. Soma 2 Wafalme 5:26-27. Je, hii inaonekana kuwa adhabu ya haki kwa kudanganya kidogo na “kuvitwaa”?

1. Je, suala lipi ni la msingi kwenye dhambi ya Gehazi? (Kama jinsi ambavyo Elisha alivyomfuatia/alivyomrithi Eliya, kwa hiyo huenda Gehazi angekuwa nabii anayefuatia. Kilichomwondolea ustahili kilikuwa ni kujitafutia mambo yake mwenyewe. Sheri alimsaidia Elisha bila kujijali yeye mwenyewe. Katika uponyaji wa Naamani, uwezo wa Mungu ndio ulikuwa nguzo kuu, sio umuhimu wa Naamani au Elisha. Gehazi hakujali kuhusu mpango wa Mungu, alijali jinsi ambavyo mambo yalimtukia. Hiyo ilimwondolea ustahili wa kuwa nabii wa Mungu.)

I. Rafiki, vipi kuhusu wewe? Je, lengo lako la msingi ni kutenda wema na kuuendeleza Ufalme wa Mungu? Au, je, lengo lako la msingi ni kuyaendeleza mambo yako mwenyewe bila kujali kilicho sahihi? Je, utajitoa hivi leo kuwa mwenye bidii katika kutenda wema na kuuendeleza Ufalme wa Mungu?

IV. Juma Lijalo: Baruku: Kuandaa Urithi Katika Ulimwengu Unaovunjika.

Thursday, December 2, 2010

Somo la 11: Mjane wa Sarepta: Kuruka kwa Imani

(1 Kings 17)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Juma hili mke wangu asiye na mawaa aliniambia kuwa hataki nimnunulie kitu chochote kwa ajili ya Krismasi. Badala yake, alinitaka kutoa fedha hizo ambazo ni kwa ajili ya zawadi yake kwenye kituo chenye kuhitaji msaada kwa ajili ya kusaidia wenye shida. Fikara langu la haraka haraka lilikuwa ni “Nahitajika kufanya hilo pia.” Kisha nikaanza kupambana na hilo wazo nafsini mwangu. Vipi kuhusu wewe? Je, unapambana na ubinafsi? Ninadhani hivi sasa unauliza, je, ni ubinafsi kupokea zawadi wakati wa Krismasi? Swali zuri! Huenda jibu lina cha kujihusisha na dhana ya kama mahitaji yako tayari yametimizwa. Vipi kuhusu kuwasaidia watu wengine pale ambapo mahitaji yako yanakuwa hayajatimizwa? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kuona kile tunachoweza kujifunza kuhusu ubinafsi halisi!

I. Ukame

A. Soma 1 Wafalme 17:1-4. Kama Mungu anaweza kuzuia mvua kunyesha, je, anaweza kuwakimu wale wanaomfuata?

1. Jibu ni dhahiri, “ndiyo.” Sasa kwa nini tunapaswa kuwakimu wafuasi wa Mungu?

B. Soma 1 Wafalme 17:7-9. Je, Eliya alipaswa kufikiria kuwa Mungu alimwangusha pale kijito kilipokauka?

1. Kwa nini Mungu aliruhusu kijito kikauke?

2. Je, chakula cha Eliya kinachofuatia kitatoka wapi? (Anatakiwa kuondoka kwenda nje ya mji. Huko atalishwa na mjane.)


C. Soma 1 Wafalme 17:10-12. Hebu jiweke kwenye nafasi ya huyu mjane. Je, unaweza kuweka mahitaji ya mtu mgeni na usiyemjua dhidi ya yale ya mwanao au wewe mwenyewe?

1. Je, mjane ana wajibu wa kiroho kumpatia mwanae chakula kabla hajampatia mtu mzima aliye mgeni na asiyefahamika?

2. Nimemwita Eliya “mgeni.” Je, ukweli kwamba mjane anamtambua Eliya kama mfuasi wa “Mungu wako” unapendekeza kitu gani?


a. Je, unakumbuka kwamba Mungu alimwambia Eliya (fungu la 9) kuwa tayari alikwishafanyia kazi suala la kulishwa kwake na mjane? Je, unadhani kuwa mjane alikuwa na uelewa hapo kabla kumhusu Eliya?

