Tuesday, April 5, 2011

Somo la 2: Kutoka Kukwezwa Hadi Kutupwa Chini

(Mwanzo 3, Ufunuo 12, Ezekieli 28)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kama haki ni kama vazi, je, uovu unavaa nini? Juma hili tunaangalia kile ambacho Biblia inasema kuhusu chanzo cha Shetani na uovu. Somo letu limefanywa kuwa gumu kwa ukweli kwamba baadhi ya maandiko yanaonekana kuwa ya kiishara. Je, kipi ni kitu cha uhakika/ukweli na kipi ni cha kiishara? Je, tunazifikiaje kweli? Hebu tuzame kwenye hili tukio lisilokuwa la kawaida kwenye somo letu la Biblia.

I. Mshawishi

A. Soma Mwanzo 3:1-4. Tuna kitu cha kushangaza hapa: mnyama ambaye si kwamba tu anaongea, bali pia anamchanganya Mungu! Je, hii ni ishara, mnyama au kitu kingine tu?

B. Soma Ufunuo 12:7-9. Je, tunajifunza nini kuhusu joka ambalo “linauongoza ulimwengu wote upotevuni?” (Joka ni Shetani, Mwovu. Kwa hakika ana uwezo wa kuchukua mfano wa nyoka au zimwi/mnyama! Alikuwa mbinguni na alipigana dhidi ya Mungu na alishindwa. Alitupwa chini duniani ambapo tangia hapo amekuwa akijihusisha na kazi yake ya kuwadanganya wanadamu.)

1. Je, Shetani yu peke yake? (Hapana. Ana malaika waliopambana (kwa mafanikio) kwa ajili yake. Nao pia walitupwa chini duniani pamoja naye.)

II. Vazi la Mshawishi

A. Bado tuna maswali ambayo hayajibiwa kuhusu Shetani. Hebu tusome Ezekieli 28:11-13. Je, ni nani anayeelezewa hapa? (Mfalme wa Tiro.)

1. Je, ni ukweli upi usioendana na mfalme wa nchi? (Inasema kuwa alikuwa kwenye Bustani ya Edeni.)

a. Hebu tutafakari akilini mwetu wahusika waliotupwa katika Bustani ya Edeni. Je, ni wafalme wowote (tofauti na Mungu)? (Hapana.)

b. Kama nyoka wa Edeni hakuwa nyoka wa ukweli, je, Mfalme wa Tiro anaweza kuwa kitu kingine tu tofauti na mfalme wa kibinadamu? (Hakuna nukuu nilizokwishawahi kuziona zinakubaliana nami, lakini kama kweli tulizoziona (na tutaziona) zote zinachukuliwa kuwa za kweli, basi nyoka wa Edeni na Mfalme wa Tiro wana tabia moja – wote walikuwa Edeni. Hitimisho la kimantiki ni kuwa Shetani alichukuwa mfano wa nyoka na mfalme. Shetani alimmiliki nyoka na mfalme, au kwa namna fulani hivi alichukua sura zao. Huenda hii ni mifano ya awali kabisa ya wizi wa sura!)

B. Soma Ezekieli 28:14. Je, hii yaweza kuwa Mfalme wa Tiro? (Sasa tuna mahali pa tatu, “mlima mtakatifu wa Mungu” na maelezo ya tatu “kerubi” ambayo yumkini hayawezi kumwelezea mfalme wa kidunia. Hata hivyo, yanaendana kabisa na kile tulichojifunza kumhusu Shetani hadi hivi sasa. Ushahidi ni wa kutosha kabisa kuwa Shetani anaelezewa hapa, na wala si mwanadamu wa kawaida.)

C. Basi sasa tunajua kuwa Ezekieli anamwelezea Shetani, hebu turejee nyuma na tusome tena Ezekieli 28:13. Je, Shetani amevaa nini? (Vazi lililofunikwa na dhahabu na mapambo yanayotokana na almasi. Mengi ya mawe haya yalikuwa kwenye kifuko cha kifuani cha kuhani mkuu (Kutoka 28:15-21) na mengi yapo kwenye misingi ya Yerusalemu Mpya (Ufunuo 21:19-20).)

1. Je, vazi hili linapendekeza nini kumhusu Shetani wakati alipokuwa mbinguni? (Ya kwamba alikuwa amekwezwa.)

2. Je, Shetani alipatikanaje? (Alikuwa mtu aliyeumbwa – kama wanadamu na malaika.)

3. Tulianza kwa kuuliza “kama haki ni kama vazi, je, uovu unavaa nini?” Je, jibu ni “dhahabu na mapambo yanayotokana na almasi?”

a. Kama hiyo ni kweli, je, tunaelezeaje kifuko cha kifuani cha kuhani mkuu na mawe katika Yerusalemu Mpya? (Tunahitaji jibu zuri zaidi.)

D. Angalia tena Ezekieli 28:14. Je, kazi ya Shetani mbinguni ilikuwa ipi? (Alikuwa amepakwa mafuta na Mungu mwenyewe kama “kerubi mkuu” katika mlima mtakatifu wa Mungu.)

E. Soma Ezekieli 28:15. Je, dhambi iliingiaje mbinguni? (Hili fungu linasema kuwa Shetani aliumbwa akiwa mkamilifu bila kuwa na mawaa. Ezekieli 28:12 inasema alikuwa “mfano wa ukamilifu, amejaa busara na mkamilifu wa uzuri.” Siku moja “uovu ulionekana” ndani ya Shetani.)

1. Je, hili ni jibu la kuridhisha?

F. Soma Ezekieli 28:16-17. Hii inatupatia maelezo ya kina ya jinsi dhambi ilivyoibuka mbinguni. Je, ni matatizo gani katika maisha ya Shetani yaliyoiingiza mbingu na dunia kwenye pambano linaloendelea dhidi ya dhambi? (Majivuno ni tatizo la kwanza. Tatizo la pili linaonekana kuwa ni matendo yasiyokuwa ya haki au kiburi/majisifu/ufidhuli vinavyoibuka kutokana na umiliki mkubwa wa mali.)

1. Fikiria vitu ambavyo kanisa lako mahalia linavichukulia kuwa vinatosha kukufuta ushirika. Je, kiburi kipo kwenye hiyo orodha?
a. Vipi kuhusu matendo yasiyokuwa ya haki au majisifu/ufidhuli kulingana na mafanikio yako maishani?

b. Au, je, sifa hizi yumkini zaidi zinakufanya uchaguliwe kwenye uongozi kanisani?

2. Nini kilichofanya Shetani atupwe kutoka mbinguni? (Majivuno/kiburi.)

a. Kwa hiyo sasa, uovu unavaa nini? (Baini kuwa Ezekieli 28:17 unafungamanisha kiburi cha Shetani na uzuri wake. Hii inapendekeza kuwa vazi la Shetani la dhahabu na mapambo ya almasi lilikuwa sehemu ya tatizo lake la kiburi. Jibu letu linapaswa kuwa, “uovu unavaa kiburi/majivuno.”)

3. Hebu tuangalie sehemu nyingine ya Ezekieli 28:17: “umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako.” Kwa kawaida huwa tunachukulia uzuri na hekima kama mibaraka mikubwa. Je, tunakosea?

a. Nani aliyemfanya Shetani kuwa mrembo/mzuri? (Mungu! Uzuri na hekima ni mbaraka. Lakini, zinaweza kutumiwa vibaya kirahisi. Vyote vinazaa kiburi/majivuno. Kiburi ni uovu ambao tunahitaji uwezo wa Mungu.)

III. Kuepuka Vazi la Mshawishi

A. Soma Kumbukumbu la Torati 8:2-5. Je, lengo la Mungu kwetu ni lipi? (Unyenyekevu?)

1. Ninatambua kuwa uovu unavaa kiburi/majivuno, lakini ninachukia kufedheheshwa/kudhalilishwa/kuvunjiwa heshima/kuaibishwa. Je, hicho ndicho alichonacho Mungu mawazoni mwake kwa ajili yetu?

a. Kama sivyo, je, Mungu anapendekeza kuwa anataka kutufanyia nini katika kipaumbele cha “unyenyekevu?”

2. Hivi sasa ninasoma kitabu kinachoitwa “Cheche: Mapinduzi Mapya ya Sayansi ya Mazoezi na Ubongo kilichoandikwa na Eric Hagerman” (Spark: The Revolutionary New Science of Exercise and the Brain, by Eric Hagerman). Kitabu hiki kinajaribu kubaini uhusiano wa karibu uliopo baina ya mazoezi na afya ya ubongo. Kwa urahisi kabisa, mazoezi yanaunyoosha/yanauchangamsha mwili ambao unaisaidia akili kuweza kuhimili msongo. Je, hii ndio kanuni tunayoiona kwenye Kumbukumbu la Torati 8? (Ndiyo. Jangwa lilikuwa sehemu yenye msongo mkubwa kuishi. Watu walipokuwa na njaa, walipatwa na msongo. Lakini, Mungu aliwaokoa kutoka kwenye msongo wao. Hii iliwasaidia kukua katika imani kwa kuwaonyesha kuwa njia ya kuachana na msongo ilikuwa ni kumwamini Mungu.)

3. Je, mafungu haya ya Kumbukumbu la Torati 8 yako kinyume kwa namna gani na kuvaa vazi la kiburi? (Majivuno/kiburi kinakufanya ufikiri kuwa unaweza kutenda wewe mwenyewe. Wewe ni bora zaidi/una hadhi ya juu. Kumwamini Mungu na kumwona akitenda kazi kwenye yale mambo yanayokupa msongo kunaongeza imani yako kwake.)

B. Je, nidhamu ya Mungu ni ya muhimu kiasi gani maishani mwako? (Kama unataka kukua (misuli, afya ya kihisia, imani, nk.) unatakiwa kunyooshwa. Unajua kuwa hii ni kweli kutokana na mazoezi. Kama tumeichukulia nidhamu kama mazoezi, tungeifurahia yote kupita kiasi.)

1. Kama ndivyo, je, kuinyoosha imani yeti ni tofauti kiasi gani? (Unyooshaji wa imani (kama tulivyojifunza juma lililopita) unaonyesha kuwa hatuwezi kufanya hivyo. Hata hivyo, ukuaji wa imani unakuja kwa kutambua kuwa Mungu anaweza. Anatupatia mana na mavazi hayachakai. Hii inafanya vazi letu la haki likue na vazi letu la kiburi linywee.)

IV. Shabaha ya Mshawishi

A. Soma Ufunuo 12:17. Je, mtazamo wa Shetani kwetu ni upi? (Amekasirika. Anaendeleza vita dhidi yetu.)

1. Je, Shetani anatumia silaha gani dhidi yetu? (Kiburi!)

2. Je, fungu la 17 linapendekeza ulinzi gani? (Juma lililopita tulijifunza kuwa sheria inathibitisha/inashuhudia haki kwa imani. Sio tu kuwa utii wa sheria ni ngao dhidi ya uovu, lakini sheria inatukumbusha kuhusu dhambi zetu na kutoboa kiburi chetu. Ushuhuda wa Yesu ni kwamba aliishi na kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Kuishikilia kikamilifu imani yetu katika Yesu ni ulinzi wetu bora zaidi dhidi ya ushari wa hasira na ujivuni wa Shetani.)

B. Rafiki, je, ni kwa dhati kiasi gani unachukulia tatizo la kiburi maishani mwako? Je, utadhamiria hivi leo kuvua vazi lako la kiburi na kulibadilisha na vazi la Mungu la haki? Kama inachukua nidhamu kidogo kukusaidia uweze kuona utofauti, basi msifu Mungu!

V. Juma Lijalo: Vazi Lisilokuwa na Hatia.

0 comments:

Post a Comment