Monday, May 9, 2011

Somo la 7: Katika Uvuli wa Mbawa Zake

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(2 Samweli 12, Zaburi 32)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Nilipokuwa nakua, nilijifunza katika shule yangu ya Kikristo kuwa dhambi hufuatiwa na janga/maafa. Hiyo ni kweli mara kwa mara. Unastahili adhabu, unapata adhabu, na unapaswa kuelewa vizuri zaidi kuliko kumwomba Mungu kukuepusha na kile unachostahili, sawa? Huenda hapana. Somo letu juma hili linamwangalia mmojawapo wa mashujaa wakuu wa Mungu katika Biblia, aliyejiingiza katika dhambi kubwa, na kisha akateseka na adhabu. Lakini, kwa sababu fulani fulani hivi, bado alionekana kuwa na shukrani kwa ulinzi wa Mungu. Inaonekana kuwa kama fumbo/mwujiza. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kuona kile tunachoweza kujifunza!

I. Katika Uwajibikaji

A. Soma 2 Samweli 12:1-3. Lilikuwwa wazo la nani la kumwambia Mfalme Daudi kisa hiki? (Mungu alimtuma Nathani.)

1. Je, unaweza kujifananisha na mtu masikini kwenye hicho kisa kwa sababu una mnyama kipenzi?

B. Soma 2 Samweli 12:4-6. Jiweke kwenye nafasi ya Mfalme Daudi. Unadhani ungefikiria kwa nini Nathani alikuwa anakuelezea hiki kisa? (Mfalme alikuwa ni hakimu pia. Bila shaka Daudi alifikiri Nathani alikuwa anawasilisha suala gumu kwake ili alisuluhishe.)

1. Je, unakubaliana na hitimisho la Daudi?

2. Je, sio ukatili mno kumtaka mtu afe kwa ajili tu ya mnyama? (Daudi hamaanishi kifo hapo, anadhani kuwa huo ni ukiukwaji mkubwa mno wa haki za binadamu.)

C. Soma 2 Samweli 12:7-9. Unadhani ni kwa nini Mungu alimtaka Nathani amwingie Mfalme Daudi kwa kutumia njia hii – kwa kutumia kisa? (Alimtaka Daudi atangaze hukumu ya kunyang’anywa ujikwezaji wake.)

1. Je, umewahi kumsikia mtu akisema kitu fulani, sio kukushutumu, lakini kitu chenye athari ya kukutia hatiani kutokana na dhambi yako? (Hii imenitokea. Nilidhani kuwa dhambi haikuwa mbaya kiasi hicho (na huenda hata sio dhambi), hadi pale mtu fulani aliposema jambo fulani lililoiweka kwenye mwanga halisi.)

2. Kama wewe ungekuwa Daudi, je, ungesema kuwa hukumwua mke wa Uria, na kwa hiyo analojia/hali hiyo sio sahihi? (Daudi amekwama, kwa sababu jibu lingekuwa, “Hapana, badala yake ulimwua jirani (Uria).”)

3. Kisa cha Nathani kinasaidia kufunua mzizi wa hizi dhambi za kutisha. Ni nini hiki? (Ubinafsi. Kutaka kitu tusichokuwa nacho – kitu kinachomilikiwa na mtu mwingine.)

D. Soma 2 Samweli 12:10-12. Je, Mungu anaiangaliaje dhambi ya Daudi? (Ya kwamba Daudi “amemdharau” Mungu.)

1. Kwa nini jambo hili ni la Mungu binafsi? Daudi haonekani kumdharau mtu yeyote – alianguka tu kwa mwanamke mzuri na baadaye alikuwa anajaribu kuifanya dhambi yake kuwa siri. (Mungu haziangalii Amri Kumi kama aina fulani ya orodha inayopendekezwa. Mungu anaangalia matendo yetu yakiakisi upendo wake kwetu. Hatumpendi pale tunapowajeruhi vibaya sana majirani zetu.)

2. Kama wewe ungekuwa Daudi, je, ungeziangaliaje siku zijazo?

E. Soma 2 Samweli 12:13. Je, unadhani nini kilisababisha ungamo la Daudi, kisa, kauli kwamba alikuwa amemdharau Mungu, au utabiri kuhusu siku zijazo?

1. Je, kauli ya Daudi ni sahihi kiukweli? Ukizingatia kuwa, Daudi alifanya uzinzi na kusababisha mume kuuawa, je, ni sahihi kusema kuwa “amemfanyia Bwana dhambi” kinyume na zile zilizokuwa za moja kwa moja kwenye msitari wa Daudi?

2. Je, Mungu anasema nini kuhusu dhambi ya Daudi? (Imesamehewa. “Imeondolewa.”)

II. Kusamehewa

A. Soma Zaburi 32:1-2. Daudi anatolea maoni dhambi tuliyoijadili hivi punde. Nilidhani kuwa tatizo la Daudi lilikuwa ni kwamba alikuwa anafunika dhambi yake – na Mungu akakabiliana naye kwa ajili ya hiyo dhambi? Je, inamaanisha nini kuwa “anasitiri” dhambi zetu? (Baada ya dhambi kusamehewa, Mungu anazichukulia kuwa historia.)

1. Baini maneno “ambaye rohoni mwake hamna hila.” Je, ni muhimu kiasi gani kwetu sisi kufikia hii hali? (Tumia hiki kama kipimajoto: kama unataka kuwapotosha watu, hiyo ni ishara kwamba kuna kitu fulani kibaya kwenye mwenendo wako/tabia yako.)

B. Soma Zaburi 32:3-4. Je, hii inaathirije afya zetu? (Daudi anasema kuwa alijisikia vibaya (aliugua) na alijisikia kuathirika kimwili (mifupa kuchakaa, mwili kudhoofu).)

1. Je, inamaanisha nini kwa “mkono” wa Mungu “kunilemea” usiku na mchana? (Dhamiri yake ilimsumbua. Alishindwa kupata usingizi kwa sababu ya hiyo dhamiri.)

2. Hebu tutafakari kidogo. Kama Daudi alihangaishwa sana na hatia kiasi kwamba hakuweza kulala usiku, kwa nini Nathani alijipenyeza kwake na kisa cha kumtia hatiani dhambi yake? (Zaburi hii iliandikwa baadaye sana. Tunapokuwa katikati ya dhambi, tunakuwa na wakati mgumu kuona mambo kwa wazi. Baadaye tunakuwa na maono ya wazi kabisa ya dhambi zetu.)

C. Soma Zaburi 32:5. Je, hatua ya kwanza ya kupata ahueni kutokana na shinikizo la hatia na majuto/toba ni ipi? (Kukiri dhambi zetu kwa Mungu. Lazima tuache kujidanganya kuhusu dhambi zetu.)

1. Baini hii kauli ya kufurahisha “ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.” Nilidhani Mungu alisamehe dhambi. Je, ni kitu gani kingine kinachopendekezwa na hii kauli? (Daudi alibaini “mkono mkuu “ wa Mungu juu yake. Hiyo ilikuwa hatia. Mungu sio tu kuwa anasamehe dhambi, anatutua hatia zetu.)

2. Je, sio kitu cha asili kujisikia hatia kuhusiana na jambo la kutisha tulilofanya – hata baada ya kuwa tumesamehewa? (Soma Ufunuo 12:10. Shetani ndiye anayetushitaki kuhusiana na dhambi iliyosamehewa. Kama tumefanya mambo kwa usahihi, kwa kiwango kinachowezekana, hakuna kitu cha ziada tunachokiweza. Mungu anasamehe dhambi zetu na anatutua hatia zetu.)

III. Matokeo/Madhara

A. Soma tena 2 Samweli 12:10-12. Kuna uzuri gani wa kumwondokeshea Daudi hatia kama anaishia kwenye haya matokeo yote ya kutisha?

1. Je, kweli Mungu amemsamehe Daudi kama anamhuzunisha na haya matokeo?

2. Je, kweli Mungu alitia msukumo wa ubakaji wa wazi wa wake za Daudi? (Soma 2 Samweli 16:22, Mambo ya Walawi 20:11 na Yakobo 1:13-15. Mungu anachukia dhambi. Kwangu mimi naona haiwezekani kwamba Mungu alimhamasisha Absalomu mwana wa Daudi kutenda dhambi. Badala yake, inaleta maana zaidi kusoma hili kama unabii wa Mungu kuhusu matokeo ya siku zijazo ya dhambi ya Daudi.)

3. Tumejadili Zaburi 32:1 inayosema kuwa dhambi zilizosamehewa “zinasitiriwa.” Je, matokeo haya yanaonekana kama “kifuniko” kwako? Baini kuwa Mungu anatumia neno “mwangaza wa mchana” mara mbili – ambayo tu ni kinyume cha “kusitiri” au “siri!” (Dhambi itatuua. Hatia inaifanya miili yetu ichakae. Mungu anaondoa vyote hivyo. Dhambi zetu, hata hivyo, zipo katika mazingira ya mwendo ambayo Mungu ataitumia kama adhabu.)

a. Lengo la hii adhabu ni lipi? (Soma 2 Samweli 12:14. Kipengele kimoja cha dhambi ni utukufu wa Mungu. Kama Mfalme wake aliyependelewa, Mfalme aliyembariki, amejihusisha kwenye hiyo tabia ya kutisha, hiyo inajiakisi vibaya sana kwa Mungu. Mungu ataonyesha maadui zake kuwa kanuni za ulimwengu ni za kweli: utovu wa nidhamu kwa Mungu unaleta matokeo ya kutisha – hata kwa wale ambao Mungu anawapenda.)

B. Soma Zaburi 32:6-7. Hebu subiri kidogo! Hivi punde tu tumejadili jinsi Mungu anavyosamehe dhambi, lakini anaruhusu matokeo ya dhambi zetu yatuadhibu. Je, Daudi anaongelea nini? (Kama Daudi angemfuata Mungu, asingekuwa kweye haya matatizo. Hata hivyo, nadhani Daudi anasema zaidi – kwamba hata katika matokeo/madhara Mungu alimlinda.)

1. Je, kitu kama hicho kinawezekana? Mungu anaruhusu adhabu na kisha anakukinga kwenye mchakato mzima? Katikati ya adhabu unajisikia kuimba kuihusu? (Soma Luka 7:47. Unapotambua ni kwa kiasi gani umesamehewa, unapenda “sana.” Unaingia kwenye mkataba na matokeo halisi kwa sababu unatambua kuwa ni makosa yako na ni ya haki. Wakati huo huo Mungu anakupenda sana alikufa kwa ajili ya dhambi zako za kutisha. Alikusamehe. Kwa shukrani unamsifu Mungu! Hakukuua. Hakukutenga/hakukuweka kando. Anakupenda!)

C. Soma Zaburi 32:8-9. Nina mashaka kama wengi wa wanaosoma fungu hili wamefanya uzinzi na kisha kumwua mwenzi asiye na hatia. Je, wito wa Mfalme Daudi kwetu ni upi? (Kujifunza kutokana na kisa chake. Kujifunza kuhusu upendo wa Mungu na msamaha wake. Kujifunza kuhusu matokeo/madhara. Aidha unaweza kufuata “ushauri” kama huu, au unaweza kuwa kama mtu mshupavu/mkaidi na kuacha dhambi zako zikuvute maishani. Ni uchaguzi wako.)

D. Soma Zaburi 38:10-11. Ahadi ya Mungu kwetu ni ipi? (Upendo wake hautashindwa! Kama tukitubu dhambi zetu, na kuamini neno la Mungu kuhusu namna bora ya kuishi, furaha, shangwe, nyimbo za kusifu zitatunyanyua kutoka kwenye matokeo ya dhahiri ya dhambi zetu.)

E. Rafiki, vipi kuhusu wewe? Dhambi inavutia. Dhambi inaonekana kufurahisha. Lakini, dhambi ina matokeo mawili makubwa. Kwa kutenda dhambi tunaonyesha kuwa tunadharau upendo wa Mungu na kafara yake kwa ajili yetu. Kwa kutenda dhambi, tunajiweka wazi kwenye matokeo/madhara ya kutisha. Je, utadhamiria hivi leo kuepuka somo la ushupavu/ukaidi, na badala yake kujifunza kutokana na kisa cha Daudi?

IV. Juma Lijalo: Mavazi ya Utukufu.

0 comments:

Post a Comment