Thursday, January 13, 2011

Somo la 4: Mahusiano

(Luka 14, Waefeso 4, Warumi 2, 1 Petro 3)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mwanzoni kabisa mwa Biblia tunaona Mungu anasema “si vema mtu awe peke yake.” Mwanzo 2:18. Katika hiyo kauli Mungu anaonekana kuelezea suala la mahusiano. Hata hivyo, ni mara ngapi unaona kwamba kuwa na mahusiano na watu wengine, na si kuwa peke yako, kunasababisha matatizo mengi? Je, Biblia inatufundisha nini kuhusu mahusiano? Je, kauli ya Mungu kuhusu wanadamu kutokuwa peke yao ina maana ya ndani zaidi? Hebu tuzame kwenye somo letu na kujifunza kile ambacho Biblia inafundisha kuhusu mahusiano!

I. Njia ya Kuelekea Kwenye Heshima

A. Soma Luka 14:7. Je, unapenda kuheshimiwa? Je, heshima ni mojawapo ya malengo yako maishani?

1. Kama hawa watu wangekuwa wanakula peke yao, kusingekuwa na tatizo, sawa?

2. Jiweke kwenye nafasi ya mmojawapo wa wageni. Ukweli kwamba umechagua sehemu ya “heshima” inasema nini kuhusu mtazamo wako kuhusu baadhi ya wageni wengine? (Unadhani kuwa hawana umuhimu mkubwa/sio wa muhimu sana.)

B. Linapokuja suala la biashara, je, unatafuta kuwa kwenye nafasi ya juu?

1. Je, hiyo inamaanisha kuwa wewe ndie una vigezo vikubwa kabisa, au unatafuta nafasi ya juu kwa sababu nyinginezo?

2. Je, ulimwengu unapendekeza nini kuhusu kutafuta hadhi/staha, heshima na mafanikio?

3. Kama hautafuti kuheshimiwa, kuwa na hadhi na mafanikio, je, wewe u mvivu? Je, unapungukiwa na motisha?

C. Soma Luka 14:8-9. Je, kuna mantiki gani dhidi ya kukalia kiti kisichokuwa na umuhimu mkubwa? Kwa sababu tu wewe sio mtu wa umuhimu mkubwa haimaanishi kuwa wewe ni mtu mwenye umuhimu mdogo katika sherehe ya harusi, sawa?

D. Soma Luka 14:10. Je, unadhani ni jambo gani zuri Yesu analojaribu kutufanyia? (Anatupatia vidokezi (taarifa za ndani) vya kutusaidia kuepuka kudhalilishwa. Anatoa mwelekeo wa kuheshimiwa.)


1. Kama hatukuambiwa kuwa kukalia kiti chenye umuhimu mdogo ilikuwa ni ‘njia ya siri” ya kuheshimiwa, je mtu yeyote tofauti na yule ambaye kwa dhahiri hana umuhimu angefanya hivyo?

2. Je, ni kwa jinsi gani kwa mantiki ya kawaida mtu ataamua mahali pa kukaa? (Ungejipima wewe mwenyewe dhidi ya watu wengine. Yesu anatuambia kuyaangalia mahitaji ya watu wengine kwanza – sio kuweka madai yetu mbele.)


3. Je, unadhani kuwa katika uhalisia maishani mwenyeji anajali kuhusiana na mahali unapokaa na hivyo aje na kukupandisha hadhi? (Mungu wetu ndie Mwenyeji, na anajali.)

E. Soma Luka 14:11. Kwa nini hii ni kweli? (Kujikweza wewe mwenyewe kunaonyesha msingi wa kujipenda kwako. Kuwa mnyenyekevu kunaonyesha msingi wa kuwajali watu wengine.)

1. Kama uko makini na kufuatilia ushauri wa Yesu kwa sababu unataka kufurahia hadhi, kwa sababu unataka kuinuliwa/kukwezwa, je, hiyo inaonyesha kuwa wewe si mnyenyekevu?

a. Je, Yesu anapendekeza kuwa tunapaswa kuonekana kuwa wanyenyekevu, lakini si wanyenyekevu kiukweli?

F. Soma Waefeso 4:1-3. Je, unadhani Paulo anamaanisha nini anapotuambia tuwe na “unyenyekevu wote?” Je, mtu mwenye unyenyekevu wote anaweza kuwa na mpango wa siri wa kutaka kuheshimiwa na kukwezwa?

G. Soma Warumi 2:7. Je, nini lengo la watu waliotajwa hapa? (Utukufu, heshima na kutokuharibika!)

H. Soma Warumi 2:8. Kama unatafuta utukufu na heshima, je, haujitafutii mambo yako mwenyewe?

I. Soma Warumi 2:9-11. Je, hii inapendekeza nini kuhusu kama tunapaswa kutamani kuheshimiwa? (Kuwa na matamanio ya utukufu na heshima kunaendana na kuwa Mkristo. Kama isingekuwa hivyo, Yesu na Paulo wasingevitaja kama thawabu. Swali ni kuwa, tunafanyaje katika kuupata utukufu na heshima?)

II. All Hat, No Cattle

A. Soma Mathayo 23:5-7. Kama ningekuambia kuwa ungeweza kupata heshima kwa kuwa na “phylactery” (pochi ndogo) pana na "kishada" kirefu, je, ungejua kile ambacho ungepaswa kukifanya? (Phylacrery ni pochi ndogo iliyo na maandiko kutoka kwenye Biblia. Vishada vilimanisha kuwakumbusha watu kuhusu maneno ya Mungu yaliyomo kwenye Biblia (angalia Hesabu 15:39). Kishada kirefu kilimaanisha kuwa kwa hakika mtu alikuwa anamsikiliza Mungu kwa ukaribu.)

B. Wengi wenu mnasoma haya kwenye tovuti ya "GoBible.org" Je, watu wenye phylactery (pochi) kubwa, kishada kirefu hawaiendelezi Biblia? Je, huo si umuhimu wa
"GoBible?"

C. Je, nini kilicho kitu cha kisasa kinachoendana na phylactery (pochi) na kishada kirefu? (Biblia kubwa inayong’aa.)

1. Je, vipi kuhusu Biblia kubwa ya familia, yenye vumbi, iliyowekwa kimashuhuri nyumbani?

2. Je, watu wa aina hii wanalipa heshima neno la Mungu? (Wanajitangaza kuwa wanaijali sana Biblia kuliko watu wengine.)

a. Je, hivyo ni vibaya?

3. Je, vipi itakuwa bora zaidi? (Kuonyesha unaijali Biblia kwa kutii – kuwaweka watu wengine mbele/kuwapa kipaumbele. Walikuwa kama mwonekano (hat), sio kitu (ng’ombe.))

D. Soma Mathayo 23:8-12. Je, nini ulio mwelekeo wa kukwezwa? (Unafanikiwa katika hilo kwa kuwatendea watu wengine kwa unyenyekevu, kwa kutokalia kiti bora kabisa, kwa kukubali/kutwaa jina lililokwezwa au kwa kuwa na Biblia inayong’aa.)

E. Soma Waebrania 5:4-5. Fikiria kile kisa chetu cha awali kinachohusu mwenyeji wa sherehe ya harusi kukuita kwenye nafasi ya juu. Je, nini wajibu wetu katika kutafuta utukufu na heshima? (Utukufu na heshima vinaendana na Ukristo. Kudai utukufu na heshima haviendani na Ukristo. Kama tukiwatumikia watu wengine kwa unyenyekevu, Mungu atatufanya tuheshimiwe.)

1. Je, tumekwenda nje kabisa ya mada? Je, muktadha huu unasaidiaje masuala ya mahusiano? (Haupo katika ushindani na wafanyakazi wenzako, marafiki zako na wanafamilia wenzako kuutafuta utukufu. Upo katika ushindani na watu wengine kuona kuwa nani anaweza kuwa wa msaada zaidi!)

III. Malipo

A. Soma 1 Petro 3:8. Je, hii inaendanaje na suala la kuwatumikia watu wengine kwa unyenyekevu? (Inatuambia tuwe wanyenyekevu. Lakini, muhimu zaidi, huruma, upole na upendo vinaonyesha kuwa tunaweka matamanio yetu ya kibinafsi pembeni na kuangalia mahitaji ya watu wengine.)


1. Hebu turejee kwenye utangulizi kidogo. Mungu aliposema “si vema mtu awe peke yake” (Mwanzo 2:18), je, alikuwa anazungumzia tu kuhusu ndoa? (Hapana. Kama tupo peke yetu, tunafikiria kuhusu mahitaji yetu tu. Tunapokuwa katika uhusiano, tunafikiria kuhusu mahitaji ya watu wengine.)

B. Soma 1 Petro 3:9 na Mambo ya Walawi 24:19-20. Je, Mungu amebadili wazo lake? Anasema katika Malaki 3:6 kuwa hana kigeugeu! (Sidhani kama Mungu anatufundisha kuhusu haki katika 1 Petro 3, anatufundisha kuhusu mahusiano. Kuwajali watu wengine kupo juu ya haki. Haki ni muhimu kwa jamii (Warumi 13:3-5), lakini linapokuja suala la mahusiano binafsi, haki inachukua nafasi ya nyuma.)

C. Soma 1 Petro 3:12-13. Kama tuna huu mtazamo wa kujitoa nafsi kuhusu mahusiano, je, tutateseka kutokana na mambo yasio ya haki? (Fungu hili linatupatia uhakikisho wa aina mbili. Kwanza, Mungu anapingana na waovu. Pili, asili ya mambo ni kwamba kama unatamani kutoa msaada, watu watakuwa wema kwako.)


D. Soma Luka 17:1-4. Linapokuja suala la kupingana na dhambi, je, tuanzie wapi? (Tunaanza na sisi wenyewe! Yesu anasema “jichunge!”)

1. Je, Yesu anapendekeza kuwa tulinganisheje “hakuna kulipiza” na msamaha dhidi ya dhambi inayoendelea? (Kuyaangalia mazuri ya watu wengine bila ubinafsi haimaanishi kuwa tupo kimya kuhusu dhambi. Baini hatua za msamaha: 1) Kemea dhambi; 2) Mtu aliyekemewa anatubu; na 3) Unasamehe – bila kikomo.)

E. Soma Mathayo 5:23-24. Je, ni mtu gani aliye na kinyongo? (Mtu asiyekuwa madhabahuni!)

1. Tunapaswa kulielewaje hili – tunahitaji kupatanishwa na watu wasiotupenda?

2. Miaka kadhaa iliyopita fungu hili lilinifanya kujaribu kupatana na mtu aliyeonekana kunichukia kwa sabau nilikuwa ninakemea dhambi. Je, hicho ndicho ambacho fungu hili linamaanisha? (Ulikuwa mchakato unaouma sana. Nilijifunza kuangalia/kuchukulia mambo kutokana na mtazamo wa mtu aliyekemewa. Mtu aliyekemewa alinichukia kidogo, lakini bado hakuwa tayari kuwa rafiki yangu. Manufaa ya juhudi zangu yalikuwa kwamba wanafamilia sasa waliona ukweli kwa wazi zaidi na walivutwa zaidi kuja kwangu na kanisani. Sasa ninafikiri kuwa fungu hili linaelekezwa kwenye hali ambapo mtu na madhabahu vimefanya jambo baya.)

F. Rafiki, ninatumaini kuwa hadi hivi sasa unaona Biblia inafundisha kuwa kutokuwa wabinafsi, kuyaangalia mazuri ya watu wengine (badala ya mambo yako mwenyewe mazuri) ndio ufunguo wa mahusiano mazuri. Je, utakiri na kutubu kuhusiana na mtazamo wako wa ubinafsi na kumwomba Roho Mtakatifu akujaze roho ya kutokuwa na ubinafsi?

IV. Juma Lijalo: Hatia.

0 comments:

Post a Comment