Thursday, June 9, 2011

Somo la 12: Vielelezo Zaidi vya Mavazi

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

Zingatia:
Mwandishi wa somo hili anasema kuwa kama yalivyo maneno yasiyokuwa ya kawaida – “Walmart” ni maduka makubwa ya rejereja kule Marekani. Yana bei za chini za bidhaa, yana bidhaa nyingi na yanauza karibia kila kitu. Baadhi ya maduka ya Walmart yanakuwa wazi kwa muda wa saa 24. Watu wengi masikini wananunua vitu kwenye maduka hayo, lakini hata mwandishi (Profesa Bruce Cameron) pia anafanya manunuzi kwenye maduka hayo! Matabaka yote ya jamii wanafanya manunuzi pale – isipokuwa labda watu wenye hadhi ya juu kabisa. Mwandishi anapendekeza kuwa kama kuna maduka ya aina hiyo nchini kwako, basi uwe huru kutumia maduka hayo badala ya Walmart. Hapa kwetu Tanzania tumetumia maduka ya Kariakoo ambapo kwa kiasi fulani yanashabihiana na hayo maduka ya Walmart. Nawe pia jisikie huru kutumia maduka mbadala ya aina hiyo yanayopatikana mahali ulipo. Angalizo hili linahusika pia kwenye somo la juma lililopita la “Vazi la Harusi.”

Somo la 12: Vielelezo Zaidi vya Mavazi
(Marko 5, Yohana 13 & 19, Mathayo 26-27)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.


Utangulizi: “Mtu anamuuma mbwa.” “Kisasi cha wapumbavu.” “Mwanaume mwenye sura mbaya anamwoa binti mrembo.” Kauli hizi zinatupatia habari zisizotarajiwa. Kwa kawaida mbwa huuma watu, mabarubaru (vijana wadogo wanaochipukia na walio katika umri wa kubalehe) maarufu, werevu na wenye mwonekano mzuri wanaonekana kutapakaa, na mwanaume mzuri anamwoa binti mzuri. Vipi kama Ufalme wa Mungu una kila kitu kinyume chake? Je, Mungu anaongoza ufalme wa wapumbavu? Au, je, hivyo ndivyo tu ulimwengu unavyofikiria? Kama Mungu ana mambo yenye kinyume, kwa nini? Je, kuna mbaraka katika hili kwa mtu wa kawaida? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kubaini!

I. Ushindi wa Najisi

A. Soma Marko 5:21-24. Unadhani ni kwa nini Yesu alikwenda pamoja na Yairo? (Yairo alikuwa na jambo la dharura. Alikuwa na imani. Alikuwa mkuu wa sinagogi.)

B. Soma Marko 5:25-26. Hebu jiweke kwenye nafasi ya huyu mwanamke. Je, ungejisikiaje? (Amechanganyikiwa. Ametumia fedha zake zote akitafuta matibabu, na alikuwa anaendelea kujisikia vibaya zaidi.)

C. Soma Marko 5:27-28. Je, huu ni mpango wa namna gani? (Soma Mambo ya Walawi 15:25-27. Hapaswi kumgusa Yesu kwa sababu atamfanya kuwa najisi. Hiyo itamfanya Yesu kupitia mchakato wa utakaswaji.)

D. Soma Marko 5:29-34. Je, ni bahati mbaya tu kuwa huyu mwanamke aliponywa? Je, Yesu hana udhibiti wa nguvu/uwezo wake mwenyewe? (Mwanzoni kisa kinataka kuonekana kuwa kama hivyo, lakini tunaona kuwa uponywaji wake ni thawabu ya imani.)

E. Soma Marko 5:35. Kama Yesu angekuwa hapotezi muda kijingajinga na huyu mwanamke, je, binti wa Yairo angekufa?

1. Jiweke kwenye nafasi ya Yesu. Una watu wawili wahitaji: binti mdogo wa mkuu wa sinagogi aliye katika hali ya dharura, na mwanamke najisi aliye na ugonjwa sugu usio wa dharura. Je, ungemwona yupi kwanza? (Kutokana na mtazamo wa watazamaji, uamuzi wa Yesu kwa hakika hauna maana yoyote.)
2. Je, unaweza kutafakari uamuzi wa Yesu kama unaleta maana yoyote? (Yesu hajali hadhi ya mtu yeyote. Yesu hajali muda. Kama ukiendelea kusoma hiki kisa, Yesu anamfufua huyu msichana mdogo. Anafanya kila kitu kwa usahihi, kwa mujibu wa ratiba yake.)


II. Ushindi wa Mwosha Miguu

A. Soma Yohana 13:1-8. Kwa nini Petro anapinga Yesu kumwosha miguu yake?

B. Soma Marko 14:10-11. Kwa nini Yuda anamsaliti Yesu?


C. Soma Mathayo 20:20-21. Kwa nini mama wa Yakobo na Yohana (Angalia Marko 10:35) anaomba kwamba wanawe wawe kwenye nafasi ya juu kwenye Ufalme wa Yesu? (Maswali yote matatu yana jibu moja. Petro anaamini kuwa Yesu anakaribia kuwa Mfalme. Yuda anaamini kuwa kama akimtia Yesu “kashikashi” kidogo, Yesu ataonyesha uwezo wake na kuwa Mfalme. Mama anaamini Yesu atakuwa Mfalme.)

D. Hebu turejee kwenye Yohana 13:3-4 kuhusiana na chakula cha jioni cha Pasaka. Je, nini kipo mawazoni mwa wanafunzi? (Wanataka kuonyesha kuwa wao ni wa muhimu sana. Wanastahili nafasi za juu kwenye ufalme ujao wa Yesu. Kwa hiyo, hawadiriki kuruhusu waonekane wadhaifu kwa kuosha miguu ya mmoja wa wapinzani wao.)

1. Je, nini kimo akilini mwa Yesu? (Yesu anajua kuwa kila kitu kimewekwa chini ya uwezo wake!)

2. Je, hii inahusianaje na kisa cha Yairo? (Yesu anaonyesha mfano wa utume ambao hakuna aliyeutarajia. Anamtumikia kila mmoja bila kujali mahali pao maishani au mahali pake.)

3. Je, hii inafanya kazi kwa wale tu ambao (kama Yesu) wanafahamu wao ni Mungu? (Mambo mawili. Kwanza, Yesu alikuwa na mambo ya kutisha yenye kufedhehesha mbele yake. Pili, uhusiano wetu na Mungu unapaswa kuwa chanzo cha ujasiri wetu – ujasiri unaoturuhusu kutumikia.)

III. Ushindi wa Mshitakiwa

A. Soma Mathayo 26:59-61. Chukulia kwamba unashughulikia mashtaka ya kesi dhidi ya Yesu? Je, tatizo ni lipi? (Watoa mashtaka wanatafuta “ushahidi wa uongo” na wana mashahidi wengi wa uongo wa kujitolea. Tatizo lazima liwe kwamba hakuna hata mmoja wa hawa mashahidi wa uongo wanaaminika.)

1. Kwa nini wale wawili hatimaye walishuhudia ukweli? (Inaonekana kama kile alichokisema Yesu kwenye Yohana 2;9)

2. Je, unaweza kuuweka huu ushuhuda kwenye kumbukumbu? (Swali ni kwamba, “Ili iweje?” Jinsi ushuhuda unavyotoka, inaonekana kana kwamba Yesu ana wazimu, sio mhalifu.)

B. Soma Mathayo 26:62-63. Unadhani ni kwa nini Yesu alinyamaza? (Soma Kumbukumbu la Torati 17:6. Sehemu ya sheria ya Mungu ni haki ya kukaa kimya kwenye hukumu ya kesi ya kifo. Kujiponza/kujitia hatarini mwenyewe kulizuiwa. Yesu aweza kuwa alikuwa anadai haki yake dhidi ya kujitia hatarini yeye mwenyewe. Yaweza pia kuwa shtaka ni la kebehi/dhihaka sana kiasi kwamba Yesu alilichukulia kutostahili kupatiwa jibu.)

C. Soma Mathayo 26:63-66 na Mambo ya Walawi 21:10. Nani anapaswa kushtakiwa hapa? (Kuhani Mkuu. Anakiuka kanuni ya “mashahidi wawili” kwenye hukumu za vifo, na anakiuka kanuni dhidi ya kurarua vazi lake. Katika Mamo ya Walawi 10:6 Haruni anaonywa kuwa kama atakiuka hii kanuni atakufa.)

1. Kwa nini Kuhani Mkuu alifanya kile alichokifanya? (Aliweza kufanya hivyo. Alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo.)


D. Yesu alipokuwa akipitia huu mchakato, nini kilikuwa kinakuja kufikia mwisho wake? (Mfumo wote wa hekalu (patakatifu). Sio tu kwamba Kuhani Mkuu alirarua vazi lake, lakini pazia la hekalu lilipasuka kutoka juu hata chini (Marko 15:38-39). Mamlaka zilipotosha ujumbe wa Mungu wa Mwanakondoo wa Mungu. Nguvu/uwezo ulibadilishwa na uchaji wa Mungu.)

IV. Ushindi wa Uvumilivu

A. Soma Mathayo 27:27-31. Baini kuwa ishara za mfalme zilikuwa ni njia ya kumdhalilisha Yesu. Kwa nini Shetani alitia moyo huu udhalilishaji mahsusi? Je, nini kilikuwa mawazoni mwa Shetani? (Kumbuka kwamba dhambi ya Shetani ya awali ilikuwa ni kutaka kuwa kama Mungu. Isaya 14:14-15. Dhambi ya asili ya mwanadamu ilikuwa ni kutaka kuwa kama Mungu. Mwanzo 3:1-4. Shetani aliamini kwamba kama alitilia shaka na kukejeli hadhi ya Yesu kama Mungu, Yesu angeivunja.)

B. Je, unataka iweje watu wanapokutania? Vipi kama wapo dhati kabisa kuhusu ukweli kwamba wanadhani una hadhi ndogo?

1. Je, unajibu vipi/unafanya nini pale watu wanapokutendea bila heshima? Vipi kuhusu pale ambapo watu wasiokuwa watiifu wanatoka katika “hali ya chini” maishani?

C. Kwa nini Yesu hakuvunja? (Kwa sababu hakuwa kama Shetani na hakuwa kama Hawa/Eva na hakuwa kama wewe na mimi. Alikuwa mnyenyekevu. Na uvumilivu wake ndio uliomfikisha kwenye hili jaribu la kutisha. “[Yesu], akiwa katika asili ya Mungu, hakuchukulia usawa wake na Mungu kuwa kitu cha kung’ang’ania.” Wafilipi 2:6)

D. Je, hivi visa viwili vya mwisho vinatufundisha nini kuhusu asili ya mamlaka? (Shetani na mawakala wake walitumia mamlaka, na matamanio ya uongozi, na tamaa ya mamlaka, kuendeleza ufalme wao usiokuwa wa haki. Mamlaka hayataongeza hadhi yako kwa Mungu, lakini inaweza, kuongeza urahisi wa kumwangukia Shetani.)

V. Ushindi wa Mavazi Yaliyopotea.

A. Soma Yohana 19:23-24. Je, udhalilishaji wa Yesu wa mwisho ni upi? (Kwamba anachapwa akiwa uchi na mavazi yake walipewa wauaji wake.)

B. Soma Warumi 8:1-4. Je, udhalilishwaji wa Yesu ulitufanyia nini sisi? (Ulitupatia fursa ya uzima wa milele wenye utukufu.)

C. Hebu tutafakari huu mfululizo wa visa kuhusu mavazi. Yesu (angalao kwa muda fulani) anampendelea mwanamke najisi dhidi ya Yairo, Yesu anaonyesha mfano wa unyenyekevu wa kuosha miguu, Yesu (Kuhani Mkuu wa mwisho) anatiwa hatiani kwa uwezo mbadhirifu wa Kuhani Mkuu, Yesu (Mfalme wa Wafalme) haheshimiwi kama mfalme, Yesu anadhalilishwa msalabani ili kutupatia uzima. Je, ni masomo gani tunayopaswa kujifunza kutokana na hili? (Kama kweli tunataka kuwa kama Mungu (mwangalie Hawa), basi tutaweka kando kiburi/majivuno yetu. Mungu amebadilisha mpango wa mambo ya kidunia. Anaendeleza unyenyekevu. Haangalia masuala ya hadhi. Anahamasishwa na upendo unaowatendea watu wote kwa usawa.)


D. Chukulia masomo yetu mawili ya nyuma. Kwenye kisa cha mwana mpotevu, kijana mkubwa “mwema” yupo hatarini kuipoteza mbingu, wakati kijana mdogo “mwovu” anaingia kwenye uzima wa milele. Kwenye kisa cha harusi ya mwana wa mfalme, marafiki na wanaostahili ufalme wanakataliwa ilhali wanunuzi wa maduka ya Kariakoo wanaingia mbinguni. Katika somo la juma hili tunajifunza kuwa unyenyekevu ni kitu cha kunga’ng’ania, na mamlaka ni mtego. Je, Yesu amefanya mambo kinyume mpango mzima wa mambo?

1. Kama ndivyo, kwa nini? Kwa nini dunia imepinduliwa juu-chini na hakuna kitu hata kimoja kinatokea kama tulivyotarajia? (Soma Mika 6:8. Hiki ndicho kiini cha injili – kuitafuta haki na rehema na kutembea kwa unyenyekevu na Mungu wetu aliyetembea kwa unyenyekevu.)

2. Je, hii ni habari njema? (Ndiyo! Njia hii ipo wazi kwa kila mtu. Hata watu wa “kawaida” wanastahili. Kwa hakika, wanaweza kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi.)

E. Rafiki, je, unafuata mfano wa unyenyekevu? Je, unawajali wanaoonewa/wanaokandamizwa/watu hohe hahe na wasio na uwezo? Au, je, lengo lako maishani ni kutafuta uwezo na mamlaka? Kwa nini usomwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, kuubadilisha moyo wako?

VI. Juma Lijalo: Kumvaa Kristo

0 comments:

Post a Comment