Somo Limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Yohana 4)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Fikiria wewe kuwa na uwezo wa kumuliza Yesu kwamba ni kitu gani alichodhani kuwa kilikuwa cha muhimu sana kuhusiana na ibada. Je, hicho kitu hakitakuwa maalum? Hata hivyo, imebainika kuwa tunalo jambo hilo kwa uhakika kabisa na limeandikwa kwenye Biblia. Hebu tuzame mara moja kwenye somo letu la Biblia na kujifunza zaidi!
I. Mgeni Mwenye Uhasama/Uadui
A. Soma Yohana 4:1-3. Inaonekana kana kwamba Yesu anapata ushindi kwenye huu mpambano wa ubatizo! Je, kwa nini ajiondoe, tena pale anapokuwa ameshinda? (Huu sio mpambano, ni dhana isiyohitaji kuzingatiwa. Mafarisayo sasa wanabadili mtazamo wao na kumfanya Yesu kuwa “adui” mkuu. Yesu aliamua kwamba ilikuwa vema ajitoe/arudi nyuma.)
B. Soma Yohana 4:4. Njia ya moja kwa moja kuelekea Galilaya ni kupitia Samaria. Wayahudi na Wasamaria hawakuwa wakipendana kwa sababu Wayahudi walidhani Wasamaria walikuwa wadhaifu. Kwa hiyo, Wayahudi mara kwa mara hawakupitia Samaria. Je, unadhani ni kwa nini Biblia inasema Yesu “alipaswa” kupitia Samaria? (Huenda Roho Mtakatifu alimwongoza kupitia Samaria.)
C. Soma Yohana 4:5-8. Ni yapata saa sita za mchana. Kwa nini Yesu akae kisimani badala ya kwenda na wanafunzi kununua chakula? (Kwa mara nyingine tena, hii inapendekeza kuwa Roho Mtakatifu anamwelekeza kuwa mahala hapa.)
D. Soma Yohana 4:9. Je, umewahi kujaribu kuzungumza na watu fulani, na wakataka kubadilisha mazungumzo hayo kuwa kwenye masuala ya kisiasa au ya kibaguzi? Je, hii inakuambia nini kumhusu huyu mwanamke wa Kisamaria? (Anataka kuwa mwenye machukizo.)
1. Hebu tuchukulie kwamba Roho Mtakatifu anamwongoza Yesu kuwa na huu mjadala. Je, utalichukuliaje? “Asante, Roho Mtakatifu, nilihitaji kofi la maneno usoni!”
2. Je, utashawishika kujibu, “Acha mambo yasiyokuwa na mantiki. Mimi nina kiu tu!”
II. Mahusiano ya Kiinjili na Maji ya Uzima
A. Soma Yohana 4:10. Je, unadhani kwamba ni kweli Yesu ana kiu, au anajaribu tu kuanzisha mazungumzo?
1. Je, Yesu anajaribu kuyaelekeza wapi haya mazungumzo? (Kwenye utume wake duniani.)
B. Soma Yohana 4:11-12. Jibu la swali lake kuhusu Yesu na Yakobo ni “Ndiyo.” Je, unadhani mwanamke alimaanisha hili kama swali? (Hapana. Anamshutumu kwa kuwa mtu asiye na akili timamu – akijiondosha kwenye uhalisia.)
C. Soma Yohana 4:13-15. Je, mwanamke amebadili mtazamo wake ghafla dhidi ya Yesu? (Inaonekana kuwa hivyo.)
1. Je, unadhani ni kwa nini hili lilitokea? Je, twawezaje kutoka kwenye uhasama/uadui hadi kwenye werevu? (Uwezo wa Mungu.)
2. Je, unao marafiki na watu wengine unaowafahamu wenye uhasama na Mungu na kwa hiyo ni maadui kwako?
a. Je, ni somo gani tunaloweza kujifunza kuhusu kushiriki injili na watu wenye uhasama?
3. Hebu turejee nyuma na kutafakari kauli za Yesu. Je, ni maji gani anayoyazungumzia Yesu?
a. Soma Yohana 7:37-39. Yesu anatupatia kile alichompatia huyu mwanamke. Je, umekikubali?
b. Je, maisha kama yale yaliyokuwa na “mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake” yataonekanaje?
(1) Yesu anatumia ishara ya maji kwa sababu maalum. Maji yanafanya kitu gani? (Yanaburudisha. Yanafanya mambo yaonekane yenye uhai/upya. Yanafanya mambo yakue.)
(2) Je, maisha yako yapo kama haya? Je, unawatia nguvu wale wanaokuzunguka? Je, unawaburudisha/fariji watu wengine? Je, unawasaidia kukua kiroho?
(3) Fikiria kanisa zima lililojaa watu wanaotoa mito ya maji ya uzima! Je, aina hiyo ya ibada itaonekanaje?
D. Soma Yohana 4:16-18. Juma lililopita tulijifunza kwamba Mungu alisema kuwa atatusikiliza tutakapomtafuta kwa moyo wetu wote, na hatawasikiliza wale waliomkataa hata kama walipiga kelele sikioni mwake. Huyu ni mwanamke asiyekuwa na maadili. Kama Roho Mtakatifu ndiye aliyeongoza hili kutaniko, je, ni kwa nini? (Kuna tofauti kati ya wale wanaogeuza kwa ukakamavu migongo yao kwa Mungu na kuiendeleza ibada ya uongo, na wale wanaojichafua tu katika dhambi.)
1. Je, kwa nini Yesu aliisonda dhambi yake? (Alimwonyesha kwamba aliufahamu ukweli – kitu ambacho huenda mtu mgeni asingeweza kukijua. Hakuwa mtu asiyekuwa na akili timamu. Na kwa kuongezea, Mungu anatupima kwenye maeneo yetu yenye udhaifu wa kiroho.)
E. Soma Yohana 4:19-20. Mwanamke anakiri kuwa Yesu ni mtu maalum, lakini kisha anabadili mada. Kwa nini? (Huyo mwanamke ni kama jinsi sisi tulivyo. Tunamwendea mtu anayeibukia kiroho, na tunataka kuongelea kuhusu masuala makuu/makubwa ya kiteolojia yanayotenganisha kanisa letu na makanisa mengine, hatutaki kuongelea kuhusu dhambi kwenye maisha yetu wenyewe!)
III. Ushauri wa Yesu Juu ya Ibada ya Kweli
A. Soma Yohana 4:21. Yesu anaendelea mbele na jaribu la mwanamke la kutaka kubadili mada kwenye masuala makubwa/makuu ya kiroho. Je, sio jibu sahihi kwamba watu wanapaswa kuwa wanaabudu Yerusalemu? (Soma 1 Timotheo 2:8. Yerusalemu itaharibiwa hivi karibuni. Mfumo wa patakatifu pa mbinguni utatimizwa kwa kafara ya Yesu na ufufuo. Yesu anaelekeza wakati ambapo kila mtu mahali popote anapaswa kuinua mikono yake katika maombi na kumwabudu Mungu!)
B. Soma Yohana 4:22. Yesu anasema wokovu watoka kwa Wayahudi, kwa nini? Je, huku sio kumdhihaki/kumfedhehesha huyu mwanamke? (Wayahudi walikuwa na mfumo wa patakatifu uliokuwa ukijielekeza kwa Yesu. Yesu alikuwa Myahudi katika uanadamu wake.)
C. Soma Yohana 4:23-24. Tunaingia kwenye ushauri wa Yesu usio na kikomo kuhusu ibada! Hebu tuchimbue zaidi kile inachomaanisha kumwabudu Mungu katika “roho na kweli.” Je, kauli ya “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho” inaleta mantiki yoyote kwako?
1. Hebu tuseme hili katika muktadha unaofanana: “Baba yako ni mwanaume, lazima uzungumze nae kama mwanaume.” “Mama yako ni mwanamke, lazima uzungumze nae kama mwanamke.” Je, hiyo inatufundisha nini kuhusu kuwasiliana na wazazi wetu?
2. Hebu tusome Mathayo 28:18-19. Katika hili fungu Yesu anatuambia kuwa Mungu ni zaidi ya Roho, Yeye pia ni Baba na Mwana. Je, Yesu anatuambia nini katika Yohana 4:24 kuhusu kumwabudu Mungu katika “Roho?” (Katika kiwango cha kawaida kabisa, Mungu yu tofauti na miungu ya uongo kwa sababu yeye sio sanamu na hazingirwi na mahala pamoja. Hii kimantiki inaendana na jibu la Yesu kwenye swali kuhusu mahali pa ibada. Unaweza kumwabudu Mungu mahali popote. Katika kiwango cha ndani zaidi, Yesu anatuambia kuwa Roho Mtakatifu ndiye kiini cha ibada.)
