Sunday, January 30, 2011

Somo la 6: Fikra Njema

(Mathayo 5, Luka 6, Wakolosai 3, Warumi 8)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Umewahi kuwasikia Wakristo wakijadiliana kuhusu “imani” dhidi ya “matendo?” kwa hakika umewahi. Kama unadhani hii haielezei suala hili kwa usahihi, hebu chukulia muktadha mwingine: “haki kwa mtazamo.” Kwa miaka mingi sasa, nimefikia muafaka wa kuamini kuwa imani na matendo sio vitu mbadala. Badala yake, vinaendana. Nimefikia muafaka na kuamini kuwa vyote viwili vinatokana na mtazamo wetu. Somo letu juma hili linahusiana na “Fikara Njema,” ambalo linaonekana kuwa kama aina nyingine inayosimama kwa ajili ya “mtazamo.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kuona kile tunachoweza kukibaini kwenye hii mada!

I. Mauaji

A. Soma Mathayo 5:17-19. Je, mtazamo wa Yesu dhidi ya Amri Kumi ni upi?

1. Je, ni rabsha gani anayoitabiri Yesu kuhusu wafuasi wake na Amri Kumi? Yesu anatabiri wafuasi wake hawatakubaliana juu ya umuhimu ya kuzishika Amri Kumi.) anatuambia kuwa mbinguni, wale waliofundisha hapa kuwa kuzishika amri hakukuwa kwa muhimu, hawatapaa kwenye daraja la kwanza kwenye ndege inayoitwa “Air Heaven.” Huenda watasafiri wakiwa kwenye chumba cha kubebea mizigo.)

a. Je, itakuwa busara kwetu sisi kufikiria sasa hivi kwamba tufikirie sio tu kuingia mbinguni, bali hadhi yetu pale? Tena ikizingatiwa kuwa, ni kitu cha milele! (Kama unasema “ndiyo,” basi kuwa na uhusiano wetu mwema na amri ni muhimu.)

B. Soma Mathayo 5:21. Je, ulisikia kauli hii wapi? (Soma Kutoka 20:13: “Usiue.”)

C. Soma Mathayo 5:22. Je, hii inapatikana mahala popote kwenye Amri Kumi? Kwa kuwa Yesu ni Mungu, siwezi kukanusha haki yake ya kuanzisha fungu la sheria mpya. Lakini, Yesu alianza kwa kusema kuwa tunapaswa kuwafundisha watu kuzishika amri zilizopo. Hakutuambia kuanzisha fungu la amri mpya. Je, unaelezeaje maneno ya Yesu kuhusu hasira na kuapiza?

D. Soma Luka 6:43-45. Je, kuna uhusiano gani kati ya mti na na tunda? (Asili ya mti inaashiria asili ya tunda.)

1. Hebu tutumie hili kwenye kauli za Yesu kuhusu mauaji. Je, mauaji ni mti au tunda?

a. Je, hasira ni mti au tunda?

b. Je, kuapiza ni mtii au tunda?

c. Je, moyo ni mti au tunda? (Yesu haanzishi amri mpya. Anataja tu matendo maovu yanayotoka kwenye moyo mwovu (mtazamo mwovu). Uapizaji na hasira vinatoka kwenye moyo mwovu. Hayo tu ni mafunuo ya awali ya mtazamo unaoweza kuishia kwenye mauaji.)

E. Soma Mwanzo 4:1-5. Kwa nini Kaini alighadhibika? (Mungu alionekana kumpendelea Habili dhidi yake.)

1. Kwa nini Mungu alionyesha upendeleo? (Dhana ni kwamba Habili alimtii Mungu kwa kuleta sadaka ya wanyama.)

a. Je, aina ya sadaka inajalisha? (Je, haitegemeani na muktadha na zawadi/talanta za asili alizopewa mtu? Habili alikuwa mfugaji, Kaini alikuwa mkulima. Mtazamo mpana unahitaji kuwa kila mtu anapaswa kutoa sadaka katika njia ambayo inaendana na talanta zake, sawa? (Kwa hakika sivyo.)

F. Soma Mwanzo 4:6-8. Fuatilia hatua zilizoishia kwenye mauaji. Kutotegemea kanuni za Mungu, hasira, ukataliwaji unaotokana na mashutumu, na hatimaye, mauaji.)

1. Je, unaweza kuona kuwa hasira inahusiana na mauaji?

2. Kama ungekuwa unampa Kaini ushauri kuzuia hili tatizo la umauti, je, ungempa ushauri gani?

3. Angalia tena Mwanzo 4:6-7. Je, ni ushauri gani anaoutoa Mungu ili kuepusha njia inayojielekeza kwenye mauaji? (Mungu anamwambia Kaini kuwa lazima “aushinde” mtazamo wake wa kidhambi. Badala ya kufanya chochote kile ambacho Kaini anafikiria ni bora, anatakiwa kuwa na mtazamo wa kutaka kufanya kilicho sahihi machoni pa Mungu.)

G. Hebu tuchimbue jinsi gani tunaweza kuwa na mtazamo bora.

II. Njia Mbili

A. Soma Mithali 14:22. Je, ni uamuzi gani wa muhimu tunaopaswa kuufanya ili kuamua njia ya maisha yetu? (Tuna maneno mawili muhimu, “njama” na “mpango.” Zinawakilisha uamuzi wa makusudi wa kutenda wema au uovu. Kwa hiyo, vita dhidi ya dhambi maishani mwako vinaanza na mawazo yako – hususan, kama unapanga jambo jema au unapanga njama za uovu kwa watu wengine.)

B. Soma Wafilipi 4:8. Hili ni jaribio binafsi. Unapokuwa na muda wa kuiacha akili yako kuwa huru, je, ni kitu gani unachokifikiria?

1. Je, unafikiria kuhusu kutembea na mke/mume wa mtu fulani? Je, unafikiria jinsi ambavyo usivyo na furaha ukilinganisha na watu wengine? Je, unafikiria jinsi ambavyo una wivu kuhusiana na mafanikio ya watu wengine? Je, unafikiria jinsi ambavyo unaweza kumkandamiza mtu fulani?

2. Je, unapanga jinsi ambavyo unaweza kuubeba mzigo wa mtu fulani? Je, unapanga jinsi ambavyo unaweza kuwa mbaraka kwa mtu fulani?


3. Au, unatumia muda wako ukifikiria jinsi ambavyo unaweza kuboresha raha au hadhi yako maishani? Kwa miaka kadhaa, nimekuwa kila mara nikilala nikifikiria jinsi ambavyo ninaweza kubadilisha basi la biashara kuwa gari la nyumbani ambalo mtu anaweza kuishi ndani yake “nitakapostaafu.” Kisha nitaweza kuliendesha kuizunguka Marekani nikifundisha hili somo na kuhubiri. Kwa hakika ilikuwa raha, na haraka haraka ninapitiwa usingizi nikiwa na mipango yangu. Ingekuwa bora kiasi gani kama ningepitiwa usingizi nikipanga jinsi ambavyo ninaweza kuboresha maisha ya mtu fulani, badala ya kuboresha basi.)

4. Je, athari za usomaji wako, kuangalia televisheni na kusikiliza redio vinaingiaje kwenye mwelekeo tuliopewa kwenye fungu la 8? (Vina athari kubwa sana kwenye vitu tunavyovifikiria.)

C. Soma Wakolosai 3:1-2. Je, umefikiria kuhusu kustaafu? Je, unajali kuwa utapata fedha kiasi gani au utaishi kwa muda gani (ambayo ni maswali yanayohusiana)? (Isipokuwa tu kama u mdogo sana, utakuwa umefikiria haya masuala.)

1. Je, unaufahamu msemo, “Nitalala/pumzika/staafu nitakapokuwa nimefariki?” Tunachukulia hili kama mzaha, kwa sababu hakuna hata mtu mmoja anaeleza kwa undani jinsi inavyokuwa wanapokuwa wamekufa. Je, mwandishi wa Wakolosai anapendekeza nini? (Tunahitajika kutumia muda mwingi kufikiria kuhusu mbingu, sio kustaafu hapa.)

D. Soma Wakolosai 3:5 na Wakolosai 3:12. Je, unayafanyaje haya?


1. Je, umewahi kujaribu kuelekeza mawazo yako kwenye mambo mazuri? Je, umewahi kuangalia televisheni nzuri (isiyovutia mara nyingi) na “kutupilia mbali” televisheni inayofurahisha? Je, hiyo inaonekanaje kwako?

2. Je, umewahi kutumia muda ukifikiria jinsi ambavyo unaweza “kujivika” unyenyekevu? Au, je, mara nyingi unajaribu kujiepusha kutofedheheshwa/kutodhalilishwa?

E. Hebu tufanye tathmini. Tumedhamiria kwamba kuwa na mtazamo sahihi ni ufunguo katika kumpendeza Mungu. Tumedhamiria pia kuwa kujipatia mtazamo sahihi ni suala la uchaguzi wetu. Tunahitajika kuyaelekeza mawazo yetu kwenye “masuala yaliyo juu,” badala ya jinsi ya kutosheleza mambo yetu “yenye asili ya hapa duniani.” Hii itatusaidia kuyaendeleza mambo mema na sio uovu.)

III. Uwezo wa Roho Mtakatifu

A. Isipokuwa kama wewe u mwenye haki zaidi kwa kiasi fulani kuliko mimi (ambavyo ninafikiria ni kweli) vionjo vyako vya televisheni vinajielekeza kwenye ufurahishaji na kamwe hutumii muda ukifikiria jinsi ya kudhalilishwa/kufedheheshwa kinyume na kepuka kufedheheshwa/kudhalilishwa. (Hata hivyo, kama unapinga kwa mimi kulinganisha kuwa mnyenyekevu dhidi ya kudhalilishwa/kufedheheshwa, pingamizi lako linahimilika. Kama wewe upo kama mimi, unajua kuwa kuielekeza akili yako kwenye mambo mema sio kazi rahisi. Hebu tugeukie mbele kwenye jinsi ambavyo tunaweza kutenda hili. Je, tunayawekaje mawazo yetu kwenye mambo yaliyo mema badala ya mambo yaliyo maovu?

B. Soma Warumi 8:5-9. Je, Biblia inatufundisha kuwa ufunguo wa fikara njema ni upi? (Kwanza, tunarejea kwenye hili suala la kufanya uchaguzi kati ya kile ambacho asili yetu ya kibinadamu inakitamani na kile ambacho Roho Mtakatifu anakitamani kwa ajili yetu. Lakini, mara tunapofanya uchaguzi, Biblia inasema (mara tatu!) akili zetu “zinadhibitiwa” na Roho Mtakatifu.)

1. Je, nini ulio mustakabali wetu kama tukishindwa kumwomba Roho Mtakatifu kudhibiti fikra zetu? (Paulo, aliye bingwa wa haki kwa imani pekee, anatuambia kuwa kama hatufanyi uamuzi sahihi kuhusu nani anayedhibiti mawazo yetu, tutateseka mauti ya milele. Hatuwezi kuwa na imani, hatuwezi kumpendeza Mungu, kama mtazamo wetu ni mwovu.)

C. Rafiki, wokovu unakuja kwa neema pekee. Lakini, kuchagua kuikubali neema ni mtazamo. Je, utachagua hivi leo kumwomba Roho Mtakatifu akujie na kudhibiti mawazo yako, ili kwamba mtazamo wako (tamanio lako) uwe ni kumpendeza Mungu?

IV. Juma Lijalo: Tumaini Dhidi ya Mfadhaiko

0 comments:

Post a Comment