Friday, June 24, 2011

Somo la 1: Ibada Katika Kitabu cha Mwanzo: Madaraja ya Waabudu

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Mwanzo 4 & 22)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Nimebaini mabadiliko ya utamaduni nilipokuwa mtu mzima. Nilipokuwa kwenye makuzi (ukuaji) katika mazingira ya Kikristo ya kijijini nchini Marekani, watu ama walikuwa Wakristo au waasi, na waasi kwa ujumla walikubaliana na uasi wao. Waasi hawakutaka kudai kuwa wao ni watu wema, walikuwa jinsi walivyo (walikubaliana na hali yao.) Siku hizi watu wote wanadai kuwa wao ni watu wa “kiroho.” Watu, ambao siku za zamani walikuwa tu ni waasi, sasa wanadai kuwa wana utaratibu binafsi wa kimaadili ambao ni wa hali ya juu kuliko ule unaoelezewa kwenye Biblia. Somo letu juma hili ni kuhusu madai ya hali ya kiroho nje ya ule ulioidhinishwa na Mungu. Kwa vile tunapata huu mwanzo katika kitabu cha Mwanzo, labda “mabadiliko ya utamaduni” niliyoyasema hapo awali, ni mabadiliko tu ya uelewa wangu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kujifunza zaidi!


I. Majuto ya Wazazi

A. Soma Mwanzo 4:1. Fikiria furaha na maajabu/mshangao kwenye uzao wa kwanza katika historia ya mwanadamu! Je, Hawa alimpa sifa nani? (Mungu.)

1. Unafahamu kisa cha anguko la wanadamu dhambini (Mwanzo 3), unadhani Adamu na Hawa walikielezeaje kwa Kaini?

a. Je, unadhani bado walikuwa wanamlaumu mtu fulani kwa ajili ya anguko? (Angalia Mwanzo 3: 12-13.)

1. Kama wewe ungekuwa Adamu au Hawa, je, ungesisitiza kitu gani kwenye elimu ya kidini kwa Kaini? (Utii kwa Mungu?)

1. Je, unadhani Adam na Hawa walimwambia Kaini kuwa nini kilikuwa madhara makubwa kabisa ya dhambi yao? (Kutokuishi mbele za Mungu?)

I. Wana Wawili, Sadaka Mbili

A. Soma Mwanzo 4:2-5. Kama nipo sahihi kwamba Kaini alilelewa kwa mtazamo kwamba anapaswa kutii, je, unaielezeaje sadaka yake? Kama wewe ungekuwa Kaini, je, ungethibitishaje chaguo lako la kutoa sadaka? (Uanuwai/utofauti! Kila mtu ana talanta tofauti, thawabu na uwezo. Nitampatia Mungu kitu kilicho na maana kwangu – kinachoakisi talanta na kazi zangu. Kuna barabara nyingi za kuielekea sadaka, na nitapita kwenye barabara ambayo inaendana na jinsi nilivyo.)

1. Soma Mambo ya Walawi 17:11. Vipi kuhusu kafara ya damu iwe ndio kafara inayojitosheleza? (Hatuoni maelekezo ya wazi kwa Adamu na Hawa na watoto wao kuhusu jinsi ya kutoa sadaka. Hata hivyo, taarifa ya kuwa uchi ikiwa ni matokeo ya dhambi (Mwanzo 3:6-7) na uvishaji wa Mungu wa nguo za ngozi (kifo cha mnyama ili kuficha dhambi ya wanadamu – Mwanzo 3:6-7) inafunua mpango wa Mungu. Bila shaka ndio maana Mungu alitoa maelekezo, haikuandikwa tu kwenye Biblia.)

A. Hebu turejee Mwanzo 4:5. Kama Kaini hamtii Mungu, kwa nini anaghadhibika? (Lazima atakuwa alikuwa na sababu za kuamini kuwa yupo sahihi. Hiyo inapendekeza kuwa kiukweli kabisa aliamini “uanuwai wa thawabu” ulikuwa ni jibu sahihi kwa maelekezo mahsusi ya Mungu (na kinyume chake.)

A. Soma Mwanzo 4:6-7. Je, hii inatuambia nini kuhusu asili ya maelekezo ya Mungu kuhusu ibada kwa Kaini? (Kauli za Mungu zinafunua kwamba Kaini alifahamu vema. Alijua cha kufanya. Mungu anasema kuwa suala ni rahisi: tii! Bila shaka ndio maana hili lilionekana kama vile kwa wazazi wake.)

1. Je, nini kilicho mbadala wa utii kwa Kaini? (Kaini atatawaliwa na dhambi.)

1. Kwa nini Mungu anaielezea dhambi kana kwamba ni kitu chenye uhai? Mnyang’anyi/mporaji wa aina fulani? (Sura iliyotangulia inamwelezea Shetani kama mnyama anayetafuta kumdanganya Hawa. Mwanzo 3:1-5. Dhambi sio ya kupita, ni kama mporaji.)

1. Uvishaji wa mavazi ya ngozi na maelezo ya Mambo ya Walawi 17:11 ya upatanisho wa damu vinatuonyesha kuwa haki kwa imani, na sio matendo binafsi, tayari vipo kama mpango wa Mungu. Kama hiyo ni kweli, kwa nini Mungu yu mahsusi kabisa kuhusu sadaka ya Kaini? (Wokovu sio mpango wa “njia nyingi.” Ni ama utoe kafara ya damu, au uwe na sadaka isiyokubalika.)

A. Angalia tena Mwanzo 4:7. Je, hii inaendana vipi na neema – haki kwa imani? Mungu anawezaje kuwaambia wanadamu “waishinde” dhambi? (Neema ni uchaguzi. Ama tunaweza kuishi maisha ambayo tunakubali neno la Mungu na kujaribu kuishi kulingana na neno hilo, au tunaweza kufanya kanuni zetu wenyewe zinazoendana na hisia zetu wenyewe za usahihi na ubaya, na kupuuzia kanuni za Mungu. Neema inahusisha uchaguzi.)

I. Matokeo ya Sadaka Isiyo Sahihi

A. Soma Mwanzo 4:8-9. Je, unawezaje kuelezea hili? Ni kwa jinsi gani kimantiki Kaini alitoka kwenye lawama ya Mungu hadi kwenye mauaji yaliyodhamiriwa? (Hii inatupatia dira ya wazi ya wale wanaokubali haki kwa imani na wale wasiokubali. Kama Kaini angesema tu, “Sawa Mungu, nimetenda dhambi, nitafuata maelekezo yako” angekuwa salama. Badala yake, sio tu kwamba aliendelea kuasi dhidi ya Mungu, alimghadhibikia ndugu yake aliyetii. Utii wa Habili ulikuwa ni karipio kwa Kaini. (Na unashangaa kwa nini chombo cha habari cha taifa kina uhasama/uadui kwa wale wanaotafuta kuitii Biblia!) Mitazamo miwili iliyowasilishwa na wana wawili kimsingi inatofautiana.)

A. Soma Mwanzo 4:10-12. Je, unafikiria nini kuhusu hukumu iliyowekwa na Mungu?

1. Je, ungetoa hukumu kali zaidi ya hiyo?

1. Je, adhabu ya Kaini ni ipi kwa hakika? (Hawezi kuwa mkulima tena. Atakuwa “mtoro” na mtu asiye na kikao duniani.

a. Je, hii inaendana na adhabu yoyote iliyowekwa na Mungu siku hizi? (Tunawaona wanadamu ambao, ikiwa ni matokeo ya fedheha ya dhambi, wanafukuzwa kutoka kwenye taaluma wanayoipenda.)

A. Soma Mwanzo 4:13-14. Je, Kaini ametubu? (Kamwe hasemi kuwa anaomba msamaha kwa mauaji. Anahoji kuwa adhabu yake imekuwa kubwa. Ana wasiwasi kwamba mtu fulani mwingine tofauti na Mungu atampa hukumu.)

1. Baini hili lalamiko jingine: kwamba atasitirika mbali na uso wa Mungu. Je, hii inaonyesha kuwa ametubu kwa dhati? (Naamini kuwa majuto makubwa kabisa ya Adamu na Hawa yalikuwa ni kutengwa kwao na Mungu. Bila shaka walishiriki haya majuto na Kaini alipokuwa anakua. Ghafla, Kaini anakumbuka hili, na kuelewa kuwa ameanguka kwenye shimo lile lile – refu zaidi tu.)

A. Soma Mwanzo 4:15-16. Je, unaelezeaje haki ya Mungu? Je, haikumpasa kumwua Kaini pale pale? (Hii inaonyesha upendo na neema ya Mungu hata kwa mtu ambaye haonekani kutubu.)

A. Soma Mwanzo 4:14 na Mwanzo 4:17. Wale wanaopinga kumwabudu Mungu kama Muumba wanatumia haya mafungu mawili kuashiria kuwa Biblia haina suala halisia la uumbaji. Je, tuliwapata wapi hawa watu wengine wote? Wanasema, “Adamu na Hawa ni ishara tu ya watu wengine wengi walioumbwa na Mungu (au waliobadilika).” Je, unaelezeaje hili? (Soma Mwanzo 4:2-3. Baini “ikawa hatimaye akamzaa ndugu yake” (inayoruhusu kuzaliwa kwa mabinti kabla ya Habili) na “katika kipindi fulani,” inayotutaarifu kuwa kipindi fulani ambacho hakikuelezewa kilipita bila maelezo ya matukio yaliyotokea. Hakuna sababu kwa nini hiki kipindi kisingeweza kuwa miaka 200 – hata kwa idadi ya watu kutokea.)

A. Baada ya kusoma kisa hiki, unawezaje kuelezea mtazamo wa Mungu kuhusu njia anuwai/mbalimbali za wokovu? (Tunaonyeshwa Mungu mwenye upendo na rehema, lakini pia Mungu aliye na kanuni na anayezitekeleza.)

I. Abramu

A. Soma Mwanzo 12:1-3. Kama wewe ungekuwa Abramu, je, ungeondoka? (Hivi ni vichocheo vya kupendeza vya kufanya uondoke!)

1. Unadhani ni kwa nini Mungu alimtaka Abramu kuhama? (Hii inaleta wazo la utengano. Wale wanaomwabudu Mungu wanahitajika kuwa na nafasi kutoka kwa wale walio wakatili kuhusu ibada ya Mungu.)

1. Soma Mathayo 9:10-13. Je, tunalinganishaje hizi taswira mbili? (Mungu anatuita kuuhubiri ulimwengu, sio kuushambulia. Lakini, Mungu anatamani sisi tuwe na utengano fulani na dunia.)

A. Soma Mwanzo 22:1-2 na Mambo ya Walawi 20:1-3. Je, ungetoa hoja gani dhidi ya utii kama wewe ungekuwa Ibrahimu? (Mungu aliniahidi uzao mwingi! Mungu alinitaka nitengane, lakini hiki ndicho kitu ambacho kinafanywa na ulimwengu.)

A. Soma Mwanzo 22:3-5. Je, Ibrahimu anawadanganya watumishi wake kuhusu kurejea kwa Isaka?

A. Soma Mwanzo 22:6-8. Je, Ibrahimu anamdanganya Isaka?

A. Soma Mwanzo 22:9-14. Je, Mungu alitoa kafara kama jinsi Ibrahimu alivyomuahidi Isaka? (Ndiyo!)

A. Je, kisa hiki kina uhusiano wowote na kisa cha Kaini? (Vyote vinahusisha utii. Kaini aliitwa kutii dhidi ya vipaumbele vyake. Ibrahimu aliitwa kutii hata pale ambapo haikuleta mantiki ya kiteolojia.)

1. Je, tunajifunza nini kutoka kwa Ibrahimu? (Ibrahimu hakuamini Mungu angemtaka amuue mwanaye. Lakini bado aliendelea kutembea katika utii.)

A. Unapochukulia kisa cha injili, je, ni somo gani jingine tunalolipata kwenye kisa cha Ibrahimu na Isaka? (Mungu alimtoa mwanaye. Mungu ana sifa mbili za asili, upendo wa ajabu kwetu, na matarajio yake ya utii wetu.)

A. Rafiki, je, unajaribiwa kupuuzia mojawapo ya kanuni za Mungu kwa sababu ipo nje ya utamaduni wa sasa au mwelekeo wa kivitendo maishani mwako? Je, utamwomba Roho Mtakatifu leo kukupatia mtazamo wa Ibrahimu, kwamba utamtii Mungu bila kujali kama ni umaarufu au sio rahisi?

I. Juma Lijalo: Ibada Katika Kitabu cha Kutoka: Kumwelewa Mungu ni Nani.

0 comments:

Post a Comment