Somo Limetafsiriwa na Mgune Masatu
(1 Wafalme 11 & 19, Luka 16, 1 Wakorintho 9, Warumi 14)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: David Wagner ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Hillsdale alifanya utafiti kuhusu historia ya matumizi ya kinanda kilichotengenezwa kwa bomba kwenye ibada kanisani. Wagner anataarifu kwamba Thomas Brattle, mshiriki wa Kanisa la Kiprotestanti la New England, alifariki mwaka 1713. Aliliachia kanisa kinanda chake cha bomba, lakini kanisa lilikataa zawadi hiyo “likiamini haikuwa sahihi kutumia vyombo vya muziki kwenye ibada.” Je, maamuzi ya kanisa la Kiprotestanti yalikuwa ni kukataa kuendana na ulimwengu, azma ya kutokubadili/kutokuingilia/kutokuafiki ibada yake kwa Mungu? Kwa hakika, mwaka 1713 kulikuwa na mtafaruku juu ya aina gani ya muziki inayojumuisha ibada sahihi! Miaka mia tatu baadaye, kitu hicho hicho ni kweli. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuweze kubaini kile inachomaanisha “mwafaka” katika ibada!
I. Mifano ya Mwafaka wa Kidhambi
A. Soma 1 Wafalme 11:4-6. Nini kilitokea kwa Sulemani uzeeni mwake?
1. Nilidhani unapaswa kuwa mwenye busara zaidi unapokuwa mzee! Nini kilichomfanya Sulemani ateleze? (Soma 1 Wafalme 11:1-2. Mungu aliwaambia watu Wake wasiwaoe wanawake waliyoifuata miungu mingine. Sulemani hakutii hilo na lilihafifisha imani yake kwa Mungu wa kweli.)
B. Soma 1 Wafalme 11:7-8. Je, nini kilicho kiini cha ibada ya uongo? (Kujenga madhabahu kwa ajili ya miungu ya uongo, na kuiabudu.)
C. Soma 1 Wafalme 18:19-20. Je, nini ulikuwa mgogoro wa ibada uliowafanya Eliya na Mfalme Ahabu wawe na ugomvi? (Unaweza kuhitajika kusoma muktadha mpana, bali ugomvi ulikuwa ni kama Baali, Ashera au Yehova ndiye alikuwa Mungu wa kweli.)
D. Soma 1 Wafalme 19:14-18. Haya ni mazungumzo baina ya Mungu na Eliya. Je, hitimisho lisilo sahihi la Eliya lilikuwa ni lipi? (Alidhani kwamba, yeye peke yake, ndiye alikuwa mwaminifu kwa Mungu. Badala yake ilibainika kuwa angalao watu 7,000 walisalia kuwa waaminifu kwa Mungu.)
1. Je, jaribu la Mungu la kuwagawa wale waliokuwa bado wanamwabudu dhidi ya wale waliolegeza masharti kidhambi lilikuwa ni lipi? (Kama “walimsujudia” ama “walimbusu” Baali.)
a. Je, inamaanisha nini “kumbusu” Baali? (Kusujudu kulikuwa ni tendo halali la kuabudu. Kumbusu Baali kuliashiria mapenzi kwake.)
II. Mifano ya Mwafaka wa Kimungu
A. Soma Kumbukumbu la Torati 4:1-4. Je, ni makosa gani mawili ambayo wafuasi wa Mungu wanaweza kuyafanya katika juhudi zao za kuepuka kumwabudu Baali? (Wanaweza kuwaambia watu kuwa matendo yasiyo ya kidhambi ni ya kidhambi, na wanaweza kuwaambia watu kuwa matendo ya kidhambi sio ya kidhambi.)
1. Je, tendo moja ni baya zaidi kuliko jingine? (Kwa hakika, yote mawili ni ukiukwaji wa mapenzi ya Mungu.)
2. Nilipokuwa chuoni, nilikuwa ninafuga ndevu (na bado ninazifuga). Sabato moja, nilipokuwa nimetembelea kanisa la rafiki wangu wa kike, niliombwa kuliongoza kanisa na kuhudumu kwa kutoa ombi. Nilikubali, kitu kilichomaanisha kuwa nilikaa mbele katika kipindi chote cha huduma kuu. Ilitokea kuwa hubiri lilihusu dhambi ya ufugaji wa ndevu. Mhubiri alimalizia hubiri lake kwa kusema kitu kama “Fidel Castro anafuga ndevu, na sote tunajua kile anachokisimamia.” Nilifikiria, “Vipi kuhusu ufafanuzi wa Yesu kuwa na ndevu?” Je, mhubiri alikuwa akitenda dhambi alipokuwa akihubiri hubiri lake?
B. Soma Luka 16:1-7. Je, meneja (wakili) ni mtu mwema au mtu mbaya? Je, meneja amelegeza kanuni zake ili aweze kuishi maisha bora? (Kwa wazi kabisa sio mwaminifu, akijipendelea mwenyewe dhidi ya bwana wake.)
C. Soma Luka 16:8-9. Je, bwana ni nani? (Yesu ndiye anayeelezea hiki kisa. Anajiweka yeye mwenyewe kwenye nafasi ya bwana.)
1. Je, Yesu anaona kitu gani kuwa ni chema kwenye hiki kisa cha kutokuwa na uaminifu na usaliti? (Ya kwamba meneja ni mwerevu. Yesu anasema kuwa wafuasi Wake wanahitajika kuwa werevu zaidi.)
D. Soma kwa makini Luka 16:9. Je, unadhani “mali ya udhalimu” ni ipi? (Lazima viwe vitu ambavyo dunia inavichukulia kuwa ni vya thamani: fedha, uzuri, ushawishi.)
1. Je, inamaanisha nini “kujifanyia marafiki?” (Kwa vile “makao ya milele” yanaelezea mbingu, Yesu anatuambia tutumie zana za kidunia kuwaleta watu kwenye injili.)
E. Soma Luka 16:10-12. Je, ni kwa namna gani hili ni hitimisho sahihi kwenye kisa tulichokisoma hivi punde? (Kwa hakika mwanzoni hii haileti maana hata kidogo. Kisa kinaleta maana iliyo kinyume chake! Lakini, kama tukiangalia kwa undani zaidi, tunaona kwamba Yesu anatufundisha kwenye hiki kisa kuwa tunahitajika kuwa werevu kama dunia katika kuipeleka injili kwa watu wengine – na tunahitajika kutumia mali ya kidunia kutenda hilo.)
1. Je, unadhani kuwa fasili/ufafanuzi wa Yesu kuhusu mwafaka ni upi? (Tunalegeza msimamo kuhusu injili pale ambapo hatutumii rasilimali zetu zote zilizopo kuuendeleza ufalme wa mbingu. Sisi ni watumishi wasioaminika kama tukimwangusha Mungu katika hili!)
F. Soma 1 Wakorintho 9:19-22. Mtume Paulo anaelezea njia yake ya kuwaleta watu wengine kwa Yesu. Je, yeye ni mtu wa mwafaka?
1. Je, Paulo ni mnafiki, anaamini jambo moja na kutenda jambo jingine?
2. Je, unadhani Paulo anamaanisha nini anapoandika “Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi?”
3. Soma Wagalatia 2:11-13. Hebu subiri kidogo! Paulo anamshutumu Petro kwa kuwa “kama Myahudi, ili awapate Wayahudi,” sawa? Je, hilo silo aliloliandika Paulo kwamba tunapaswa kulifanya?
a. Je, kuna tofauti gani unayoiona hapa? Je, unaelezeaje karipio la Paulo kwa Petro? (Petro hajaribu kuwapata Wakristo wapya, “watu kutoka kwa Yakobo” tayari walikuwa Wakristo. Tatizo linaonekana kuwa mwafaka wa Petro unawaumiza Wakrito wapya kutoka kwa mataifa.)
b. Je, ni kanuni ipi ya kuiendeleza injili unaweza kuichukua kutoka kwenye hoja ya Paulo ya mwafaka na mwafaka wa Petro? (Paulo anaonekana kusema kwamba katika hali tofauti anajirekebisha ili afanane na utamaduni wa kuwaleta watu wengine kwenye injili. Petro anawaudhi tu Wakristo waliopo.)
III. Mwafaka Usiokuwa na Mwafaka
A. Soma Warumi 14:1-4. Mimi ni mla mboga mboga, kwa hiyo imani yangu sharti iwe dhaifu! Soma tena 1 Wakorintho 9:20. Unatabasamu ninapoandika kuwa mimi ni mla mboga mboga. Je, hisia zako zingekuwaje kama ningeandika “nipo chini ya sheria?” Hisia mojawapo inaonekana kuwa ni mjadala usiokuwa na madhara (isipokuwa kama nina afya njema), wakati ambapo hisia nyingine inaonekana kuwa ni kosa kubwa la kiteolojia. Je, ni kwa kiasi gani tunatakiwa kuchukulia utayari wetu hadi kwenye mwafaka?
B. Soma Warumi 14:13-18. Je, utasema kile ambacho Paulo anakitetea hapa kuwa ni “mwafaka?”
1. Je, kiwango cha Paulo cha mwafaka usiokuwa na mwafaka ni kipi? (Usifanye kitu chochote kitakachomzuia mtu mwingine kuipata imani.)
C. Hebu tuone kama tunaweza kufikia baadhi ya hitimisho kuhusu ibada. Tumejifunza kwamba Yesu anatuita watumwa wasio waaminifu kama hatutumii zana za kidunia kuiendeleza injili. Tumejifunza kwamba Paulo anatetea kuhusu kuendana/kukubaliana na mawazo ya tamaduni tofauti (na kiteolojia?) ya kuiendeleza injili. Tumejifunza kwamba Mungu anatuambia kuwa ni dhambi kuzuia mambo ambayo hajayazuia (au kuruhusu mambo anayoyazuia). Pia tumejifunza kwamba Sulemani alipojiingiza kwenye miungu ya kitamaduni ya wakeze wa kigeni, alitenda dhambi. Hebu niambie, ni kanuni gani za ibada unazoziamini Mungu anazihitaji?
1. Hebu tukurejeshe nyuma kwa miaka 300 na kisha utumie kanuni yako. Upo kwenye Baraza la Kanisa la Kiprotestanti ambalo ni punde tu limebaini kwamba Thomas Brattle amekupatia kinanda chake cha thamani. Je, utapigaje kura yako?
a. Vipi kama nikiongezea ukweli kwamba watu wengi ambao hawakuwa na moyo wa kujiunga na kanisa la Kiprotestanti wangejiunga nalo kama wangeweza kusikia muziki wenye kuburudisha kutoka kwenye kinanda?
D. Rafiki, maoni yangu ni kwamba kanuni isiyoyumba ya Mungu kuhusu ibada inahusu kutoabudu miungu ya uongo. Kanuni yake ya pili ni kwetu sisi kutumia akili zetu za kawaida na busara kuendana na utamaduni wa kuiendeleza injili. Kanuni yake ya tatu ni kwamba epuka kuwatukana/kuwafedhehesha wale ambao imani yao ni dhaifu – wale ambao wanachanganya vipaumbele vyao vya kitamaduni na sheria ya Mungu. Ili kuweza kuzishika hizi kanuni zote kwa uzuri zaidi, ushauri wangu ni kuabudu katika kanisa linalokua (lile linaloiendeleza injili) ambalo lina mtindo wa ibada unayoitaka.
IV. Juma Lijalo: “Usiamini Katika Maneno ya Udanganyifu”: Manabii na Ibada
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment