Friday, August 19, 2011

Somo la 9: “Usiamini Katika Maneno ya Uongo/Udanganyifu”: Manabii na Ibada

Somo Limetafsiriwa na Mgune Masatu


(Yeremia 7, Isaya 58, Mika 6)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Miaka mingi iliyopita, nilikuwa eneo la Michigan kukutana na kundi la walimu waliokuwa na pingamizi la kidini kuhusu kukitegemeza chama cha walimu. Walimu wengi walifurahi sana kwa mimi kuwasaidia kwa sababu waliridhika kwamba haikuwa ikimpendeza Mungu kusalia kwenye hicho chama kilichopingana na kanuni za Mungu. Mwalimu moja alijali sana kuhusiana na wajibu wake kwa Mungu, lakini pia alijali kuhusiana na bima ya gari lake iliyotolewa na chama cha walimu. Alitaka kujua kama akijiondoa kutoka kwenye chama angeweza kuendelea kuhudumiwa na chama kuhusu bima ya gari lake. Nilipomwambia kuwa, “Hapana,” wasio wanachama hawakuwa na haki ya kuendelea kudhaminiwa bima, alijibu kuwa itakuwa gharama sana kwake kuweka pingamizi la kidini. Tulipokuwa tukiondoka kikaoni, niligundua kuwa alikuwa akiendesha gari jipya aina ya Cadillac. Imani yake inaweza kuthamanishwa na kiasi alichoweka akiba kutokana na bima iliyotolewa na chama cha walimu. Je, vipi kuhusu sisi? Je, imani yetu inaleta utofauti maishani mwetu? Je, inapaswa kuwa hivyo? Au, je, haki kwa imani inatupumzisha kutoka kwenye vitu kama hivyo? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze kuhusu imani inayoleta utofauti!

I. Watu wa Mungu, Kanisa la Mungu

A. Soma Yeremia 7:1-2. Je, Mungu alikuwa akimfikiria nani akilini mwake kama mpelekaji wa ujumbe Wake? (Watu wake. Aliwataka wale waliokuwa wakiingia kwenye ibada kuusikia huu ujumbe.)

B. Soma Yeremia 7:3-4. Mungu anasema “Unatakiwa kufanya mabadiliko maishani mwako (tengenezeni njia zenu na matendo yenu)”. Baadhi ya watu wanajibu wakiwa na neno kuhusu jiografia: “Hili ni hekalu la Bwana.” Je, kiuhalisia kabisa watu hawa wanasema nini? (Wanaabudu katika kanisa lililo sahihi.)

1. Baini kwamba hawa watu wanarudia jibu lao mara tatu. Kwa nini? (Kurudia jambo mara mbili katika Biblia ni njia ya kawaida ya kusema kwamba kitu fulani ni cha muhimu. Huenda walisema mara tatu ili kujiridhisha wao wenyewe.)

2. Fungu linapendekeza kwamba “Hili ni hekalu la Bwana” ni kauli ambayo watu wanaitumia mara kwa mara. Mungu anaiita kauli kuwa “maneno ya uongo.” Je, ni kitu gani kwenye kauli hiyo kinapotosha? (Utambulisho wa kanisa sio unaokuokoa.)

a. Baini kuwa hawa watu sio tu kwamba walikuwa na “kanisa” sahihi, bali pia walikuwa wakiingia kwenye mfumo sahihi wa ibada. Tena muhimu zaidi, walikuwa wakimwabudu Mungu wa kweli. Je, mfumo sahihi wa ibada mbele za Mungu wa kweli unaweza kuwa wa uongo?

C. Soma Yeremia 7:5. Je, Mungu anawataka watu Wake wafanye nini? (Wabadili “njia zao.” Kwa Kiebrania inamaanisha “barabara,” kwa hiyo hii inamaanisha uelekeo wa maisha yao, mtazamo wao. Mungu anataka badiliko la mtazamo.)


1. Hebu tusimame kidogo na kutafakari hili. Hawa watu walikuwa na kanisa sahihi, Mungu wa kweli, na ibada sahihi, lakini Mungu aliwaita kuwa waongo. Je, hii inatufundisha nini kuhusu ibada? (Kwamba haikomi/haiishi pale tunapoondoka kanisani.)

II. Ibada Inayoishi

A. Soma Yeremia 7:6-7. Je, mgeni, yatima na mjane wana kitu gani cha kawaida kwa pamoja? (Wamepungukiwa uwezo katika jamii.)

1. Je, utawakandamiza kwa kutowasaidia? (Kuna mafungu mengine ya Biblia yanayojadili kuhusu kuwasaidia wahitaji, lakini hilo sio fungu mojawapo. Neno la Kiebrania linalohusu “ukandamizaji” linamaanisha “laghai/ghilibu” au “kiuka.” Watu hawa kwa ujasiri kabisa wanawaonea watu wasiojiweza.)

2. Kinyume na kuwadhuru wasiojiweza, ni kitu gani kingine hawa watu wanakifanya? (Wanawaua watu wasiokuwa na hatia.)

3. Je, kwa ujumla unaelezeaje mtazamo wa hawa watu wa Mungu? (Wanatumia vibaya uwezo wao.)

4. Marekani, serikali inawalipa watu masikini na wasio na kazi, na hii inaongeza kodi ya ziada kwa watu wanaofanya kazi kwa bidii na kufanikiwa. Kwenye demokrasia, tunaamua vitu kwa kupiga kura, na tuna wapiga kura muhimu wengi walio masikini kuliko wapiga kura muhimu walio matajiri. Je, watu masikini wanaweza kutumia vibaya uwezo wao, au je, hii tu ni dhambi ya matajiri?

B. Soma Yeremia 7:7-8. Je, Mungu atawabariki wale wanaotumia uwezo wao vibaya? (Hawawezi kumtegemea Mungu, kwa kuwa Mungu anasema kwamba wanajidanganya. Mungu anawaambia kwamba atawanyang’anya miji yao na nchi yao.)

C. Soma Yeremia 7:9-11. Je, tunamwabudu Mungu kwa usahihi kama tunatumia vibaya uwezo wetu? (Hapana! Mungu anasema kuwa hawa watu wanawadhuru watu wengine kwa kutumia njia mbaya kabisa. Kwa kuongezea, wanaitii miungu mingine.)

1. Je, hii inasema nini kuhusu haki kwa imani?(Sidhani kama haki kwa imani inahusika hapa, kwa sababu hawa watu wanaiweka imani yao kwa Baali, ingawaje wanahudhuria kwenye kanisa sahihi. Matendo mabaya yanaelezea tu kwamba hawana mtazamo wa utii kwa Mungu.)

2. Baini kwamba Mungu anasema kuwa anawaona. Je, anatuona?

a. Kama unasema, “ndiyo,” hebu ngoja nikuulize swali wewe binafsi. Je, matendo yako yanabadilika kulingana na kama watu wengine wanakuangalia? Je, utaangalia vipindi vya televisheni hivyo hivyo, kuangalia tovuti hizo hizo, au kusikiliza muziki huo huo kama viongozi wako wa kanisa wakiwa pamoja nawe?

(1) Kama usingefanya hivyo, basi kwa nini ujihusishe na mambo haya wakati ambapo Mungu anakuona?


(2) Je, mwenendo wetu mbele za Mungu (anayesema kuwa anaangalia muda wote) ni suala la ibada? (Ibada ni kumheshimu Mungu na kumwonyesha utii wetu. Kwa muktadha huo, utii ni ibada.)

III. Wafuasi Waaminifu

A. Soma Isaya 58:1. Je, Mungu anafadhaika kuhusiana na dhambi za watu?

1. Je, Mungu anaziitaje dhambi zao? (Uasi.)

a. Hili ni neno linalofurahisha sana. Ninaamini katika haki kwa imani. Ni njia pekee ya kuuelekea uzima wa milele. Lakini, hebu tuchunguze tatizo la dhambi. Je, Mungu anaiangaliaje dhambi, na hiyo inasema nini kuhusu haki kwa imani? (Dhambi ni uasi dhidi ya Mungu. Ni kuukataa ufalme Wake. Imani na matendo haviwezi kutenganishwa kimantiki, kwa sababu matendo yetu yanatokana na mitazamo yetu. Dhambi inatokana na mtazamo wa uasi dhidi ya Mungu.)

B. Soma Isaya 58:2. Je, kwako wewe watu hawa wanaonekana kuwa ni waasi ?

C. Soma Isaya 58:3. Hebu tuangalie sehemu ya kwanza ya hili fungu. Je, hawa watu wanajikana nafsi?

D. Soma Isaya 58:3-4 na Warumi 7:14-15. Je, Isaya anazungumza na kikundi cha watu ambao wanafanana kabisa na mtume Paulo (na, kama ukweli ukielezwa, wanafanana tu kama wewe na mimi)?

1. Je, lengo la kufunga na “kujinyenyekeza kwetu” ambavyo watu wanasema kuwa wanavifanya ni lipi? (Kujikana nafsi.)

2. Kwa nini “uwanyonye … wafanyakazi” au muanze “kupigana kwa ... ngumi?” (Wanajipendelea wenyewe dhidi ya wafanyakazi wao. Wanasisitiza kutekeleza mawazo yao dhidi ya washiriki wa kanisa wenzao. Kwa hakika hiki ni kinyuma cha kujikana nafsi!)

E. Soma Isaya 58:6-7. Je, Mungu anatoa wito gani kwenye (saumu) mfungo wetu? (Kuwa na msimamo/uthabiti! Kujichunguza binafsi. Tunawezaje kusema kuwa tunajikana nafsi, kama tunawanyanyasa watu wengine kwa ajili ya manufaa yetu? Mungu anatuambia tufumbue macho yetu na kuona mambo kama vile Yeye anavyoyaona.)

F. Hebu turukie nyuma hadi mwanzoni kabisa mwa huu mjadala. Soma tena Isaya 58:2. Kutokana na kile kinachoendelea, je, tunawaelezeaje hawa watu? (Je, mtu fulani amewahi kukutaka utoe maoni/mawazo yako, na ikaonekana kuwa hawana haja na maoni yako – isipokuwa kama unakubaliana nao? Hawa watu hawaulizi kwa sababu wapo makini kuhusiana na utayari wao wa kubadilika. Wanatafuta uthibitisho/uidhinishwaji wa kimamlaka wa matendo yao ya ubinafsi!)

1. Je, uko makini kwa kiasi gani kuhusu kutafuta na kufuata maoni ya Mungu?


G. Soma Mika 6:6-8. Sadaka za kuteketezwa, kondoo, mafuta, vyote ni mifano ya kafara ya Yesu inayokuja kwa ajili/niaba yetu. Je, hii inatufundisha nini kuhusu haki kwa imani ya kweli? Ibada ya kweli? (Kutoa kafara (sadaka), kuomba kwa jina la Yesu, bila kujali kuwa ni mara kwa mara kiasi gani tunafanya hivyo, havituokoi. Hizi sio kama kauli ya kimaajabu, au neno la siri (password) la mwisho. Badala yake, ibada ya kweli, haki kwa imani ya kweli inahusisha mtazamo unaoakisiwa kwenye maisha yetu ya kila siku: rehema, haki, kujitahidi kusalia kwenye hatua za Mungu.)

H. Rafiki, je, umeyachunguza maisha yako? Je, ibada yako ni ya juu juu? Je, mtazamo wako wa kila siku unaendana na mtazamo wako unapokuwa kanisani? Je, unamwomba Mungu, lakini hutaki kwa hakika kujua jibu lake? Je, mara zote wewe ni mbinafsi, ukitumia udhaifu wa watu wengine? Mwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, abadilishe moyo wako na mtazamo wako, ili kwamba “utembee kwa unyenyekevu pamoja na Mungu wako.”

IV. Juma Lijalo: Ibada – Kutoka Uhamishoni Hadi Urejeshwaji.

0 comments:

Post a Comment