Sunday, January 23, 2011

Somo la 5: Hatia

(Mwanzo 3 & 4, 1 Yohana 3)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mmojawapo wa marafiki zangu wa karibu kabisa alitumia miaka mingi kupata matibabu ya kisaikolojia ili aweze kutokomeza hatia. Kwa kuwa rafiki yangu hakuwa tena na mwenendo wa Kikristo, nilipomwona nilimwambia kuwa “hatia ni njema,” linapokuja suala la Mungu kuhangaisha mioyo yetu kuhusiana na mitazamo yetu na tabia zetu. Hatimaye, rafiki yangu aliamua kuwa ni vema kwake yeye kuniondoa katika sehemu ya maisha yake. Unafikiriaje, je, hatia ni njema au mbaya? Ufunuo 12:10 inamwita Shetani mshitaki wa ndugu zetu. Je, nilikuwa nafanya sehemu ya Shetani? Dhamiri yako inapokuhangaisha, je, unaweza kuichukulia kama majaribu ya Shetani ya kukukatisha tamaa? Au, je, ni Roho Mtakatifu anayekuita ili ufanye toba? Hebu tuzame kwenye Biblia yetu na kuona kile inachotufundisha kuhusu hatia!

I. Hatia Kama Rafiki

A. Soma Mwanzo 3:5-7. Je, Shetani alikuwa sahihi aliposema kuwa kula tunda kungemfanya Hawa kuujua uovu?

B. Soma Mwanzo 3:8. Kwa nini Adamu na Hawa walijificha ili Mungu asiwaone? (Walijisikia hatia.)

1. Hebu tuchunguze hili zaidi kidogo. Hawa alitaka kufahamu kuhusu uovu, lakili alipoujua alijisikia hatia na akajificha Mungu asimwone. Je, ni lengo gani lililofanywa na hatia katika huu muktadha: lengo jema au lengo baya?

a. Je, hatia ingetenda jambo gani kama ingejidhihirisha yenyewe kabla Hawa hajala tunda?

C. Soma Mwanzo 3:9-11. Kama hatia ni kitendo cha Mungu kukabiliana na sisi kuhusiana na dhambi zetu, tuna mapazia yaliyofunuliwa katika kisa hiki na kwamba tunaweza kuona jinsi hii inavyofanya kazi. Je, Mungu anafanya nini kukabiliana na Adamu dhidi ya dhambi yake? (Anaitaja dhambi mahsusi.)

D. Soma Mwanzo 3:12. Je, Adamu ametubu dhambi yake? (Anawalaumu Mungu pamoja na Hawa!)

E. Soma Mwanzo 3:13. Je, Hawa ametubu dhambi yake?

F. Je, ni lengo gani chanya (Mungu kukabiliana nasi kuhusiana na dhambi yetu) linalotimizwa na hatia? (Lengo ni kutufanya tuifikilie toba na kukiri dhambi.)


II. Hatia Kama Adui

A. Soma Mwanzo 4:8. Adamu na Hawa waliposikia kuwa Kaini alimuua Habili na kwamba Kaini alitimuliwa/alifukuzwa, je, unadhani walijisikia hatia?

1. Je, walipaswa kujisikia hatia?

a. Je, katika huu muktadha, hatia ilikuwa njema au mbaya? Yaani, je, hisia za hatia zinaishia kwenye jambo lolote jema?

B. Soma Ufunuo 12:10. Je, ni nani aliye mshitaki wa watu wa Mungu? (Usomaji wa hii sura nzima unafunua kuwa Shetani ndiye mshitaki.)

1. Je, mshitaki amepelekwa wapi? (Ametupwa chini duniani na malaika waliomfuata/waliomtii.)

2. Je, hiyo inapendekeza nini kuhusu shughuli za sasa za Shetani? (Ya kwamba Shetani na malaika wake bado wapo kwenye harakati za kutushitaki kuhusu dhambi zetu.)

C. Soma Zakaria 3:1-2. Je, ni wajibu gani tunaouona hapa kwamba Mungu na Shetani wapo kwenye harakati za kushitaki? (Shetani anashitaki na Mungu anatetea.)


D. Soma Wakolosai 1:21-22. Tumejifunza kuwa hatia inaweza kutusaidia tukiri na kuigeukia dhambi. Pia tumejifunza kuwa hatia ni nyenzo ya Shetani. Je, Wakolosai inatuambia kuwa ujumbe wa injili ni upi? (Kwamba kukubali kifo cha Yesu kwa ajili ya dhambi zetu kunatuweka huru sio tu kutoka dhambini, bali “kutoka kwenye mashitaka.”)

III. Dhamiri na Hatia

A. Soma 1 Yohana 3:19-20. Je, inamaanisha nini kwa moyo wako “kutulizwa” au moyo wako kukuhukumu? (“Kutulizwa” kunamaanisha hakuna hatia, “kuhukumu” kunamaanisha unajisikia mwenye hatia.)

1. Tumejifunza kuwa msamaha wa dhambi unatuweka huru dhidi ya mashitaka, lakini je, vipi kama dhamiri zetu bado zinatutaabisha? Je, Mungu au Shetani anaongea nasi?

a. Je, dhamiri zetu hazidhibitiwi na Roho Mtakatifu?

2. Je, unadhani fungu la 20 linamaanisha nini linaposema kuwa “Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu?” (Hii inapendekeza kuwa tunaweza kuwa na dhamiri hafifu – dhamiri isiyoakisi mapenzi ya Mungu.)

B. Soma 1 Yohana 3:21-24. Je, tunapataje dhamiri iliyoumbwa sawaswa? (Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.)

1. Kama tuna dhamiri iliyoumbwa sawasawa, je, hatia ina wajibu gani maishani mwetu? (Ni mwongozo. Tunahitajika kuwa makini sana wakati ambapo “mioyo yetu inapotuhukumu.”)

C. Soma 1 Yohana 4:1-3. Je, tunatambuaje roho wa uongo akiongea nasi? (Roho wa uongo haikiri kuwa Yesu ni Mungu aliyefanywa kuwa mwanadamu.)

1. Je, hiyo inajihusishaje na hatia? (Kumbuka injili inasema kuwa Yesu alikuja kutuweka huru dhidi ya dhambi na mashitaka! Kama dhambi yako imesamehewa, ni roho wa uongo anayekushitaki.)

D. Soma 1 Timotheo 4:1-2. Je, ni aina gani za dhamiri walizo nazo hawa watu? (Dhamiri zilizolemaa/zenye hitilafu. Dhamiri zilizofanywa na pepo na waongo.)


1. Nini kinakujia akilini unapofikiria dhamiri “sugu kama chuma cha moto?” (Hii ni dhamiri inayotisha, dhamiri iliyojeruhiwa.)

E. Soma 1 Timotheo 4:3-5. Ni kwa njia ipi dhamiri hizi zina hitilafu/zimelemaa? Je, zi vipofu katika dhambi? (Hapana. Hawa watu wanaita dhambi vitu visivyo dhambi. Dhamiri hizi zinaongozwa na mapepo ili kuamini kuwa mambo mazuri ni mabaya.)

F. Soma Zaburi 103:8-9. Je, unadhani ni kwa muda gani Mungu wetu mwenye upendo anatushitaki? Je, ni kwa muda gani Mungu wetu anatupatia hatia? (Hadi pale tunapokiri dhambi zetu na kuikubali kafara yake kwa ajili ya dhambi zetu.)

1. Je, ni nani anayetushitaki baada ya hapo? (Mapepo!)

G. Soma Zaburi 103:10-12 na Mika 7:19. Je, ni mahali gani ambapo Mungu anaweka dhambi zetu za kale? (Mbali sana kwa kadri inavyowezekana!)

1. Soma Waebrania 8:12 na Waebrania 10:17. Je, tunawezaje kuwa na uhakika kuwa ni kazi ya roho mwovu kutufanya tujisikie hatia kuhusiana na dhambi tulizozikiri? (Mungu hakumbuki dhambi zetu! Hawezi kuwa Mungu anayetutaabisha.)

a. Je, unamtukuza Mungu wako mwenye rehema sasa hivi?

IV. Kukiri Kuliko Sahihi

A. Soma Zaburi 32:1-4. Tuna taswira ya picha mbili katika nyakati. Je, ni wakati gani ambapo Mfalme Daudi anajisikia kubarikiwa? (Ni pale ambapo dhambi yake imesamehewa na kusitiriwa.)

1. Je, inamaanisha nini dhambi zako “kusitiriwa?”

2. Je, ni wakati gani ambapo Mfalme Daudi anajisikia vibaya sana kuhusiana na dhambi yake? (Soma Mithali 28:13. Kukaa kimya kuhusiana na dhambi zetu, yaani, bila kuzikiri/kuzitubu kunasababisha matatizo.)

B. Soma Zaburi 32:5. Je, ni kwa namna gani Daudi anatoka katika mahali anapojisikia vibaya sana hadi mahali ambapo anajisikia kubarikiwa? (Anatubu dhambi yake kwa Mungu na Mungu alimsamehe.)

C. Soma Zaburi 32:6. Je, Daudi anamaanisha nini anapoandika “wakati unapopatikana?” Je, Mungu hapatikani mara zote? (Daudi anapendekeza kuwa tunahitajika kutenda kwa usahihi linapokuja suala la kutubu dhambi.)

D. Hatua yetu ya kwanza kuelekea kwenye maisha huru yasiyokuwa na hatia ni kukiri/kutubu dhambi zetu. Soma Zaburi 51:4. Biblia yangu inanukuu sehemu ya pembeni kuwa Mfalme Daudi aliandika hivi baada ya kuwa amefanya uzinzi na Bathsheba. Je, Daudi anawezaje kuandika kuwa alimtenda dhambi Mungu “peke yake”?

1. Daudi pia alimuua Uria. Alimtunia jemadari wake kwenye njama ya mauaji. Bila shaka kabisa, alizungushia yote haya kwa mlima wa uongo. Je, ni kwa jinsi gani “Mungu peke yeke” ndilo neno sahihi? (Dhambi ni dhidi ya Mungu. Dhambi inasamehewa kwa kukiri/kutubu kwa Mungu – na si kwa wanadamu.)

2. Kwa nini watu wengi wanapendekeza kuwa tunahitajika kutubu dhambi zetu kwa watu wengine? (Soma Hesabu 5:5-7. Hakuna mwanadamu anayeweza kutusamehe dhambi. Tunatubu dhambi zetu kwa Mungu peke yake. Hata hivyo, Mungu anatutaka “kuweka mambo sawa” na mtu tuliyemuumiza/tuliyemkosea.)

a. Je, umewahi kutenda dhambi na kudhani kuwa mtu uliyemkosea amekuadhibu kikatili? (Ikubali kwa kuwa Mungu anaafiki/anaidhinisha asilimia 20 ya adhabu kama fidia!)

E. Soma Yakobo 5:13-16. Fikiria kwamba ulimsengenya mtu fulani na kamwe hakugunda hilo. Je, unapaswa kumwendea mtu huyo na kusema “Samahani kwa kusema mambo mabaya juu yako?” (Hapana. Tunakiri kwa watu wengine ili tu “kutuliza” dhambi. Kama mtu huyo kamwe hajawahi kujua kile ulichofikiria juu yake, kukiri kutasababisha maumivu ambayo amri ilikusudia kuepusha. Haitatuliza kitu chochote. Badala yake, inakupasa kumwendea mtu aliyekusikia ukisema hili, na kulisahihisha.)

1. Je, ni kwa nini basi, Yakobo anatuambia kuungamiana sisi kwa sisi? (Kwa hakika sio kwa ajili ya kusamehewa. Yakobo anaelezea jinsi ambavyo jumuiya ya kanisa inatusaidia kukabiliana na matatizo. Kama tuna “mshirika muwazi” (sio mtu asiyejua kuhusu dhambi yako dhidi yake) anayekubali dhambi zetu atatusaidia kuziepuka.)

F. Rafiki, dhamiri iliyofanywa vema ni thawabu ya Mungu ya kutusaidia kuepuka dhambi. Kama umetenda dhambi, msifu Mungu kwamba huhitajiki tena kujisikia hatia dhidi ya dhambi iliyosamehewa! Kama una dhambi ambayo hujaitubu kwa nini usiitubu sasa hivi na kuuacha mzigo wa hatia nyuma yako?

V. Juma Lijalo: Fikara Njema

0 comments:

Post a Comment