Monday, May 16, 2011

Somo la 8: Mavazi ya Utukufu

(Isaya 1 & 61, Warumi 3, Luka 10)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Huenda pambano kamwe halitaisha kwa kile ambacho ni sahihi kwenye ibada kanisani. Nina upendeleo wa wazi kabisa na ninawajua watu wengine ambao kwa wazi kabisa hawakubaliani nami. Somo letu juma hili linagusia jambo fulani la ndani zaidi – Jambo gani lililopo kwenye ibada yetu? Je, tunapaswa kuwa macho kwenye uovu ambao unaweza kujificha kwenye ibada yetu na kuubatilisha? Kwa vile tunaishi ili kumpa Mungu wetu sifa na utukufu, hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kufunua kama tuna hatia ya uovu ambao hata unaifanya ibada yetu isikubalike mbele za Mungu!

I. Imani Isiyokubalika?

A. Soma Isaya 1:1 na Isaya 1:10. Je, Isaya anazungumza na viongozi wa Yuda na Sodoma na watu wa Gomora? (Hapana. Je, wazazi wako wamewahi kukwambia “unaenenda kama watoto [watukutu] wa jirani?” Mungu anasema kuwa watu wake wanaenenda kama watu wa ajabu wa Sodoma na Gomora.)

B. Soma Isaya 1:11. Je, Isaya amepotosha ujumbe wa Mungu? Hawa wanyama wa kafara walijielekeza kwenye kafara ya Yesu. Je, Mungu amewahi kusema “sijali kuhusu ukweli kwamba unadai kafara ya Yesu kwa ajli ya dhambi zako?”

C. Soma Isaya 1:12-14. Tunasema nini pale Mungu wetu anapotuambia hataki tuitunze Sabato tena? Hataki twende kanisani? Anachukia anapotuona tunamwabudu?

1. Je, umuhimu wa haki kwa imani kwamba watu waovu (ambapo sote tu waovu) humwendea Mungu wakidai kafara ya Mwanaye na kumwabudu kwa utoaji wake wa ajabu wa wokovu?

a. Kama hivyo ndivyo, je, unaelezeaje huu mkanganyiko katika Isaya? (Sasa unajua kwa nini kwamwe usitie mguu wako kwenye Agano la Kale, sawa? Ninatania tu kwa wale wasiokuwa na uhakika.)

D. Kioja kinaendelea hapa. Kitu kigumu kueleweka kinasemwa. Hebu tuendelee kusoma ili kuona kama tunaweza kubaini hili. Soma Isaya 1:15-16. Je, Isaya anatuambia kuwa kafara zetu (imani), ibada, kusifu na maombi (sala) hayatatufanyia jambo lolote jema isipokuwa tu kama “tutaacha kutemda mambo mabaya?”

1. Soma Warumi 3:19-24. Kama tungeweza kuwaweka Isaya na Paulo kwenye chumba kimoja, je, wangekubali? Je, Paulo angesema, “Rafiki, tuna toleo la kisasa kwa ajili ya mfumo wako?”

2. Angalia tena Isaya 1:16. Je, “kuosha” kunahusika vipi na kutufanya kuwa wasafi kiroho? (Hiki ni kitu kilicho nje kinachodhibiti “matendo yetu maovu.”)

E. Soma Isaya 1:17. Je, Mungu anawaita watu wake “Sodoma” na “Gomora” kwa sababu hawawasaidii watu wanaoonewa, mayatima na wajane?


1. Kwa nini Mungu hataji uongo, wizi, uuaji, uzinzi? Vipi kuhusu ushoga? Mungu, hata hivyo, anawaita kuwa Sodoma na Gomora!

2. Ni kwa jinsi gani Mungu anavyoziita dhambi fulani majina na kuzifananisha na kuwaonea wasiokuwa na uwezo, kunajihusishaje na haki kwa imani?


a. Au, hatupaswi tena kuwa na wasiwasi juu ya masikini na wasiojiweza kwa sababu kwa kuwa sasa tuna mfumo mpya kwa ajili ya injili?

II. Kukitafakari

A. Soma Isaya 1:18. Mungu anasema “hebu tusemezane” hebu tufanye hivyo. Tunaposoma kuhusu dhambi zetu nyekundu kuwa nyeupe kama theluji au sufu, je, hiyo ni ishara ya haki kwa matendo yetu? (Hapana, hii ni ishara ya kuosha – suala la nje ambalo halibadili matatizo yoyote ya ndani.)

B. Soma Luka 10:25. Je, ungependa kujua jibu la swali hili? Hii itatuambia kama mfumo wetu wa wokovu umefanywa kuwa wa kisasa/umetengenezwa upya, sawa?

C. Soma Luka 10:26-28. Je, hili ndilo jibu ulilotaka kulisikia – kwamba mfumo wako wa wokovu umefanywa kuwa wa kisasa?

1. Je, tunahitaji kuwaweka Yesu na Paulo chumbani ili wajadili haki kwa imani?

D. Soma Luka 10:29. Mtaalam wa sheria alimjibu Yesu jibu sahihi. Je, Biblia inamaanisha nini pale inaposema “naye akitaka kujidai haki?” (Sote tunataka kuyafanya matendo yetu kuwa ya haki – ambapo inamaanisha kuwa sote tunatafuta njia ya kutompenda jirani yetu kiukweli kama nafsi zetu!)

E. Soma Luka 10:30-37. Je, jibu hili linakusaidia uweze kujihesabia haki? (Hapana! Hili linatuambia kutumia muda wetu na fedha kuwajali na kuwatunza wahitaji wa kimwili, kifedha, na ulinzi walio wapumbavu wa rangi nyingine – hata wenye viburi na kujisifu!)

1. Je, unaweza kufikiria tafsiri pana ya “jirani yangu?”

F. Hebu tuchukue muda kidogo kupitia tena hapa. Swali lilikuwa: “Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Jibu la Yesu ni kisa cha Msamaria kikifuatiwa na maelekezo ya “Enenda zako nawe ukafanye vivyo hivyo.” Je, tumejielekeza tu kupitia kwenye suala la haki kwa imani?

1. Kama wewe ni mtu wa “haki kwa matendo,” je, tumepitia kwenye suala la tumaini lako kwenda mbinguni kwa sababu (hapa ninabashiri) kazi zako dhaifu hazianzi kujilinganisha na zile za Msamaria?

G. Hebu tumrejeshe Paulo kwenye mjadala wetu. Soma tena Warumi 3:19-20. Je, Msamaria Mwema ni mtu wa kubuni? Lengo lisilofikiwa? (Ndiyo.)

1. Je, unadhani kuwa hii ndio ilikuwa dhana ya Yesu? (Fikiria ambavyo mtaalam wa sheria angefanya kama Yesu angemjibu moja kwa moja: “Nenda mbinguni? Niamini!” Mtaalam wa sheria alisema “kuitii sheria ndio ufunguo wa kwenda mbinguni.” Yesu akajibu, “Ngoja nikuonyeshe kile ambacho inachomaanishwa kuitii sheria.” Tunajua mtaalam wa sheria hakufikia kiwango hiki kwa sababu (kama sisi tulivyo) “alitaka kujihesabia haki” kwa kuangalia tafsiri finyu ya “jirani” yake. Hakupata tafsiri finyu. Hakupata tafsiri finyu. Yesu alimwonyesha njia pekee yenye uhakia ya kwenda mbinguni ilikuwa ni kukubali haki ya Yesu kwa niaba yake.)

H. Sasa hebu terejee kwenye tatizo la marafiki zetu wa Sodoma na Gomora katika Yuda. Je, unaweza kuelezea kwa nini Mungu hakutaka kafara zao au ibada walipokuwa wakiwaonea na kutowasaidia wasiokuwa na uwezo? (Hadhira ya Isaya haikuelewa kuwa walikuwa watu wa Sodoma na Gomora. Haki kwa imani inafanya kazi pale tu tunapoitegemea. Kwa kadri tunavyofikiri kuwa tu wema vya kutosha, tunategemea matendo yetu ili kuokolewa. Matendo yetu kamwe si mema vya kutosha. Kama unatilia shaka hilo angalia kwa makini kama unampenda jirani yako kama Mungu alivyokupenda. Mungu alikufa kwa ajili yako.)

1. Mwanaume (mwanamke) wa Gomora, je, unamtendea vipi masikini na asiyejiweza?

I. Soma tena Isaya 1:18-20. Je, ujumbe wa Isaya kwetu ni upi kuhusu mavazi? (Kama ukiyafikiria (kwa kutafakari), utaona kuwa dhambi zako zinaweza kubadilika kutoka nyekundu hadi kuwa nyeupe kwa uoshaji wa njia moja tu.)


1. Je, maneno “utayari/radhi/hiari,” “pinga/kinza/bisha” na “uasi” yanajihusishaje na hii njia moja ya wokovu? (Huu ni mitazamo.)

a. Je, hiyo inamaanisha kuwa tunaamini kwenye haki kwa mtazamo? Mtazamo wetu unatuokoa au unatusababisha tupotee?

b. Vipi kuhusu wazo kwamba hatuwezi kufanya jambo lolote kustahili wokovu? Je, kuna jambo la ziada linalosema kuwa mtazamo wetu ni wa kipekee?

J. Soma Isaya 1:21-23. Mungu anamaanisha nini anapouita “mji mwaminifu” kuwa “kahaba?” (Watu wamemgeuka Mungu. Sio waaminifu kwake. Sio waaminifu kwenye kanuni zake. Hawaakisi upendo wake kwa sababu hawawatendei yatima haki. Kwa hakika, hata wamekataa kuwasikiliza na kuwawasilii wajane.)

1. Je, hili ni tatizo la kimtazamo? (Ndiyo!)

K. Tunapozungumzia “imani,” je, kweli tunamaanisha “mtazamo?” (Nadhani hivyo. Imani sio maneno matupu (Yakobo 2.) Imani ni mtazamo. Ni mtazamo kwamba Mungu anatupenda sana kiasi kwamba aliiacha mbingu na kufa kicho cha mateso kwa ajili yetu. Kwa hiyo lazima tumpende na “jirani” yetu ambaye pia alimfia (alimfilia). Tunajua hatuwezi kufikia kiwango cha “Msamaria” wa Mungu. Kwa hiyo tunakubali (tunapokea) haki kwa imani ya Yesu na kwa shukrani tukifuata kiwango cha Msamaria.)

III. Vazi la Utukufu

A. Soma Isaya 61:1-3. Je, masikini, waliovunjika moyo, mateka na wafungwa ni akina nani? (Hawa sio tu watu wasiokuwa na fedha. Hii inamaanisha watu walio masikini kwa sababu maisha yanakwenda mrama na hawana injili.)


B. Soma Isaya 61:10-11. Je, habari njema ya injili imefanywa kuwa mpya/ya kisasa kutoka katika nyakati za Isaya? (Wokovu wetu unatoka kwa Mungu pekee. Anatupatia “vazi la wokovu” “vazi la haki.” Anawapatia wale wanaotambua kile ambacho sheria inawataka kutenda, wanatambua upungufu wao katika kuitunza sheria, na wana mtazamo wa upendo kwa “masikini” (wa aina zote) wanaowazunguka. Mtazomo huu unabubujika kutoka kwenye furaha ya wokovu wetu tusioustahili. Unachokonoa zawadi ya upendo kwa wale wanaotuzunguka.)

C. Rafiki, je, moyo wako bado haujavunjika? Je, umetambua kwamba sheria inaleta mbele yako kiwango cha Msamaria kwa walio wahitaji, lakini umeshindwa kwa masikitiko kufikia hicho kiwango kwa sababu mara zote unajaribu kujihesabia haki? Kwa nini sasa hivi usikubali kwamba kamwe huwezi kufikia kiwango kwa nguvu zako mwenyewe? Kubali kwamba unahitaji zawadi ya vazi la neema na haki. Kwa nini usimwache Mungu avunjevunje moyo wako na kukufungulia njia ya furaha na upendo kwa walio masikini?

IV. Juma Lijalo: Alama Iliyonyakuliwa Kutoka Motoni

0 comments:

Post a Comment