(Isaya 64, Warumi 3, Mathayo 22)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Kama maishani mwako mwote umekuwa ukienenda kwa busara kiujumla kwa kuwaheshimu wazazi wako na Mungu, u na kasoro tofauti kwenye eneo moja muhimu: haki kwa imani. Hakuna kitu kama kujikwaa kwenye dhambi ya kutisha ili kujifunza somo muhimu kuwa hatuna kitu chochote binafsi kitakachotuokoa. Tunaweza kuwa bora kuliko wengi wa wale tunaowafahamu, lakini kwa hakika tumepotea, isipokiwa tu kama tutayategemea kikamilifu kabisa maisha, kifo na ufufuo wa Yesu kwa niaba yetu. Katika somo hili tunaanza mfululizo mpya unaojielekeza kwenye masuala ya ishara katika Biblia zinazotufundisha kuhusu hitaji letu la Mwokozi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kuangalia kuwa joho/vazi la Yesu la haki linamaanisha nini!
I. Tusiomstahili Mungu Wetu
A. Soma Isaya 64:1-2. Biblia inasema kuwa Mungu ni kama moto na sisi ni kama vichaka (au vijiti) na maji. Je, moto unavifanyia nini vichaka na maji? (Unabadili maumbo yao. Unaondoa molekuli zao! Unaviharibu.)
1. Je, sisi ni maadui wa Mungu? Au, Isaya anaandika kuhusu kitu kingine?
B. Soma Isaya 64:4-5. Je, Mungu wetu yukoje kinyume na mungu/miungu mingine? (Anatusaidia. Miungu mingine inawataka wanadamu waisaidie. Katika hili, Mungu wetu ni wa kipekee.)
1. Nini kilichosababisha ufa/mpasuko kati yetu na Mungu wetu mwenye msaada? (Mungu alitaka kuwa na ubia na sisi ambapo kwa furaha kabisa “tungetenda vitu kwa usahihi.” Lakini, tumeshindwa katika jukumu hilo. Tumetenda dhambi dhidi ya njia za Mungu na tunaendelea kutenda dhambi.)
C. Soma Isaya 64:6. Je, tu wabaya kiasi gani? (Matendo yetu bora, “matendo yetu ya haki” (si mimi ninayesema hivi, hivi ndivyo Waebrania inavyomaanisha) ni kama pamba au kipande cha nguo kilichotumiwa na mwanamke wakati wa hedhi).
1. Nilipokwenda kwenye mjumuiko wetu wa miaka ishirini tangu tulipomaliza elimu ya juu ya sekondari, fikra zangu zilikuwa wazi kabisa kuhusu mahusiano. Sasa nilijua kuwa kila mtu katika elimu ya juu ya sekondari alikuwa na hisia za kutokujiamini – ilhali nikifikiria kuwa kila mmoja (au tuseme kwa wengine) alijisikia kujiamini. Sote tulikuwa na mtazamo mbaya tulipokuwa katika elimu ya juu ya sekondari – mtazamo uliofanya maisha yawe magumu zaidi! Je, mtazamo wa aina gani tunaopaswa kuwa nao kuhusu haki yetu kuwa “kama matambara yenye kutia kinyaa?” (Ninapambana na dhambi na ninakarahishwa na udhaifu wangu. Ni ahueni kubwa kujua kuwa hii ni kawaida/kanuni, hata miongoni mwa wale wanaotamani kutenda matendo ya haki.)
D. Soma Isaya 64:9. Je, tumaini la Agano la Kale lilikuwa lipi? (Sisi ni watu wa Mungu. Tunatumaini kuwa hatakuwa na hasira kupita kiasi, tunamwangalia kwa ajili ya kutuokoa kutoka dhambini.)
E. Soma Zaburi 14:2-3. Je, Mungu anawaona watu wangapi wenye haki anapoangalia chini kutokea mbinguni? (Hakuna hata mmoja – angalao miongoni mwa wanadamu!)
F. Soma Zaburi 14:7. Je, fungu hili linasema kuwa lipi lililo tumaini la wanadamu wapotovu? (Fungu hili linatupa taarifa kwa undani zaidi kuhusu wokovu: tumaini letu ni kuwa Mungu ataturejeshea wokovu wetu.)
II. Urejeshwaji
A. Soma Warumi 3:9-12. Je, tumesoma hili mahala fulahi hapo kabla? (Ndiyo! Paulo ananukuu lugha kutoka Zaburu 14 – tuliposoma hivi punde.)
B. Soma Warumi 3:19-20. Je, nafasi/uwezekano wetu wa kuwa wenye haki kwa kutii sheria ya Mungu ni upi? (Sifuri!)
1. Je, lengo la sheria ni lipi basi? (Ni kutufanya tu kuwa na ufahamu wa dhambi zetu.)
C. Soma Warumi 3:21. Je, chanzo pekee cha haki yetu ni kipi? (Mungu.)
1. Je, sheria ina chochote cha kujihusisha na haki yetu?
a. Kama ndivyo, jukumu lake ni lipi? (Haki yetu ni “tofauti na sheria.” Hata hivyo, sheria “inathibitisha” ukweli kwamba chanzo chetu pekee cha haki ni Mungu.)
(1) Je, ni kwa jinsi gani hiyo ni kweli? (Kuwa mwaminifu. Je, utii wako wa sheria ukoje/unaendeleaje? Ukweli kwamba unapambana kutii ni ushuhuda wa sheria kuwa haki huja kutoka kwa Mungu pekee.)
2. Je, manabii wanathibitisha vipi kuwa haki hutoka kwa sheria peke? (Chukulia mashujaa wako wa Agano la Kale. Je, ni wangapi kati yao walitenda dhambi ambazo unadhani kuwa ulikuwa mwerevu vya kutosha kuziepuka?)
D. Soma Warumi 3:22-26. Je, tunapataje hii haki kutoka kwa Mungu? Je, tunashiriki vipi katika wokovu wa Mungu wa wanadamu waovu? (Kwa imani katika Yesu.)
1. Je, Yesu aliifanyaje hii haki ipatikane kwetu? (“Mungu alimwasilisha kama kafara ya upatanisho.” Hii inaleta akilini huduma ya hekaluni la Agano la Kale ambapo damu (kifo) cha mnyama kiliwasilishwa kwa ajili ya dhambi za mwanadamu. Nadharia ilikuwa kwamba mwanadamu hakupaswa kufa kwa sababu mnyama alikufa badala ya mwanadamu.)
a. Chini ya mfumo wa Agano la Kale, je, mwanadamu alipata msamaha wa dhambi? (Hili ni suala la msingi: hakuna hata wakati mmoja katika Biblia ambapo dhambi iliondolewa kwa matendo ya haki. Hakuna Kamwe. Dhana ya msingi ya mfumo haijabadilika. Sasa tuna hekalu la mbinguni na Yesu kama kafara yetu. Angalia Waebrania 9:11-14.)
2. Baini kuwa Warumi 3:22 inasema “hakuna tofauti.” Je, ni aina gani ya tofauti inazoziongelea? (Tofauti katika haki yetu. Kiwango cha utii wetu unaotarajiwa hauleti tofauti yoyote. Sote tunapotea bila neema ya Mungu. Sote tunapotea kama hatukubali mbadala wa haki wa maisha, kifo na ufufuo wa Yesu.)
III. Joho
A. Soma Mathayo 22:1-7. Je, nini kinapaswa kututokea kulingana na dhambi zetu? (Kama tukimkataa Mungu, adhabu ni kali.)
1. Hili ni fumbo/mithali. Unadhani nini kinachomaanishwa kwa “sherehe ya harusi ya mwanawe?” (Maelezo ya Adam Clarke yanajibu, “upekee wa Injili, kipindi ambacho wanadamu wanakaribishwa kushiriki mibaraka inayonunuliwa na ….. kupata mwili na kifo cha Bwana wetu mbarikiwa.”
B. Soma Mathayo 22:8-10. Baini kuwa watumishi wa awali hawaku “stahili kuja.” Je, hili kundi jipya “lilistahili kuja?”
1. Kama huu ndio “upekee wa Injili,” je, hii inatufundisha nini kuhusu yule anayestahili kuujia wokovu? (Wale wasiojali na walio na uhasama hawastahili kuja. Wale wanaokubali wito/ukaribisho, hata kama ni “wabaya,” wanastahili kuja!)
C. Soma Mathayo 22:11-12. Hawa watu walikuja moja kwa moja kutoka mitaani. Je, ni kwa jinsi gani wangeweza kuwa na mavazi ya harusi? (Maelezo ya Adam Clarke yanaeleza kuwa mtu aliyewakaribisha wageni aliandaa vazi kwa ajili yao. “Kuwa na uwezo wa kununua mazazi ya dharura ya wageni maalum kwa ajili ya sherehe ya harusi, ilikuwa ni desturi miongoni mwa Wayunani wa kale.”)
1. Je, kwa nini mtu asiyekuwa na vazi la harusi alitekewa? (Hivyo ndivyo jinsi tulivyo pale tusipokuwa na visingizio vya msingi. Huu ni uthibitisho zaidi kuwa mfalme alitoa mavazi. Vinginevyo, jibu la kwanza la yule mtu lingekuwa “nilikuwa ninafanya manunuzi katika duka la Shoprite na nikaambiwa kuwa lazima nije mara moja!”)
D. Soma Mathayo 22:13-14. Je, ni kwa jinsi gani mfalme anaweza kusema “wateule ni wachache?” Ni nani aliyefanya uchaguzi? (Mfalme alichagua kumtupa yule mtu kutoka kwenye sherehe ye harusi.)
1. Je, nini kilikuwa na ambacho hakikuwa msingi wa uchaguzi wa mfalme? (Hakuchagua kulingana na nani aliyekuwa rafiki yake wale walioalikwa wa kwanza. Hakuchagua kulingana na kama mgeni alikuwa mzuri au mbaya. Uchaguzi wake ulitegemeana na wale tu waliovaa vazi la harusi.)
a. Je, hii inamaanisha kuwa watu wabaya wanaokolewa?
b. Je, ishara ya vazi la harusi inasema nini kuhusu tabia ya wale wanaookolewa? (Chochote kile ambacho hawa wageni walikivaa kwenye harusi (ambayo kwa hakika haikuwa mavazi ya harusi kwa sababu yote yalinunulia kwenye duka la Shoprite), nguo zao wenyewe zilifunikwa na joho la harusi. Tabia yetu iliyo na dosari inafunikwa na joho kamilifu la haki ya Yesu!)
E. Tulianza na Isaya. Hebu turejee tena na tusome Isaya 61:10. Je, haki kwa imani (kwa vazi) ni dhana ya Agano Jipya tu? (Hapana.)
1. Je, ni nini kwa hakika, kilicho asili ya vazi tulilopewa na Mungu? (Uvikwaji wa wokovu na haki!)
F. Rafiki, je, utavaa vazi la haki ambalo Yesu Mfalme wetu anatupatia? Au, je, utatekewa kwa sababu unadhani kuwa mavazi yako mwenyewe ni mazuri vya kutosha?
IV. Juma Lijalo: Toka Kutukuzwa Hadi Kutupwa Chini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment