Somo Limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Matendo 1, 2, 17, & 18, 1 Wakorintho 13)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2009, Bruce N. Cameron, J.D. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Somo hili pia linaweza kupatikana kutoka http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, watu walioishi na Yesu waliabuduje? Kanisa la awali lilijawa watu waliopata fursa ya kumsikiliza Yesu akifundisha. Je, walipata utambuzi maalum kutoka kwa Bwana wetu? Je, tunaweza kuingiza kile walichokuwa wakikiabudu kwenye ibada yetu? Hebu tuzame kwenye Biblia na kuona kile tunachoweza kujifunza!
I. Maelekezo
A. Soma Matendo 1:1-3. Je, ni mambo gani mawili aliyoyajadili Yesu na wafuasi wake baada ya ufufuo wake? (Kwamba kwa hakika alikuwa amefufuka kutoka kaburini, na Ufalme wa Mungu.)
1. Je, Yesu alikuwa ni mwalimu pekee aliyehusika? (Hapana. Fungu linaelezea kwamba Yesu alichukuliwa juu “alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu.”)
B. Soma Matendo 1:4-6. Baada ya maelekezo yake baada ya ufufuo kuhusu Ufalme wa Mungu, je, wafuasi wa Yesu waliyaelewa vizuri? (Hapana! Bado walidhani kwamba Ufalme wa Mungu ulikuwa uletwe kwa urudishaji wa Ufalme wa Israeli.)
1. Je, unaelezeaje kwamba wanafunzi bado walikuwa wamekosea kuhusiana na hili? (Hii inaonyesha kwamba mara nyingine tunakuwa na ugumu mkubwa wa kuuelewa ukweli – hata pamoja na kuwa na walimu bora kabisa.)
C. Soma Matendo 1:7-9. Kwa nini Yesu hakusema, “Enyi wapumbavu! Kwa nini mmekuwa hamnisikilizi kwa makini”?
1. Je, inawezekana kwamba wanafunzi hawakuwa wamekosea? (Soma Ufunuo 21:1-3. Muda unakuja ambapo Yesu atafanya mambo yote mapya katika nchi, ikijumuisha kuileta Yerusalemu Mpya kutoka mbinguni.)
2. Baini katika Matendo 1:8 kwamba Yesu anawarejea wafuasi wake kuwa mashahidi “katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria.” Je, hii inapaswa kuwaambia nini wafuasi wake kuhusu ufalme? (Ya kwamba Ufalme wa Mungu sio tu Israeli, bali Samaria na hata mwisho wa nchi.)
3. Je, hii inatufundisha nini kuhusu ibada katika kanisa la awali? (Bado walikuwa wanatafuta suluhisho la masuala ya msingi ya injili.)
D. Hebu tuangalie tena Matendo 1:8. Tumejifunza kwamba Roho Mtakatifu tayari alikuwa akifanya kazi pamoja na Yesu katika kuwaelekeza wafuasi wake. Je, Yesu anaahidi nini anaposema “mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu?” (Hii inapendekeza viwango vya nguvu/uwezo vya karama ya Roho Mtakatifu.)
1. Soma tena Matendo 1:5. Je, inamaanisha nini “kubatizwa katika Roho Mtakatifu?”
E. Soma Matendo 1:12-14. Unadhani walikuwa wanasali kwa ajili ya kitu gani? (Urejeshwaji wa Ufalme wa Yerusalumu. Uwezo wa Roho Mtakatifu.)
F. Je, ni masomo gani tunayoyapata hapa kuhusu ibada? (Walikuwa kwenye maombi. Tunahitajika kuomba kwa ajili ya uelewa sahihi wa injili. Tunatakiwa kuomba sio tu kwa ajili ya Roho Mtakatifu, bali kubatizwa katika Roho, kupokea uwezo mkuu mkubwa.)
II. Utimizwaji
A. Soma Matendo 2:1-4. Tuliona kwamba Roho Mtakatifu alifanya kazi pamoja na Yesu kutoa mfululizo wa mwisho wa maelekezo kwa wafuasi wa Yesu. Je, nini kilicho tofauti sasa? (Roho Mtakatifu amekuja kwa nguvu.)
