(1 Wafalme 17-19)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, misongo yote ni mibaya? Najua kuwa msongo mkubwa kupita kiasi unanifanya niweze kuugua kirahisi. Kwa upande mwingine, misongo mingine inanifanya niweze kufanya kazi kwa ufanisi. Inapokuja suala la kutoa mhadhara, misongo mingine inanifanya niweze kuzungumza vyema zaidi. Msongo mkubwa kupita kiasi unaufanya ubongo wangu kuwa rojorojo. Hebu tukubaliane kuwa msongo mkubwa kupita kiasi sio mzuri kwetu. Je, unajihisi kuwa una msongo mkubwa kupita kiasi? Fikiria msongo aliokuwa nao baba yangu (na wengine wengi kama yeye) katika kipindi cha uhai wake kwenye ukanda wa mapigano wakati wa Vita vya Pili vya Dunia! Kamwe sikuwahi kufikiria kuwa kama ningeshindwa kesi mahakamani mtu fulani anaweza kuniua! Kama unahisi kuwa unateseka na msongo mkubwa kupita kiasi, fuatana nami tunapoendelea kubaini kile ambacho Biblia inakwenda kutufundisha kuhusu kukabiliana na msongo!
I. Msongo Dhidi ya Wasiwasi
A. Juma lililopita tulijadili kile ambacho Biblia inakisema kuhusu wasiwasi (dukuduku). Je, msongo na wasiwasi ni kitu kimoja?
1. Kama sivyo, je tofauti ni ipi?
2. Kama havifanani, je, vinapishana? (Kwa hakika, wasiwasi unasababisha msongo. Kwa muktadha huo vinapishana. Lakini, kama tulivyojadili juma lililopita, kwa ujumla wasiwasi (dukuduku) unahusianishwa na kitu ambacho hakijatokea (na huenda kabisa hakitatokea). Msongo ni shinikizo unalohisi pale ambapo kitu fulani hivi chenye mkasa kinapotokea.)
B. Kama kitu kibaya hakikutokei hivi sasa, je, msongo unaouhisi ni wasiwasi tu? (Juma lililopita tulijifunza kuwa kumwamini Mungu ni suluhisho bora zaidi la wasiwasi.)
II. Eliya na Msongo wa Ujumbe
A. Soma 1 Wafalme 17:1-4. Jiweke kwenye nafasi ya Eliya. Je, Eliya anakabiliana na msongo au wasiwasi?
1. Je, unalinganishaje kazi ya Eliya katika kipimo cha msongo? (Ahabu alikuwa mfalme. Eliya alikuwa anakabiliana na mfalme kwa kuwasilisha habari ambazo Ahabu asingezipenda.)
2. Kama ungekuwa kwenye nafasi ya Eliya, je, msongo wako ungekuwa mkubwa kwa sababu kwa hakika ulikuwa na wasiwasi? (Baini kuwa Mungu alimwambia Eliya “ajifiche” baada ya kufikisha ujumbe kwa mfalme.)
3. Je, ni viongozi vipi vya msongo ambavyo Mungu alimpatia Eliya? (Alimpatia ishara kuwa alikuwa pamoja nae. Katika kuelezea dukuduku (wasiwasi) kuhusiana na siku zijazo, Mungu alimpatia Eliya maelekezo juu ya sehemu ya kujificha. Alimwambia Eliya jinsi ya kuepuka msongo wa ukame kwa kumpatia maelekezo kuhusu chakula na maji.)
4. Je, hii inapendekeza nini kuhusiana na msongo maishani mwetu? (Ya kwamba tutakabiliana nao. Lakini kama ilivyo kwa wasiwasi, kumwamini Mungu kunatupatia nafasi ya kuzuia msongo wetu.)
B. Soma 1 Wafalme 18:1. Je, hii ingekua na msongo zaidi au msongo kidogo kuliko alivyokutana na Ahabu mara ya mwisho? (Kwa upande mwingine, Ahabu alikuwa na sababu lukuki za kumdhuru Eliya. Kwa upande mwingine, uzoefu wa jinsi Eliya alivyokabiliana na Ahabu mara ya kwanza na uzoefu wa ulinzi wa Mungu unapaswa kupunguza kiwango cha msongo. Na kwa kuongezea, Eliya alikuwa anawasilisha habari njema mara hii.)