D. Soma Yohana 16:7-15. Je, ni sehemu gani ya Mungu Baba, kwa mujibu wa Yesu, itakuwa sehemu ya rejea katika kukabiliana na wanadamu? (Roho Mtakatifu.)
1. Kama Roho Mtakatifu ndiye kiini cha ibada, je, kiwango cha uhusishaji wa Roho Mtakatifu katika ibada yako ni kipi?
2. Nina marafiki wangu wa dhati kanisani kwangu wanaotumia neno “Pentekoste” kama neno hasi (sio chanya). Kama kitu ni cha “Kipentekoste,” basi kwa dhahiri ni kibaya (cha kimakosa), na kwa hiyo kukitia kitu alama kama cha Kipentekoste kinamaliza mjadala. Roho Mtakatifu alikuja kwa uwezo wakati wa Pentekoste (Matendo 2). Je, marafiki wangu, na wale wanaokubaliana nao, wanatakiwa kurekebisha fikra zao kwenye hii mada? (Nadhani hivyo!)
E. Hebu tuangalie sehemu ya pili ya Yohana 4:24. Sehemu ya kwanza ya ibada ya kweli ni Roho. Je, inamaanisha nini kuabudu “katika kweli?”
1. Soma 1 Wakorintho 14:22-25. Je, Biblia inasema nini kuhusu vipaji vya Pentekoste? (Ya kwamba vinatakiwa kutumika kwa busara. Tunaposoma 1 Wakorintho sura za 12-14 tunajifunza kwamba kanisa katika Korintho lilikuwa limejawa na uwezo wa Roho Mtakatifu. Paulo anasema hii inatakiwa kujaribiwa na “kweli.” Kumbuka kwamba katika Yohana 16:13 Roho Mtakatifu anatakiwa kutuongoza katika “kweli.” Paulo hawaambii Wakorintho kuwa wanajihusisha na nguvu za kishetani. Badala yake, anasema matumizi yetu ya Roho yanapaswa kuonyesha mantiki ya kawaida: kweli.)
2. Soma 1 Wakorintho 12:1-3. Je, ni somo gani analotupatia Paulo kuhusu Roho Mtakatifu? (Hakuna ujumbe unaotoka kwa Roho Mtakatifu utapingana na injili. Manabii wa Agano la Kale, maneno ya Yesu, na manabii wa Agano Jipya wote wataendana na Roho Mtakatifu hivi leo kwa sababu wote wana chanzo kimoja.)
3. Soma 1 Wakorintho 14:18-20. Je, hawa “ndugu” wanashawishiwa na mapepo? (Hapana. Hili ni jambo la muhimu sana. Waamini wanaweza kumtumia vibaya Roho Mtakatifu. Wanaweza kuzungumza na kuandika kama watoto. Hatutakiwi kuhitimisha kwamba kwa sababu tu mtu fulani alimtumia vibaya Roho wa Mungu kwamba ilikuwa ni ya kishetani. Huenda inaweza kuwa tu ni upumbavu.)
4. Mara kadhaa marafiki wangu wa Kipentekoste wamekuwa wakisema isipokuwa tu kama Roho Mtakatifu atazungumza nao kwenye suala la Biblia, hawatabadili msimamo wao. Je, hii ni sahihi? (Tumejifunza kwamba Roho Mtakatifu atatuongoza kwenye kweli, lakini Biblia ni Neno la Mungu. Kama Biblia ipo wazi, Roho anazungumza nasi.)
F. Rafiki, je, ibada yako ipo katika “Roho na kweli?” Baadhi ya makanisa yamo kwa undani zaidi katika “kweli” kiasi kwamba yanatii kiu ya Roho. Baadhi ya makanisa yapo kwenye undani zaidi katika “Roho” kiasi kwamba yanatii kiu ya kweli. Je, utaomba ili kwamba wewe na kanisa lako muabudu kikamilifu katika Roho na kweli?
IV. Juma Lijalo: Ibada Katika Kanisa la Mwanzo.
Tuesday, September 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment