Monday, April 18, 2011

Somo la 4: Joho la Rangi Mbalimbali

(Mwanzo 29, 30, 37 & 41)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, unapambana na hisia za kutokujiamini? Je, mara nyingine wivu huwa unakufanya ufanye vitu ambavyo vinginevyo usingevifanya? Je, ni sehemu gani ya maisha yako unayoipoteza kwa kujaribu kuwathibitishia watu wengine kwamba wewe nae una hadhi? Je, wivu umeongezea mchakato katika maisha yako na yale ya familia yako? Juma hili tunageukia kwenye familia iliyojaa wivu na hisia za uduni. Matokeo yake yalikuwa ni mambo ya kutisha. Hebu tuchimbue kwenye kisa chetu cha Biblia na kuona kile tunachoweza kujifunza!

I. Yusufu na Akina Mama

A. Soma Mwanzo 37:1-2. Baini kuwa Yusufu anafanya kazi na nduguze, lakini mama zao ni tofauti. Je, tunaelewa nini kuhusu mama mbalimbali/mama tofauti?

1. Soma Mwanzo 29:16-18 na Mwanzo 29:21-29. Je, unadhani ni uhusiano wa aina gani uliokuwepo kati ya Lea na Raheli?

a. Je, ni nani mwenye kosa kwenye hii hali?

2. Soma Mwanzo 30:1-5. Unafikiria nini kuhusu mchakato wa Bilha kuwa mke wa Yakobo?

a. Nini kilichohamasisha huu uamuzi? (Wivu.)

3. Soma Mwanzo 30:9-11. Unafikiria nini kuhusu mchakato wa Zilpa kuwa mke wa Yakobo?

a. Je, nini kilichohamasisha huu uamuzi? (Tamaa ya makuu/malengo.)

B. Hebu turejee kwenye Mwanzo 37:1-2. Baini kuwa fungu la pili linasema “hivi ndivyo vizazi vya Yakobo” na kisha papo hapo linazungumzia kuhusu Yakobo na nduguze. Je, hiyo inaleta mantiki yoyote? (Maisha ya Yakobo yanaelezewa kuwa hayaendi vizuri katika familia yake.)

1. Je, ni udhibiti gani alionao Yakobo dhidi ya hii hali?

C. Soma Mwanzo 30:22-24. Je, Raheli ana furaha kwa kumpata Yusufu? (Anataka wana wengine.)

D. Hebu tukufanye uwe mshauri wa familia (labda bingwa wa magonjwa ya akili wa familia). Je, ungetoa ushauri gani?

1. Je, ungesema kuwa wake wangepaswa kutafuta thamani yao kwa Mungu, sio kwa mume wao au idadi ya watoto wao?

E. Soma Mwanzo 30:17-18. Sasa unasemaje kuhusu ushauri wako?

1. Je, Mungu alimzawadia Lea kwa kumtoa mjakazi wake kwa mumewe? (Bila shaka Mungu alisikia maombi ya Lea. Lakini, nina uhakika Mungu hakumzawadia Lea kwa kuwa na wivu na kumtoa mwanamke mwingine kwa mumewe!)

a. Je, hii inatufundisha nini? (Kuwa makini kwa kile tunachomtolea Mungu.)

II. Yusufu na Nduguze

A. Tumejifunza kuwa hali ya familia ni mbaya. Hebu tuangalie Mwanzo 37:1-2 tena. Yusufu analeta habari mbaya kwa kaka zake wakubwa wa kambo. Kama ungeujua huu ukweli tu, je, ungekisia nini kuhusu uhusiano kati ya hawa ndugu?


1. Hebu tuonezee kweli nyingine. Soma Mwanzo 35:22 na ufikirie kile tulichojifunza kuhusu jinsi ambavyo Bilha na Zilpa walikuwa wake za Yakobo. Unadhani ni mtazamo wa aina gani waliokuwa nao wana wa Zilpa (na hususan Bilha) kuhusu hadhi yao? Walikuwa wana wa wake za Yakobo wa hali ya chini. Reubeni, mwana wa Lea, hata alilala na Bilha! Nina uhakika kuwa katika hali hii iliyojawa na wivu, walijisikia duni kwa Yusufu.)


2. Unadhani Yusufu alijisikiaje mbele ya kaka zake wakubwa? (Kwa kuwa Yusufu alikuwa na miaka kumi na saba tu, huenda aliwalea. Bila shaka ndio maana walikuwa wenye madaraka.)

3. Je, inawezekana kuwa kila mmoja – Yusufu na wana wa wake wenye hadhi ya chini – wote walikuwa na hisia za uduni?

4. Je, unadhani wana wa wake wenye hadhi ya chini walimfikiriaje Yusufu kwa kupeleka taarifa ya tabia zao mbaya?

B. Soma Mwanzo 37:3. Kwa nini Yakobo (Israeli) anampatia Yusufu hii kanzu? (Kwa sababu alikuwa mzee wakati Yusufu alipozaliwa.)

1. Je, hiyo ni sababu ya aina gani? (Yakobo aweza kuwa alikuwa na mhemuko, lakini ninaamini kwamba upendo wake kwa Raheli ulikuwa ni sehemu ya sababu ya hisia zake dhidi ya Yusufu.)

C. Soma Mwanzo 37:4. Je, Yakobo anaonyesha upendo wake kwa Yusufu kwa dhati?

1. Je, Yakobo alipaswa kutarajia hili?

a. Je, unadhani Yakobo anajali?

2. Je, unadhani Yusufu anajibuje kutokana na hii hali? (Hii itaongeza tu hisia za Yusufu kuwa alikuwa ni “mtu wa nje” na hakustahili kuwa sehemu ya “genge.”)

D. Soma Mwanzo 37:5-7. Unadhani ni kwa nini Yusufu alishiriki nao hii ndoto? Je, hakuwa makini/hakuwa na hekima? Mpumbavu? Mwenye kiburi/kujigamba? (Kwa hakika hakuwa anaonyesha umahiri wa kihisia na upevu/ukomavu, ila ninahisi alielezea kisa kwa sababu alitaka kuwaonyesha ndugu zake wakubwa kuwa alikuwa na hadhi. Walipaswa kumruhusu kuingia kwenye kundi lao.)

E. Soma Mwanzo 37:8. Je, kisa cha Yusufu kilileta athari iliyokusudiwa?

F. Soma Mwanzo 37:9-10. Mara hii, je, Yusufu ana kisingizio chochote cha kuelezea hii ndoto?

G. Soma Mwanzo 37:11. Je, hizi ndizo hisia ambazo ungezitarajia? (Unaweza kutarajia nduguze kufikia uamuzi kuwa Yusufu alikuwa fidhuli mwenye kiburi/majigambo. Wivu, sio jambo ambalo lingekuja akilini. Ukweli kwamba wana wivu inaimarisha wazo kuwa walijihisi duni, na sasa wanafikiri kwamba labda Mungu amemchagua Yusufu kuwa juu yao.)

1. Je, Yakobo anaamini kuwa hii ndoto imetoka kwa Mungu? (Yakobo anadhani kuwa ina umuhimu.)

H. Je, unadhani kuwa hizi ndoto zilitoka kwa Mungu? Kwa nini Mungu ampatie Yusufu hizi ndoto hali akijua kuwa atakuwa akiwaambia?

III. Yusufu na Misukosuko

A. Soma Mwanzo 37:12-14. Je, ni kiwango gani cha mamlaka anachopewa Yusufu?

1. Ni kwa kiwango gani Yakobo anawajibika kwa kile kitakachotokea?


B. Soma Mwanzo 37:18-20. Je, nini kilichohamasisha moja kwa moja mpango wa mauaji? (Ndoto za Yusufu.)

1. Hebu tukufanye wewe kuwa mshauri wa familia tena. Je, ungetoa ushauri gani kuepusha huu msukosuko?

a. Je, ungemwambia Yakobo, “Usimtume mwanao mdogo ili akuletee taarifa juu ya wanao wakubwa?”

b. Je, ungemwambia Mungu, “Usimpatie Yusufu hizo ndoto?” (Yakobo ana haki ya kumteua yeyote anayemtaka kuwa msimamizi. Nina uhakika palikuwepo na sababu za kumchagua Yusufu. Mungu ana haki ya kuwafunulia watumishi wake mambo yajayo. Tatizo lipo kwa ndugu zake (na kwetu sisi). Tunahitajika kushikamana na ukweli kwamba sisi si wenye akili nyingi, wenye vipaji, waaminifu, au wenye uwezo kama wengine. Labda ni muda tu (mwana wa Yakobo wa uzeeni) unampatia mtu mmoja manufaa dhidi ya mtu mwingine. Tunahitajika kukubali hili kwa neema na bila wivu.)

C. Soma Mwanzo 37:21-28 na lenga zaidi fungu la 26. Nini kinachohamasisha uamuzi wa mwisho wa nduguze Yusufu?

IV. Yusufu na Matokeo

A. Kisa chetu kinaendelea na mgeuzo wa ajabu ambapo Yusufu anajitokeza mbele za Farao Mfalme wa Misri, anafunua njaa ijayo, na anafunua jinsi ya kuepuka matokeo yake. Farao anamfanya Yusufu kuwa wa pili kimamlaka na msimamizi wa mpango wa kutuliza njaa. Soma Mwanzo 41:56-42:2.

1. Kama nduguze Yusufu wangetekeleza mpango wao wa awali na kumwua Yusufu, je, matokeo yake yangekuaje? (Huenda wengi wao wangekufa.)


a. Je, hii inatufundisha nini kuhusu hisia za wivu, uduni na ulipizaji kisasi?

2. Je, nini kilichotokea kwa nduguze Yusufu ikiwa ni matokeo ya maboresho ya mpango wao wa kumdhuru Yufusu? (Mwanzo 42-50 na Kutoka 1 vinaelezea kuwa katika mpango wa muda mfupi waliishi. Dhambi yao ilifunuliwa. Uzao wao uliishi Misri kwa miaka 430 (Kutoka 12:40), baadhi ya sehemu yao wakiwa watumwa.)


B. Rafiki, maamuzi unayoyafanya leo kutokana na hisia za uduni, wivu na ulipizaji kisasi vinaweza kuwa na athari za wazi kabisa maishani mwako, kwenye familia yako na kwenye uzao wako. Je, utaamua hivi leo kumwomba Mungu akuondolee hisia zako za uduni na wivu na kuzibadilisha na hisia za shukrani kwa kile ambacho Mungu amekutendea?

V. Juma Lijalo: Mavazi ya Kikuhani ya Neema.

0 comments:

Post a Comment