(1) Kama Mungu alishafanyia kazi suala la “ulishwaji” na mjane, je, unachukuliaje kauli yake kwamba alidhani familia yake itakufa?

3. Je, unafikiria nini kuhusu mpango wa Mungu – kumfanya mjane mwenye njaa na mwanae kuwa njia ambayo nabii wa Mungu analishwa?


a. Hebu tuchukulie kwamba wewe ndiye mtu wa mwisho kabisa kanisani mwenye vigezo vya kufanya kazi fulani. Kanisa linapokuomba kufanya hii kazi, je, unapaswa kukataa?

II. Jaribu

A. Soma 1 Wafalme 17:13-14. Je, huyu mjane anaombwa kufanya kitu gani? (Kutoa sehemu ya chakula kwa ahadi ya kupata chakula cha kutosha katika siku zijazo.)

1. Je, ungekuwa wewe ungejisikiaje? Je, ungesema kuwa mjane na mwanae wanapaswa kula kabla ya mtume?

2. Je, ungesema kuwa kuomba chakula kutoka kwa mjane anayeteseka kwa njaa na mwanae haileti mantiki – Eliya anapaswa kwenda kwa mtu aliye kwenye nafasi nzuri ya kutoa msaada?

3. Je, ungesema kuwa mtumishi kiongozi kimantiki anapaswa kuwa wa mwisho kula?

4. Je, ungeweza kubaini (kutokana na somo la juma lililopita) kuwa manabii/mitume mara nyingine wanadanganya, na huyu hapa ana sababu kubwa ya kukudanganya?

5. Je, Mungu anatutaka kutoa kile kilicho dhahiri katika kubadilishana na ahadi ya kitu fulani kikubwa zaidi?

B. Soma 1 Wafalme 17:15-16. Je, nini matokeo ya imani ya huyu mjane? (Yeye na mwanae wanapata uzima!)

C. Niliwahi kujikuta katika tatizo kubwa pale washiriki wawili wa kanisa walipojihusisha katika suala la talaka pamoja na mashtaka kuhusiana na malezi ya mtoto. Mwenzi wa mshiriki mmoja alinionyesha nyaraka za kisheria (mahojiano) kutoka kwa mwenzi mwingine mshiriki zilizouliza kama yule anayeamini katika kulipa zaka kabla ya kulipia ankara ya umeme. Je, wewe ungejibuje hili suala? (Kujibu kwamba ungetoa zaka kwanza (huenda) kungeonyesha kuwa hukuwa mzazi mkamilifu. Nilikubali kuwa shahidi kwa mzazi ambaye angelipa zaka kwanza.)

D. Soma Luka 4:23-26. Kama mchungaji wa kanisa lako atakujia na pendekezo lililotolewa na Eliya, je, utakubaliana nalo?

1. Au, utamwambia mchungaji wako kuomba kwa ajili ya chakula kingi na mafuta mengi kwanza? (Yesu anapsema kuwa mara nyingine wafuasi wake wanasita sana kusonga mbele kwa imani inapotokea kuwepo kwa watu wanaowafahamu.)

a. Je, mara nyingine huwa tunazichukulia kwa urahisi njia na utendaji/mazoea ya kanisa letu kwa sababu tu tumeyazoea?

III. Thawabu ya Imani

A. Soma 1 Wafalme 17:17. Mungu alimwokoa huyu mvulana kutoka katika njaa kwa sababu ya imani ya mama yake. Kwa nini, baada ya yote hayo, sasa Mungu anaruhusu huyu mvulana kufariki?

B. Soma 1 Wafalme 17:18. Je, mjane anamlaumu nani kutokana na kifo cha mwanae? (Kwanza, yeye mwenyewe. Kisha Eliya halafu Mungu.)

1. “Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu?” Je, hivyo ndivyo tunavyofanya pale kitu kibaya kinapotutokea?


2. Je, Mungu yupo katika biashara ya kutukumbusha dhambi zetu na kuwaadhibu watoto wetu? (Linganisha Kutoka 20:5-6 na Ufunuo 12:10 na Yohana 16:7-11 na Ezekieli 18:20. Wakati mafungu haya yanaonyesha kuwa Mungu anatusadikisha dhambi zetu, ni kazi ya Shetani kutukumbusha na kutushtaki kuhusiana na dhambi zilizosamehewa. Kwa hakika Mungu kwa namna nyingine anawaadhibu watoto wa wale wanaomchukia, lakini anaahidi kuwa tunakufa tu kwa ajili ya dhambi zetu wenyewe. Kwa hiyo, mjane alikuwa akimshutumu Mungu kwa vitu ambavyo Mungu havifanyi.)

C. Soma 1 Wafalme 17:19-20. Je, ni mashtaka gani ambayo nabii wa Mungu anayaleta dhidi ya Mungu?

1. Hebu piga hatua nyuma kidogo na ujiweke katika nafasi ya Mungu. Je, ni kwa jinsi gani ungetaka haya mashitaka yote ya kutisha yakupishilie mbali?

a. Je, ni ya kweli?

D. Soma 1 Wafalme 17:21. Je, Eliya anadhani kuwa yeye ni mwenye haki zaidi na mwenye upendo kuliko Mungu? (Ndiyo. Hivyo ndivyo kwa hakika kabisa kauli yake na maneno yake yanapendekeza. Tunahitajika kukumbuka katika nyakati za umaarufu kuwa Mungu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Alikufa katika mateso makali sana ili kuichukua adhabu tuliyostahili. Kama wakati mwingine tunafikiri kuwa tuna upendo zaidi au tunaonyesha haki zaidi (hatuonyeshi upendeleo) kuliko Mungu – tunafanya makosa na tunamkashifu!)


E. Soma 1 Wafalme 17:22-23. Jiweke kwenye nafasi ya Mungu tena. Mama amekutuhumu kwa kumuua mwanae. Nabii wako kimsingi amesema kitu kile kile. Je, ungefanya nini katika hili ombi la kumponya mvulana ukichukulia mashitaka yaliyowekwa dhidi yako?


1. Je, Mungu hapaswi kuchoshwa kujithibitisha kwa uumbaji wake maskini/wenye ufidhuli?

2. Nimeipatia sehemu hii kichwa kisemacho “Thawabu ya Imani.” Je, kichwa hicho kinakaribiana na ukweli? (Nadhani Mungu anatatizwa kidogo kuliko ambavyo tunaweza kutatizwa kuhusiana na utoaji-majina. Sababu ikiwa kuwa uitaji majina unaakisi imani kwamba Mungu yupo madarakani/katika umiliki. Kile anachokichukia Mungu ni pale tusipomjali au kuamini kuwa Mungu hana mamlaka au uwezo katika dunia.)


F. Soma 1 Wafalme 17:24. Unafikiria nini kuhusu hii kauli?

1. Kumbuka kwamba huyu ni mwanamke ambaye, yeye pamoja na mwanae, aliokolewa kutoka katika janga la njaa kutokana na tendo lake la imani na muujiza wa Mungu!

G. Rafiki, somo letu linatukumbushia hali yetu ya ubinadamu. Mara nyingine tuna uwezo mkubwa wa matendo ya imani. Halafu baada ya Mungu kuonyesha uwezo wake kwetu kwa wazi kabisa, katika dhahama inayofuatia tunamtilia shaka na kumtuhumu kwa mambo mabaya kabisa. Je, utachukua muda kidogo hivi sasa, na kufikiria kuhusu nyakati ambazo Mungu alikuongoza na kukubariki kwa wazi kabisa? Je, utaahidi, hivi sasa, kutosahau kamwe kile alichokifanya Mungu na kamwe kutomtilia shaka katika siku zijazo?

IV. Juma Lijalo: Gehazi: Kukosa Shabaha.