1. Je, kuna chochote cha kujifunza kwetu kutokana na hili jambo hivi leo? (Kama unataka kujisikia kuwa na msongo kidogo kuhusiana na kitu fulani, fanya mazoezi ya kukabiliana na msongo. Msongo unaotokana na kutoa mihadhara unapungua kutokana na uzoefu wa kutoa mihadhara. Hii inajumuisha kufanyia mazoezi kile unachotaka kukiwasilisha kwa watu.)
C. Soma 1 Wafalme 18:2-4. Tunajifunza kuwa Obadia ni mfuasi wa Mungu. Je, yeye yu mgeni wa msongo? (Kupingana na Malkia Yezebeli kwa kuwaficha manabii kunaonekana kuwa na msongo.)
D. Soma 1 Wafalme 18:7-9. Je, ni kazi yenye msongo kiasi gani anayopewa Obadia? (Anadhani kuwa kazi hiyo itamgharimu maisha yake.)
1. Je, Obadia anakabiliana na msongo au wasiwasi?
2. Je, unadhani Obadia anafikiri kuwa sababu ya Eliya kumpatia kazi yenye msongo ni ipi? (Amefanya jambo fulani hivi baya. Hiyo ni ishara ya wasiwasi.)
a. Je, wewe u kama Obadia katika muktadha huu?
E. Soma 1 Wafalme 18:10-14. Tafakari kauli ya Obadia. Nini kinachofanya msingi wa msongo wake? (Wasiwasi. Anadhani kwamba Mungu ataendelea kumficha Eliya dhidi ya Mfalme Ahabu. Lakini, Mungu hatamwepusha na adhabu ya mfalme.)
1. Baini kuwa Obadia anajitegemeza kwenye matendo yake mazuri. Anatoa hoja kuwa Mungu anapaswa kumlinda kwa sababu amewaokoa/amewalinda manabii wa Mungu. Je, hivi ndivyo tunavyopaswa kumkabili Mungu kwenye hali za misongo? (Kama kweli Mungu anakupenda, je, anahitaji kushawishiwa ili atende jambo sahihi kwa niaba yako?)
F. Soma 1 Wafalme 18:15. Hii inatuliza msongo wa Obadia. Je, unadhani mazungumzo ya Obadia yanaweza kufanya nini kwenye kiwango cha msongo cha Eliya? (Kama Obadia, mshirika wa karibu wa Mfalme Ahabu, aliamini kuwa maisha yake yangekuwa hatarini kwa kutomleta Eliya, fikiria kama Ahabu angemkamata Eliya?)
G. Soma 1 Wafalme 18:16-18. Je, Eliya anaonekana kuwa mwenye msongo?
III. Eliya na Msongo wa Mpambano
A. Soma 1 Wafalme 18:19-21. Je, umewahi kuwa mahakamani? Je, umewahi kuwa katika mpambano ambao sehemu kubwa ulikuwa hatarini? Je, umewahi kushindana/kupingana na nguvu za giza hadharani? Je, masuala haya yana msongo kwa kiasi gani?
1. Je, unadhani kuwa maisha ya Eliya yangetwaliwa kama angepoteza hili pambano?
2. Je, watu wapo upande wa Eliya? (Watu “hawakujibu neno lolote.” Wanasubiri kuona kile kitakachotokea. Eliya hana mtu yeyote anayejitokeza kumsaidia.)
B. Soma 1 Wafalme 18:22-24. Linapokuja suala la msongo maishani mwako, je, kuna haja ya kujali uwingi? (Mmoja dhidi ya 450 (au 850) haionekani kuwa jambo zuri.)
C. Soma 1 Wafalme 18:25-26. Kwa nini Eliya atake upande mwingine uanze kwanza? Je, hii ni kwa sababu wao wapo wengi? (Eliya aliwataka wao waanze kwanza kwa sababu ana uhakiwa wa matokeo.)
1. Je, manabii wa Baali wanajisikia kuwa na msongo?
D. Soma 1 Wafalme 18:27-29. Je, ni sahihi kuongezea msongo kwa wasioamini?
1. Kuwafanya wapinzani wangu waonekane wapumbavu ni mfumo wa hoja yenye ufanisi sana. Soma Luka 6:35 na 1 Petro 3:15. Je, matendo ya Eliya yanaendanaje na ushauri wa Yesu kwa Petro? (Ninapambana na hili. Siku za hivi karibuni, niliandika kwenye tovuti ambapo niliwadhihaki wale wanaosuta/wanaoshambulia imani yangu. Hata hivyo, ninahisi kuwa kuwafanyia dhihaka viongozi wa nguvu za giza ni tofauti na kuwadhihaki wale ambao wameanguka dhambini tu.)
E. Soma 1 Wafalme 18:30-35. Je, unadhani kuwa Eliya alikuwa anateseka kutokana na msongo wowote kwa sababu ya wasiwasi? (Hapana! Huyu ni mtu jasiri.)
F. Soma 1 Wafalme 18:36-39. Je, lengo la Eliya ni lipi katika huu mkabiliano wa muhimu wa msongo? (Kumpatia Mungu utukufu.)
1. Unadhani hii ina athari/matokeo gani kwenye msongo? (Kama lengo letu ni kumpa Mungu utukufu, badala ya kujipatia utukufu sisi wenyewe, viwango vya msongo wetu vitakuwa chini zaidi.)
G. Soma 1 Wafalme 19:1-4. Je, huku ni kujichosha? Kukabiliana ukabiliano wenye mantiki kwenye msongo mkubwa sana kupita kiasi? (Ninafurahi kwa kuwa hili limo katika Biblia. Maisha ya Eliya yalikuwa hatarini kwa miaka kadhaa. Yumkini alikuwa na msongo mkubwa hapa kwa sababu alikuwa amewaua manabii wa uongo. Sababu iwayo yoyote ile, tunaona kuwa hata wale wanaotenda mambo makubwa kwa ajili ya Mungu mara nyingine wanashindwa kumwamini Mungu kikamilifu.)
H. Kama unapenda kusoma aya chache zinazofuatia, utaona kuwa Mungu alimjia Eliya ili kumtia moyo/kumfariji. Soma 1 wafalme 19:19-21. Je, ni msaada gani anaoufanya Mungu kwa ajili ya Eliya ili kumsaidia kutokana na msongo? (Anampatia msaidizi.)
IV. Yesu na Msongo
A. Je, unaweza kufikiria maisha ambapo uliwaponya watu na kuwafundisha watu kuhusu Mungu wakati wote? Je, hiyo itakuwa na msongo? (Kuwaponya watu kutakuwa ni jambo la furaha kupita kiasi! Ninapenda kufundisha kuhusu Biblia.)
1. Sasa je, ni msongo gani anaokabiliana nao Yesu?
B. Soma Mathayo 12:13-15. Je, ni msongo gani anaokabiliana nao Yesu katika uponyaji? (Msongo wa Eliya ulikuwa ni mpambano na nguvu za uovu. Hiyo inatupatia mtazamo mdogo wa kiwango cha msongo aliokuwa nao Yesu kwa sababu alikuwa katikati ya pambano/vita kati ya wema na uovu.)
C. Soma Luka 5:15-16. Je, unajisikia kuwa na msongo au hatia kwa kutokamilisha mambo yote mazuri uliyohitaji kuyafanya? (Fungu hili linavutia sana. Yesu aliamua kutenga muda kwa ajili ya maombi binafsi badala ya kuponya. Hii inaonyesha kuwa hata wale wanaofanya kazi za muhimu sana wanapaswa kutenga muda wa kuachana na kazi hizo na kutafuta nguvu mpya.)
D. Rafiki, je, unajihisi kuwa na msongo? Kama kwa kumwamini Mungu unaondoa wasiwasi ambao ni sehemu ya msongo, je, ni msongo kiasi gani utasalia? Kwa kile kinachosalia, kwa nini usikitibu kwa imani na kuwa na nyakati tulivu na Mungu?
V. Juma Lijalo: Mahusiano
Wednesday, January 12, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment