Somo Limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Mambo ya Walawi 9-10, Warumi 8, 1 Samweli 15)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Juma lililopita tuliangalia patakatifu palipojengwa wakati wa safari ya wana wa Mungu kutoka Misri. Kutokea kwenye hapo patakatifu, na patakatifu pa mbinguni, tulijifunza masomo kadhaa kuhusu matamanio ya Mungu ya kuwa pamoja nasi na kutuokoa kutoka kwenye mauti ya milele. Juma hili tunageuzia usikivu wetu kwenye mwanzo wa matendo na taratibu zinazounganishwa na patakatifu kuona kile tunachoweza kujifunza zaidi kuhusu Mpango wa Mungu kwa ajili yetu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia!
I. Moto wa Kirafiki
A. Soma Mambo ya Walawi 9:1-4. Je, ni nani aliyetakiwa kutoa sadaka? (Kila mtu. Viongozi na watu wa kawaida waliambiwa kuleta sadaka.)
1. Baini kwamba Haruni alitakiwa kuwa wa kwanza kuleta sadaka. Kwa nini? (Haruni alikuwa Kuhani Mkuu. Lakini, kabla Haruni hajawahudumia watu waliosalia, ilimpasa kufanya mahusiano sahihi ya nafsi yake na Mungu.)
2. Je, ni aina gani za sadaka zililetwa? ( Sadaka za dhambi, za kuteketezwa, mahusiano (au amani) na nafaka.)
a. Fikiria kuhusu hizi aina mbalimbali za sadaka. Je, nini lilikuwa lengo la hizi sadaka? (Sadaka mojawapo ilikuwa ni kwa ajili ya kushugulikia tatizo la dhambi. Nyingine ilikuwa ni kuonyesha kuwa kitu fulani kiliachwa kwa hiari. Ya tatu, kwa mujibu wa maoni (commentary) ilikuwa ni “sherehe takatifu.” Hii ilikuwa ni sadaka ya ushirika. Sadaka ya nafaka ilikuwa (katika miktadha mingine) ni unga ambao ninadhani uliteketea kwa urahisi na kusababisha (Mambo ya Walawi 2:2) “harufu ya kupendeza kwa Bwana.”)
3. Hatushughuliki na mfumo wa kafara tena, lakini ni kanuni zipi za ibada tunazoziona katika hili? (Kujihusisha kwetu kwa kwanza kabisa ni kuangalia tatizo letu la dhambi kwa kutubu na kuiacha dhambi. Kujihusisha kwetu kunakofuatia ni kutambua na kuachana na ubinafsi wetu. Kisha, tuna mwelekeo wa ushirika wa ibada. Mwisho, tuna furaha ya ajabu ya ushirika sahihi na Mungu.)
B. Soma Mambo ya Walawi 9:5-6. Je, watu walitakiwa kufanya haya mambo ili waweze kuuona utukufu wa Mungu? (Ndiyo. Kumbuka kwamba juma lililopita tulijifunza kwamba Mungu anataka kukaa pamoja na watu wake. Mungu anataka kuwa nasi tunapokuwa tunamwabudu. Lakini, ibada haipaswi kuwa baridi (bila kuonyesha hisia). Mungu ana matakwa/mahitaji aliyoyaweka kwa watu Wake yakiwa ni masharti ya kuufanya utukufu Wake uwatokee.)
C. Mambo ya Walawi 9:7-21 inaelezea jinsi haya maelekezo yalivyotekelezwa. Hebu tusome Mambo ya Walawi 99:22-24. Je, ni kwa namna gani Mungu anaonyesha ukubali wake wa hizi sadaka? (Utukufu wake unawatokea watu na moto Wake unaziteketeza sadaka.)
1. Je, watu waliitikiaje kutokana na hili tukio? (Walipiga kelele za furaha na kuinama kifudifudi.)
D. Baadhi ya watu wanadai kuwa tunapokuwa kanisani tunapaswa kuwa watulivu sana kwa sababu sisi ni wadhambi na tupo mbele za Mungu Mtakatifu. Je, tunapaswa kuielewaje furaha, kelele na kuinama kifudifudi kwa hawa watu? (Sadaka zao zilikuwa zimekubalika. Dhambi zao zilikuwa zimesamehewa. Walikuwa mbele ya uwepo wa Mungu wao. Hiyo iliwapatia furaha kubwa waliyoielezea kwa kupiga kelele. Bila shaka waliinama kifudifudi kwa sababu walikuwa ni wanadamu mbele za utukufu wa Mungu.)
1. Je, unaweza kukumbuka wakati ambapo ulijisikia “kupiga kelele kwa furaha” dhidi ya msamaha wa Mungu wa dhambi zako na ukubali Wake kwako?
a. Kama huwezi kukumbuka kipindi kama hicho, kwa nini hukumbuki?
E. Soma Warumi 8:1-4. Je, Yesu anaitwaje? (“Kafara ya dhambi.”)
1. Kwa nini ilikuwa muhimu kwa Yesu kutolewa kafara? (Warumi 8:3 inatuambia kuwa sheria yenyewe haiwezi kutuokoa kwa sababu “ilidhoofishwa na asili ya dhambi.”)
a. Je, ni asili ya dhambi ya nani inayoelezewa na Biblia? (Ya kwangu! Ya kwako!)
F. Soma Warumi 8:12-17. Baada ya kumpokea Yesu kama kafara wetu wa dhambi, je, nini kinachofuatia? (Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu “tunayazika matendo yetu mabaya ya mwili.” “Tunashiriki katika mateso ya [Yesu].”)
1. Tulijifunza kuwa nini ilikuwa sadaka ya pili iliyotolewa katika Mambo ya Walawi 9? (Sadaka ya kuteketezwa. Iliwakilisha kuachana na kitu fulani. Ilikuwa ni sadaka ya kutokuwa wabinafsi. Kuacha vipaumbele vyetu vya kidhambi. Kukubali kwamba tutahitajika kushiriki mateso ya Yesu.)
G. Soma Warumi 8:18-19 na Warumi 8:26-27. Je, nini ilikuwa sadaka ya tatu katika Mambo ya Walawi 9? (Ushirika au sadaka ya amani.)
1. Je, hii inaakisiwaje hapa? (Mungu anamtuma Roho Wake ili aishi pamoja nasi, atuombee.)
2. Kumbuka jinsi kilele cha mchakato wa Mambo ya Walawi na zile taratibu ziliishia kwenye utukufu wa Bwana kuwatokea watu. Je, kuna ulinganifu gani na Warumi 8:18? (Milinganisho miwili: Utukufu wa Mungu unafunuliwa kwetu; na uumbaji unaosubiri Ujio wa Mara ya Pili wa Yesu.)
H. Soma Matendo 2:1-3. Je, utukufu wa Mungu ulijidhihirishaje? (Kupitia katika moto!)
I. Rejea nyuma kidogo na utafakari kile tulichojifunza. Kwa nini Mungu alianza na mfumo wa patakatifu? Kwa nini asimtume Yesu moja kwa moja, na kuacha kupitia mchakato na taratibu za Mambo ya Walawi? (Kumbuka juma lililopita nilikusimulia kisa kuhusu mwajiri wangu aliyenichorea picha/taswira? Mfumo wa patakatifu ni taswira kubwa sana ya Mungu ya mpango wa wokovu. Kwa bahati mbaya, watu wengi wa Mungu walimkataa Yesu hata pamoja na kupewa hiyo picha/taswira. Na kwa kuongezea, patakatifu ni zaidi ya taswira/picha. Waebrania 8:1-2 inatufundisha kuwa inaakisi uhalisia wa mbingu.)
II. Moto Usiokuwa wa Kirafiki
A. Soma Mambo ya Walawi 10:1. Inaonekana kwamba hili tukio linafuatia wakati wa furaha kuu ambao tumejadili hivi punde. Je, unadhani hawa vijana walifanya nini ambacho kilikiuka amri ya Mungu? (Soma Kutoka 30:7-9 na Mambo ya Walawi 16:12. Asili ya “moto ambao haukuruhusiwa.” Haiko wazi, lakini inaonekana kwamba hawakufuata maelekezo kwenye moto walioutumia.)
B. Soma Mambo ya Walawi 10:2-3. Moto unatoka kwa Mungu tena, lakini mara hii unawala makuhani badala ya kafara/sadaka. Kwa nini? (Hawakumtii na kumheshimu Mungu.)
C. Soma Mambo ya Walawi 10:4-6. Hapo kabla tulisoma kwamba Haruni “alinyamaza kimya” na sasa Musa anamwambia Haruni asiomboleze vifo vya wanawe. Kwa nini? (Kama Haruni alifikiri wanawe hawakufanya jambo lolote baya, angelalamika/angepinga. Mungu hakutaka huzuni ya Haruni dhidi ya vifo vya wanawe itafsiriwe na watu kama uasi dhidi ya adhabu ya Mungu.)
D. Soma 1 Samweli15:22–23. Samweli anamweleza Mfalme Sauli hii habari mbaya kwamba atapoteza ufalme wake kwa sababu hakumheshimu Mungu. Je, huu mfano unaendana na msalaba na Warumi 8? Je, utii wetu ni wa muhimu zaidi kuliko kafara ya Yesu? (Jibu la kwanza linaonekana kuwa “hapana.” Warumi 8:3 inanifundisha kuwa asili yangu ya dhambi inanifanya nisiweze kuishika sheria. Lakini, baini katika 1 Samweli 15:23 sababu za kukataliwa kwa Sauli: uasi na ukaidi. Warumi 8:12-14 inatuambia kuwa kama tukiishi kwa mujibu wa hii mitazamo tutakufa.)
E. Wana wa Haruni walikuwa kwenye mchakato wa sadaka, lakini walikufa. Linganisha visa vya moto wetu wa kirafiki na ule usiokuwa wa kirafiki. Je, ni masomo gani tunayopaswa kuyapata kutokana na hivi visa? (Tuna chaguzi mbili. Moto unaweza kuteketeza dhambi zetu au unaweza kututeketeza. Huu ni uchaguzi mzito wenye matokeo mazito. Kufanya uchaguzi sahihi huleta furaha. Kufanya uchaguzi mbaya huleta huzuni na mauti ya milele.)
F. Soma Mambo ya Walawi 10:8-9. Je, hii inapendekeza nini kuhusu chanzo cha dhambi ya wana wa Haruni? (Inapendekeza kuwa walikuwa wamekunywa divai/kileo. Katika sherehe za moto wa kirafiki, walianza kunywa – kulikowafanya wasiwe waangalifu na wasichukue tahadhari, wasiwe makini zaidi kuliko ambavyo walipaswa kuwa.)
1. Je, ni somo gani tunalopaswa kujifunza kutokana na hili? (Mungu anaangalia furaha katika ibada, lakini pia anatarajia uchukuliaji makini wa maneno Yake.)
G. Soma Mambo ya Walawi 10:10-11. Je, lengo letu ni lipi katika kutofautisha kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida? (Lengo letu lina cha kujihusisha na kumheshimu Mungu. Malalamiko ya Mungu (Mambo ya Walawi 10:3) yalikuwa ni kwamba hakuheshimiwa. Lengo la ibada yetu linapaswa kuwa ni kumheshimu Mungu.)
1. Je, somo hili linahusika maishani nje ya kanisa? Je, kila mara tupo kwenye utume wa kutofautisha kati ya vitu vilivyo najisi na visafi? (Soma Warumi 8:5. Warumi inatufundisha kuwa lengo la maisha yetu ni kuziweka akili zetu “kwenye yale mambo ambayo Roho anayatamania.” Huu ndio “usafi” wa Mambo ya Walawi 10.)
H. Je, umewahi kutathmini huduma yako ya ibada kuona kama inamheshimu Mungu? Je, huduma yako ya ibada inachukuliwa kwa umakini mkubwa, au inamezwa na fikra zako ndogo au mpango mdogo?
1. Vipi kuhusu maisha yako? Je, yanamheshimu Mungu?
I. Rafiki, tumeona kuwa Mungu anawakilishwa na moto. Mungu yumo kwenye moto unaoashiria uwepo Wake na huleta furaha. Lakini, Mungu pia yumo kwenye moto unaowateketeza wadhambi. Tunamshukuru Mungu kwamba tunaokolewa kwa neema. Lakini, wokovu huo unahitaji uamuzi – uamuzi wa kuishi kwa mujibu wa (moto) wa uwezo wa Roho Mtakatifu na sio kwa asili yetu ya dhambi. Je, utachagua moto wa kirafiki hivi leo?
III. Juma Lijalo: Ibada, Nyimbo na Sifa.
Friday, July 22, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment