Thursday, July 14, 2011

Somo la 4: Kufurahi Mbele za Bwana: Patakatifu na Ibada

Somo Limetafsiriwa na Mgune Masatu


(Kutoka 25, Waebrania 10)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Nilipokuwa shule, nilitumia muda wa majira ya kiangazi kufanya kazi kwenye kampuni ndogo ya ujenzi. Haikuwa kazi nzuri. Kazi ilikuya ya hatari kwa sababu wamiliki wa kampuni hawakuonekana kuwa na uhakika wa baadhi ya kanuni za msingi, mfano kiwango cha juu cha umakini. Mmojawapo wa wamiliki wa kampuni alikata kipande cha ubao aliokuwa ameukalia na alianguka urefu wa futi nane kwenye sehemu ya kutembelea iliyojengwa kwa saruji. Wamiliki wa kampuni hawakujali kabisa masuala yenye kuleta hatari kwa waajiriwa wao kwa vile hawakuonekana kubaini masuala yaliyohusisha usalama wao wenyewe. Tatizo jingine lilihusisha suala la utoaji wa maelekezo. Mmiliki mmojawapo wa kampuni alielezea kwa haraka kile alichonitaka nikijenge, na nilipokuwa sijaelewa nilichotakiwa kufanya, alichukua kalamu ya risasi (penseli) yake na kuchora chini ardhini picha/ramani ya nilichotakiwa kukifanya. Kisha alisema kuwa tayari amekwishaniambia, na hata kunichorea picha (ramani), na kwa hiyo nilikuwa na maelekezo ya kutosha. Mungu wetu ametuchorea picha/taswira (ramani) kuhusu mpango wake wa wokovu. Tofauti na picha zilizochorwa na bosi wangu wa zamani, picha/taswira (ramani) ya Mungu ina utondoti (maelekezo) wa kutosha. Hebu tuzame kwenye Biblia yetu ili tuone picha/taswira ambayo Mungu aliwachorea watu wake kuhusu wokovu!

I. Picha (Taswira) ya Mbinguni – Mungu Pamoja Nasi

A. Soma Kutoka 25:8-9 na Waebrania 8:5. Tunaona kwamba Mungu alimwambia Musa kupafanya patakatifu kwa mujibu wa “mfano” ambao Mungu alimwonyesha. Baini kuwa Waebrania inakielezea kama “kivuli cha mambo ya mbinguni.” Je, hiyo inatuelezea nini kuhusu tafsiri ya tabenakulo la duniani? (Unaweza kulinganishaje kivuli chako na wewe mwenyewe? Ni nakala halisi, lakini inatupatia tu wazo la jumla la kitu halisi.)

1. Je, Mungu alisema kuwa sababu Yake ya kumtaka Musa ajenge patakatifu ni ipi? (Mungu alitaka “kukaa pamoja” na watu Wake.)

B. Soma Ufunuo 21:2-4. Je, mpango wa mwisho wa Mungu kwa wafuasi wake ni upi? (Kwamba ataishi pamoja nao! Mbingu itashushwa duniani na Mungu atakaa na wanadamu. Baini kuwa haya ni matamanio ya muda mrefu ya Mungu.)

1. Kama watu fulani wakisema kuwa wanataka kuishi nawe (na pia wanaweza kulipa kodi ya pango la nyumba) je, hiyo inasema nini kuhusu mtazamo wao dhidi yako? (Mungu anakupenda!)

II. Picha (Taswira) ya Mbinguni – Wabia wa Wanadamu

A. Soma Kutoka 25:1-7. Je, mahala pa Mungu kukaa hapa duniani palipaswa kujengwaje? (Kutokana na sadaka kutoka kwa watu wa Mungu.)

B. Soma Kutoka 35:20-21. Je, watu walishurutishwa kumpatia Mungu nyenzo kwa ajili ya ujenzi wa patakatifu? (Hapana. “kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda” alileta sadaka.)

1. Kama wewe ungekuwa Mungu, na ikawa upendeleo wa ajabu na heshima kwa ajili ya kundi lolote lile la wanadamu ambalo ungeamua kuliheshimu kwa uwepo wako, je, ungekuwa na mtazamo huu huu dhidi ya utegemezaji kifedha nyumba yako?


2. Au, kama wewe ungekuwa Mungu, je, ungedhani kuwa isingestahili kushindana na wanadamu – na ungetamka tu halafu kasri kubwa linalotembea likatokea na kuwepo?

3. Je, hii inatufundisha nini kuhusua mtazamo wa Mungu dhidi ya wanadamu? (Inaonyesha kuwa Mungu anataka kushirikiana nasi katika kutimiza mapenzi Yake, lakini Mungu hatushurutishi – hata kama ana madai halali kwa ajili ya msaada wetu.)

C. Soma Kutoka 35:22. Je, unafikiria nini kuhusu chanzo cha dhahabu kwa ajili ya nyumba ya Mungu?

1. Unakumbuka kwamba majuma mawili yaliyopita tulijifunza kuhusu ndama wa dhahabu aliyetengenezwa na Haruni? Soma Kutoka 32:1-4. Nini kilichotumika kutengeneza ndama wa dhahabu? (Kitu kile kile – pete za dhahabu.)

2. Fikiria hata nyuma zaidi kuhusu chanzo cha hii dhahabu. Kumbuka kwamba hawa watu walikuwa watumwa. Vitu vyao bila shaka vilitoka kwa Wamisri (angalia Kutoka 12:35-36). Je, hii inatuambia nini kuhusu malengo ya Mungu kwa ajili ya mali zetu? (Kwanza, Mungu anamiliki kila kitu. Waebrania walikuwa tu na hii dhahabu kwa sababu Mungu aliingilia kati kwa niaba yao. Kwa haki kabisa Mungu angeweza kuidai yote, lakini hakufanya hivyo. Aliwaacha watu waamue. Pili, dhahabu haikuwa “safi” au “chafu,” bali suala ni kuwa watu wa Mungu wataitumiaje. Je, tutaitumia kutengeneza sanamu, au tutaitumia kumpatia Mungu utukufu?)

3. Je, hizi sadaka zinapendekeza nini kuhusu kuitegemeza kazi ya Mungu hivi leo? (Mungu anatutaka tulete talanta zetu za kilimwengu/kidunia na rasilimali zetu za kawaida na kuzitumia kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Aina zote za sadaka na talanta zinaweza kutumika kuitegemeza injili.)

D. Soma tena Kutoka 25:9. Je, kwa usahihi kabisa Mungu alimtaka Musa aweje? (Mungu anasema ifanye “sawasawa” na haya yote nikuonyeshayo.)

1. Je, unadhani kuwa Mungu anajali sana kuhusu sehemu yetu kwenye ubia wetu nae? (Mungu hatushurutishi. Mungu anatumia talanta zetu za kawaida. Lakini, Mungu ana viwango vya juu kwa ajili yetu. Kama tukichagua kushiriki kwenye kazi ya Mungu, Anatutarajia tutii.)

III. Picha (Taswira) ya Mungu – Mtazamo wa Patakatifu

A. Soma Waebrania 10:1. Baini tena rejea ya “kivuli.” Kama vile tulivyojifunza kwamba patakatifu pa duniani palikuwa ni kivuli cha patakatifu pa mbinguni, vivyo hivyo sheria ni kivuli “cha mambo mazuri yajayo.” Je, unadhani kitu halisia ni kipi – sheria nyingi zaidi?

1. Fungu hili linapendekeza kuwa lengo la sheria ni lipi? (Kutufanya kuwa wakamilifu. Kwa hili lengo, hiki ni kivuli tu.)

B. Soma Waebrania 10:2-7. Je, uhalisia wa sheria ni upi? Kipi kilicho halisi? (Kafara ya Yesu kwa ajili yetu. Lengo la sheria lilikuwa ni kutufanya tuwe wakamilifu, lakini kwa hilo ilikuwa ni kivuli tu. Yesu alikuwa halisi.)


C. Soma Waebrania 10:8-10. Kama Mungu hakupendezwa na dhabihu, kwa nini Agano la Kale lilizihitaji? (Angalia tena Waebrania 10:3. Tunaambiwa kuwa dhabihu zilikuwa ni kwa ajili yetu – kutukumbusha dhambi zetu.)

D. Unaweza kupendekezaje kuwa tunaweza kukumbushwa hivi leo kuhusu dhambi zetu? (Yesu alikufa badala yetu. Tunapaswa kukumbushwa kuhusiana na hili kupitia kwenye huduma ya Meza ya Bwana. Angalia 1 Wakorintho 11:23-26.)

1. Je, kuna njia nyingine unayoweza kukumbushwa mara kwa mara zaidi?

a. Je, kuna njia ambayo sheria inaweza kuwa sehemu ya huu ukumbusho? (Soma Mathayo 22:36-40. Yesu anatuambia kumpenda jirani yako “kama nafsi yako.” Hii inahusisha kujikana nafsi. Waebrania 10 inaelezea zaidi kuhusu kafara (kujikana nafsi). Wazo linalonijia mawazoni mwangu ni kwamba tunapojitoa kwa ajili ya watu wengine, tunakumbushwa kuhusu kafara ambayo Yesu aliitoa kwa ajili yetu. Kwa njia hii sheria ni “kivuli” cha uhalisia wa upendo wa hali ya juu wa Yesu kwetu.)

b. Soma Warumi 12:1. Je, Paulo anatufundisha nini kuhusu aina hii ya mtazamo ya dhabihu/kafara? (Ni aina ya ibada – ibada ya kweli na kamilifu/sahihi!)

2. Nipo likizo niandikapo somo hili. Nimepata kanisa mahalia ninaposalia kila Sabato ninapokuwa likizo. Makanisa haya yamekuwa madogo sana – na katika namna fulani hivi hii inakatisha tamaa sana. Kwa nini watu wachache sana wanahudhuria kanisani? Nini kinachoweza kukusababisha wewe binafsi kuliacha kanisa? (Je, tunahudhuria kanisani ili kwamba tuweze kutoa dhabihu? Au, tunahudhuria kanisani ili kwamba tuweze kulishwa kiroho na watu wengine?

a. Kama tukiamua kuwa sehemu ya kundi lililowalisha watu wengine kiroho, je, hii itatulisha?

E. Tulianza kwa kusema “Mungu amechora picha (taswira) ya aina gani kwa ajili yetu kwa patakatifu pake hapa duniani? Jibu lako kwa hilo swali ni lipi? (Mungu anataka kukaa pamoja nasi. Mungu hatushurutishi. Hata hivyo, kukaa pamoja na Mungu ni kujitoa kwa dhati kabisa. Mfumo mzima wa sheria na patakatifu unawapa watu wengine taswira ya kafara/dhabihu. Ibada ya kweli ni ukumbusho wa siku zote wa kile ambacho Mungu alikitoa kwa ajili ya dhambi zetu.)

F. Rafiki, umeyachunguza maisha yako kutathmini kama una roho ya kujikana nafsi (kujitoa), au roho ya kujipendezesha/kujifurahisha? Je, utamwomba Roho Mtakatifu hivi leo ili abadili moyo wako ili kwamba uakisi vizuri zaidi sheria na upendo wa Yesu dhidi yako?

IV. Juma Lijalo: U Heri, Ee Israeli.

0 comments:

Post a Comment