Friday, June 17, 2011

Somo la 13: Kumvaa Kristo

Somo Limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Warumi 8 & 13, 1 Wakorintho 15)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kwenye masomo kadhaa yaliyopita tulitatizika pale tulipojifunza kuwa Wakristo “wema” wanaweza kuwa kama yule kijana mkubwa kwenye kisa cha mwana mpotevu (Luka 15), au Wayahudi washika dini kwenye kisa cha “Msamaria Mwema” (Luka 10), au marafiki wa mfalme kwenye kisa cha sherehe ya harusi katika Mathayo 22. Wasomaji wa masomo “wenye haki hafifu”, kwa upande mwingine, walikuwa wakifurahia. Wokovu kwa neema ni sababu nzuri ya kufurahia na kuendelea kufurahia. Lakini, Mungu anatupatia sote (Wakristo “wema” na “wabaya” kwa pamoja) habari za kufikiria kwa umakini pale anapoelezea (Mathayo 7:13-14) kuwa njia ya kuelekea wokovuni ni “nyembamba” na “ni watu wachache tu wanaoifuata.” Je, inawezaje kuwa “nyembamba” wakati imepewa kwa wote wanaoamini? Je, kuvaa vazi la harusi la wokovu ni tukio la mara moja ambalo tunaweza kusahau baadaye? Au je, ni zaidi ya hapo? Hebu tuzame kwenye somo letu la kujifunza Biblia na kubaini!

I. Wokovu Maridadi

A. Soma Warumi 10:1-4. Je, Waisraeli wana tatizo gani? Je, wao ni wavivu? (Hapana. Wana “juhudi kubwa,” ikimaanisha “wachapa kazi.” Tatizo ni kwamba hawaelewi injili. Wana pengo kwenye uelewa wao.)

B. Ukiendelea kusoma Warumi sura ya 10 na 11 utajifunza kuwa wokovu unatokana na kuamini, lakini tatizo ni kuelewa. Soma Warumi 12:1-2. Je, Paulo anaonya dhidi ya kushindwa kupi? (Usiifuatishe namna ya dunia hii.)

1. Kwa nini hili liwe tatizo kama tuliokolewa kwa neema? (Baini kuwa Paulo bado anazungumzia kuhusu maarifa. Kama tunabadilishwa na injili, basi “tutakuwa na uwezo wa kujaribisha na kuthibitisha mapenzi ya Mungu ni yapi – mapenzi yake makamilifu, mema na ya kupendeza.” “Kupima/Kujaribisha” kitu fulani ni kujifunza zaidi kuhusiana na kitu hicho.)

a. Huu unaonekana kuwa kama mradi wa sayansi – tunajaribisha kitu fulani ili kuwa na uhakika kuwa ni cha kweli. Unadhani ni kwa nini kufuatisha namna ya dunia inamaanisha kuwa hatuwezi kufanya jaribio kikamilifu? (Tatizo la Waisraeli wa wakati wa Paulo ni kwamba hawakuelewa mapenzi ya Mungu kikamilifu. Nasi tuna changamoto iyo hiyo – jinsi ya kuelewa mapenzi ya Mungu. Kama tunabadilishwa na injili, badala ya kuufuatisha ulimwengu, tunapewa vifaa vya kumpima/kumjaribu yule anaeyaelezea mapenzi ya Mungu kwa usahihi. Kama wewe ni wa dunia, uwezo wako wa kupima/kujaribisha u butu/umefifia sana.)

II. Upendo wa Dhati

A. Soma Warumi 12:9-13. Je, kuna upendo usio wa dhati? (Ndiyo!)


1. Kama unapenda uovu, je, upendo wako kwa Mungu si wa dhati? (Haya mafungu yanapendekeza mfululizo wa viwango vya upendo wa dhati. Inaonekana kwamba upendo wa dhati unahusisha kujitolea nafsi kwa umadhubuti.)

2. Kwa kuzingatia mafungu tuliyoyasoma, je, itakuwa haki kuhitimisha kuwa kutokuelewa kwa Waisraeli waliomkataa Yesu kulitokana na upendo usio wa dhati?

a. Je, upungufu wa maarifa na upungufu wa upendo wa dhati ni kitu kimoja katika huu muktadha? Kama sivyo, je, vinafanana? (Hebu tuendelee, tunahitaji taarifa zaidi!)

B. Hebu tuendelee kusoma hoja ya Paulo. Soma Warumi 13:1-5. Kama tunampenda Mungu, je, mtazamo wetu kwa serikali unapaswa kuwa upi? (Hatupaswi kuwa waasi!)

1. Kwa nini kuna kiungo kati ya upendo wa dhati kwa Mungu na mtazamo wa unyenyekeaji dhidi ya serikali? (Warumi 13:1 inasema kuwa Mungu aliiweka mamlaka.)

C. Soma Warumi 13:6-8. Je, kodi na ushuru vina kitu gani cha kufanana? (Kumpenda Mungu inamaanisha kuwa sisi ni raia wema. Tunalipa kodi zetu na tunalipa ushuru.)

D. Soma Warumi 13:9-10. Je, wale waliookolewa kwa neema wanatii Amri Kumi? (Ndiyo!)

1. Kwa nini? (Zimetokana na wajibu wetu wa kuwapenda wengine.)

a. Hebu tupitie hitimisho letu la “upendo wa dhati.” Je, kutii Amri Kumi na kuonyesha ukarimu kwa jirani zetu ni jaribio la udhati wa upendo wetu? (Kama tunabadilishwa na injili, badala ya kuendana na dunia, tunaweza kuona hili kama jaribio la kweli.)

b. Hebu tupitie pia suala la kama upungufu wa maarifa na upungufu wa upendo wa dhati vinaendana? (Ndiyo, vinaendana. Kama huelewi kuwa upendo wa dhati unaakisiwa kwenye maisha yaliyobadilika, basi hauielewi injili.)

E. Mkumbuke kijana mkubwa kwenye kisa cha mwana mpotevu? Soma Luka 15:28-30. Je, ungechukulia mtazamo wa kijana mkubwa kuwa ule wa “upendo wa dhati?” (Hakujisikia kumpenda baba yake au ndugu yake. Alichukulia huduma yake na utii wake kwa baba yake kuwa kama utumwa!)

1. Je, neema inatutoa nje ya utii? (Sio kwa njia yoyote ile. Neema inamaanisha kuwa utii wetu unahamasishwa na upendo, sio wajibu. Kijana mkubwa alifahamu kuhusu wajibu, hakuonekana kuwa na ufahamu mkubwa kuhusu upendo. Kwa uthibitisho zaidi wa wazo kwamba neema, upendo na utii vinahusiana, soma Warumi 6.)

III. Kuelekea Kwenye Maisha ya Neema – Mtazamo Wenye Sehemu Mbili


A. Kwa hiyo, hii inatokeaje maishani mwako? Je, tunapataje upendo wa dhati unaoishia kuwa na mtazamo chanya dhidi ya Mungu, serikali na wale wanaotuzunguka? Je, tunasaga meno yetu na kufumba midomo? (Isipokuwa, kama Waisraeli,, nimechanganyikiwa kuhusu hili, nimeishi muda mrefu vya kutosha kutambua kwamba hii ni rahisi sana kuandika kuihusu, lakini sio rahisi sana kuitenda. Upendo sio kitu kinachotokana na kudhamiria, udhati au wajibu.)

B. Ninaamini kuwa kuna sehemu mbili za kuishi maisha ya kweli ya neema. Soma Warumi 8:1-4. Je, tunatimizaje matakwa ya haki ya sheria? (Yesu alitimiza “matakwa ya haki ya sheria” kwa ajili yetu. Yesu alifanya hivyo kwa niaba yetu. Hiyo ndio sehemu ya kwanza. Huo ulikuwa ni unyanyuaji wa mzigo mzito kwa Yesu, lakini sio kwangu.)

1. Baini kwamba Warumi 8:4 inaonekana kusema kuwa Yesu anatimiza matakwa ya haki ya sheria “ndani yetu, tusioishi kwa mujibu wa asili ya dhambi.” Je, hiyo inamaanisha kuwa kitu fulani hivi kinahitajika kwetu sisi kustahili kwa ajili ya sehemu ya kwanza? (Kwa hakika inaonekana kuwa hivyo. Hii inaonekana kuwa sawa kabisa na “upendo wa dhati” tuliojadili hapo kabla.)

C. Soma Warumi 8:5-8. Je, tunaepukaje kuishi kwa mujibu wa asili yetu ya dhambi? (Tunafanya uamuzi wa kuziweka akili zetu kwa kile ambacho Roho Mtakatifu anakitamani badala ya kile ambacho asili yetu ya dhambi inakitamani.)

D. Hebu turukie mbele kwa muda kidogo. Soma Warumi 8:12-15. Tunamtumiaje Roho kuyaweka mautini “matendo mabaya ya mwili?” (Hii inapendekeza mwendelezo – kuishi kwa mujibu wa Roho kunatufanya tubaini, na kisha kukataa (“kuyaweka mautini”), yale mambo yaliyo dhambi.)

E. Soma Warumi 8:9-11. Je, ni muhimu kiasi gani kuwa na Roho Mtakatifu hai maishani mwetu? (“Kama mtu yeyote hana Roho wa Kristo, basi yeye si wa Kristo.” Inaashiria matokeo ya milele ya maisha yetu – mbingu au upotevu.)

F. Ni kwa jinsi gani basi, unaelezea kuvaa vazi la Yesu la haki? (Kwa hakika sio kitu cha wakati mmoja. Sio jambo la “kusaga meno yako na kutii.” Kwanza ni (sehemu ya kwanza) uamuzi wa kukubali kafara ya maisha makamilifu ya Yesu kwa niaba yetu. Na pili (sehemu ya pili) ni uchaguzi wa kila siku wa kuongozwa na Roho Mtakatifu. Hiki ndicho ambacho Warumi inakiita “upendo wa dhati.”)

1. Ni sehemu gani ya hili ambayo Waisraeli wa wakati wa Paulo hawakuielewa? (Hawakuelewa sehemu ya kwanza (Yesu ndiye kafara ya Mwanakondoo wa Mungu). Yesu alisema walikuwa kama kijana mkubwa kwenye kisa cha mwana mpotevu – walihamasishwa na wajibu, sio upendo. Hiyo inamaanisha kuwa pia walikosa sehemu ya pili.)

2. Je, huu mjadala wa sehemu za muhimu unaharibu imani yetu kwenye wokovu wetu? (Hapana. Tunaokolewa pale tunapoamua kukubali vazi la Yesu la haki. Uamuzi huo unaweza kubatilishwa kama tunaendelea kufanya chaguzi zisizo sahihi. Uamuzi huo unathibitishwa kwa kufanya uamuzi wa kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu. Hii ndio sehemu ya “dhati” ya upendo wetu. Kile Yesu alichotufanyia kinaleta tofauti kwenye mtazamo wetu, na kwa hiyo utofauti maishani mwetu. Bado tuna “matendo yasiyo sahihi ya mwili” ya kuzikwa na uwezo wa Mungu. Lakini, tupo kwenye njia sahihi. Bwana asifiwe!)

IV. Thawabu


A. Soma 1 Wakorintho 15:50-52. Nini kinachoendelea hadi “parapanda ya mwisho?” (Miili yetu na damu. Badiliko la mwisho na la milele litakuja “kufumba na kufumbua” wakati wa Ujio wa Mara ya Pili wa Yesu. Hapo ndipo ubadilishwaji wetu utakamilika.)

B. Soma 1 Wakorintho 15:53-57. Je, ni maadui gani wanaoshindwa? (Sheria, dhambi na mauti.)

1. Kwa nini sheria kamilifu ya Mungu, nakala ya tabia yake, iwe adui aliyeshindwa? (Kwa sababu nguvu ya dhambi ni sheria. Sheria haimwokoi mtu yeyote. Inatuhukumu tu na kutuonyesha hali yetu ya dhambi. Yesu alipoitii sheria kikamilifu, alimwangamiza adui ambaye vinginevyo angehitaji kifo chetu. Kwa sababu hiyo, sheria, dhambi na mauti vyote vimeshindwa.)

C. Rafiki, je, ungependa kuingia kwenye safari ya ubadilishwaji? Je, ungependa kusikia kwamba dhambi na mauti vinashindwa maishani mwako? Kama unataka hayo, basi kubali kwa imani kafara ya Yesu kwa ajili yako, na jitoe kwamba kila siku utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie ili uishi maisha yanayoongozwa na Roho.

V. Juma Lijalo: Tutaanza mfululizo mpya wa masomo kuhusu ibada.

0 comments:

Post a Comment