1. Je, ishara za kuja kwa Roho Mtakatifu kwa nguvu zilikuwa zipi? (Upepo ulivuma kama kimbunga. Moto uliwakalia kila mmoja wao. Walipata karama ya ajabu ya kuzungumza lugha za kigeni.)
2. Kamwe hii haijawahi kunitokea. Je, hii imewahi kukutokea? Aina yote ya makanisa yana picha za moto kwenye alama zao za utambulisho na nembo zao, lakini sio moto halisi makanisani mwao. Kwa kadri ninavyoweza kuelezea, nina Roho Mtakatifu wa “kawaida.” Kamwe sijawahi kuwa na uzoefu wa Roho Mtakatifu wa “hali ya juu.” Kwa nini? (Nimewahi kuwa kwenye mikutano ambapo nilidhani kuwa kwa namna ya pekee kabisa nilijihisi kuwa na Roho Mtakatifu, lakini kamwe sijawahi kusikia upepo wala kuona moto.)
a. Je, ni kwa jinsi gani hawa wanafunzi walipokea uwezo wa aina hiyo? (Mambo mawili. Walikuwa wameahidiwa uwezo huo, na waliomba kwa dhati na bidii kabisa ili kupata uwezo huo.)
B. Je, tumeahidiwa Roho Mtakatifu kwa nguvu?
C. Wasikilizaji walisema (Matendo 2:12) “Maana yake nini mambo haya?” Hebu tusome kile anachokisema Petro kuwa inamaanisha. Soma Matendo 2:14-18. Je, tumeahidiwa Roho Mtakatifu, sio tu uwezo wa kawaida, bali uwezo wa juu/mkubwa? (Ndiyo! Kama miaka elfu mbili iliyopita ilistahili kama “katika siku za mwisho,” je, tungekuwa tunauitaje wakati wetu sasa? Kama Yoeli 2 inasema hii ahadi inahusika kwa wale walio “katika siku za mwisho,” uelewa pekee wenye mantiki ni kwamba unahusika kwetu.)
1. Unakumbuka vitu viwili vilivyohitajika kwa Roho Mtakatifu kuja kwa nguvu? Ahadi ilikuwa ya kwanza, na ombi la dhati ilikuwa kitu cha pili. Je, umeshaomba kwa dhati na kwa bidii kabisa kwa ajili ya Roho Mtakatifu kuja kwa nguvu?
D. Hebu tuendelee kusoma. Soma Matendo 2:22-24. Je, ni kitu gani hiki? (Ujumbe wa injili.)
1. Je, ni wajibu gani alioufanya Roho Mtakatifu mwenye uwezo mkubwa kwenye hii huduma ya ibada/kiinjili? (Soma Matendo 2:32-33. Roho Mtakatifu alikuwa uthibitisho wa ukweli wa ujumbe. Huduma ilipata usikivu wa watu wengine, ilithibitisha kwamba Petro hakuwa amelewa na kuyafanya haya mambo.)
E. Soma Matendo 2:37-39. Je, ni wajibu gani mwingine anaoufanya Roho Mtakatifu? (Roho Mtakatifu alisaidia kuwatia hatiani wasikilizaji kuhusu dhambi zao. (Tazama Yohana 16:8-11.) Roho Mtakatifu pia alikuwa ni thawabu iliyoahidiwa.)
1. Je, Petro alikuwa anaahidi Roho Mtakatifu wa kawaida au yule mwenye uwezo mkuu kama thawabu katika Matendo 2:38? (Je, umewahi kununua kitu na ulipokifikisha nyumbani kikaanza kutokufanya kazi kama ambavyo kilikuwa kikifanya ulipokuwa dukani? Je, ulifanya nini jambo hilo lilipotokea? Sioni jinsi ambavyo Petro alikuwa akifanya jambo lolote zaidi ya kuahidi kile ambacho wamekiona punde – Roho Mtakatifu mwenye uwezo wa hali ya juu.)
F. Soma Matendo 2:40-43. Jibu zuri ajabu! Watu elfu tatu waliongolewa kwa siku moja! Baini rejea kwa Roho Mtakatifu mwenye uwezo wa hali ya juu katika fungu la 43. Je, hii inapendekeza nini? (Kila mtu aliingiwa na hofu kutokana na maajabu na miujiza. Lakini, inaonekana kwamba ni mitume pekee ndio walikuwa wakiitenda.)
1. Je, tunapaswa kuhitimisha kwamba Roho Mtakatifu mwenye uwezo mkubwa anapatikana (alikuwa akipatikana) kwa viongozi pekee?
2. Soma tena Matendo 2:17-18. Je, ni viongozi ndio wanaoelezewa hapa? (Hapana. Ni kinyume chake tu. Vijana na wazee wana karama. Wanawake wana karama. “Watu wote” wana karama.)
3. Rafiki, sijui jibu kwamba ni kwa nini Roho Mtakatifu mwenye uwezo mkubwa hayupo hivi leo. Ninataka kuusikia upepo, kuuona moto na kupata uzoefu wa Roho Mtakatifu mwenye uwezo mkubwa. Nadhani tunahitajika kuomba kwa dhati na kwa bidii kwa ajili ya hili na kuona kile ambacho Mungu atakitenda! Kwa muda huu, hebu tutafutie ufafanuzi suala hili kwa undani zaidi.
III. Mkutano Mwingine wa Kiinjili
A. Soma Matendo 17:16-21. Je, ni aina gani ya majibizano anayoyapata Paulo kwenye mahubiri yake? (Inaonekana kuanzia kutoka kwenye kushuku hadi kwenye udadisi wa wastani.)
1. Je, mambo yangekuwa tofauti kama Paulo angekuwa na Roho Mtakatifu mwenye uwezo wa hali ya juu akitenda kazi pamoja nae?
B. Ukipitia kwa haraka haraka Matendo 17:22-31, utaona kwamba Paulo anawahubiria injili kulingana na ushahidi wa mazingira ya asili. Ujumbe wake ni sawa na wa Petro wakati wa Pentekoste. Petro alidondoa kutoka kwenye Biblia na Paulo alidondoa kutoka kwenye mambo ya asili. Soma Matendo 17:32-34. Je, Paulo ana waongofu wangapi? (Wachache tu.)
1. Petro alikuwa na Roho Mtakatifu mwenye uwezo mkubwa na waongofu 3,000. Paulo hakuwa nae na alikuwa na waongofu wachache. Je, kuna tatizo lolote kwa Paulo? Soma Matendo 9:17. Paulo (Sauli) “amejazwa Roho Mtakatifu.”)
2. Soma Matendo 18:4-5 na Matendo 18:8-11. Je, Paulo yupo na nani kwenye mahubiri yake ya injili? (Tunamtia Paulo hatiani kwa kutokuwa na uwezo/nguvu inayounganishwa na Pentekoste, lakini Mungu anasema kuwa yu pamoja na mahubiri ya Paulo.)
3. Kwa vile Mungu anasema kuwa yu pamoja na Paulo kwenye mahubiri yake, ni kwa nini Roho Mtakatifu mwenye nguvu hayupo?
IV. Ushauri Kuhusu Roho Mtakatifu Mwenye Uwezo wa Hali ya Juu/Uwezo Mkubwa
A. Soma 1 Wakorintho 13:1-3. Je, kuna uhusiano gani kati ya karama za kiroho na upendo kwa watu wengine? (Tunaambiwa kutopoteza mtazamo wa lengo. Lengo la kweli sio Roho Mtakatifu mwenye uwezo mkubwa. Hizi karama za Roho Mtakatifu ni zana za kuiendeleza injili. Kiini cha injili ni upendo kwa Mungu na wanadamu wenzetu. Mathayo 22:37-40.)
B. Soma 1 Wakorintho 14:1. Je, ni mtazamo gani tunaopaswa kuwa nao kuhusu Roho Mtakatifu mwenye uwezo mkubwa? (Tunapaswa kutamani (na kuomba kwa ajili ya) uwezo wote wa Roho Mtakatifu ambao yu radhi kushiriki nasi. Lakini, tunahitaji kutambua kwamba karama za Roho Mtakatifu ni zana kwa ajili yetu kuwaleta watu wengine kwenye Ufalme wa Mungu.)
C. Rafiki, je, utaomba kwa dhati na kwa bidii sio tu kwamba Roho Mtakatifu mwenye uwezo wa hali ya juu amwagwe kwako na kanisani kwako, bali kwamba Roho akupatie moyo wa upendo kwa watu wengine?
V. Juma Lijalo: Ibada Katika Kitabu cha Ufunuo.
Sunday, September 11, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment