Friday, October 21, 2011

Somo la 5: Imani Katika Agano la Kale

Somo Limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Wagalatia 3:1-14)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, umewahi kusumbuka kichwani mwako kuhusiana na swali la kwa nini Mungu anasema “Kwa kuwa mimi Bwana sina kigeugeu” (Malakai 3:6), lakini, inaonekana kwamba Mungu wa Agano la Kale ni tofauti sana na Mungu wa Agano Jipya? Mwonekano wa “Ahadi ya Kale” na “Ahadi Mpya” kwa hakika unaonekana kama una mabadiliko. Mungu amebadili vigezo vya uhusiano wetu! Paulo anatoa hoja kwamba Mungu hajabadili jinsi anavyowasiliana na wanadamu – na njia hiyo ni ya kuhesabiwa haki kwa aimani. Hebu tuzame kwenye somo letu la Wagalatia 3 na kujifunza zaidi!

I. Aliyerogwa!

A. Soma Wagalatia 3:1. Chukulia kwamba umekaa pembeni ukimsikiliza Paulo akisema maneno haya kwa Wagalatia. Je, wamedharauliwa?

1. Kama ndivyo, kwa nini? (Paulo anasema kuwa wanaenenda kama watu “waliorogwa” na kama wale walio chini ya ushawishi wa mwovu. “Enyi waovu msio na akili (wapumbavu).)

2. Je, hivi ndivyo ambavyo Paulo anapaswa kuzungumza na wale ambao hivi leo wanaamini kuwa wanaweza kuokolewa kwa matendo yao wenyewe?

B. Ninasita kuwaita washiriki wenzangu wa kanisa kuwa “waovu wasio na akili (wapumbavu),” kwa hiyo lazima Paulo atakuwa alikuwa na sababu nzuri ya kuwaita kuwa wapumbavu. Je, ni sababu gani anayoitoa katika Wagalatia 3:1? (Walimwona akielezea kuhusu Yesu kusulubiwa.)

1. Tafakari kuhusu jambo hili. Kwa nini kusulubiwa kwa Yesu kunawafanya Wagalatia kuwa wapumbavu? Au, kuwa wenye mapepo? (Kwa nini Mungu afe kifo cha uchungu mikononi mwa uumbaji wake? Dhana hii ni ya kipuuzi kama inavyoonekana. Ni pale tu unapoona kuwa tulisulubiwa pamoja na Yesu (Wagalatia 2:20) ili kukamilisha matakwa ya sheria, ndivyo inavyoonekana kuwa ni upuuzi na kama kuwa na mapepo kufikiria kuwa juhudi zetu zina maana.)

2. Hebu tutumie mfano. Unatengeneza sanamu kutoka kwenye kipande cha mti, na kisha unailetea sadaka kila asubuhi ili iweze kukusamehe dhambi zako. Je, huo ni upumbavu? (Ndiyo! Kwa sababu wewe ndiye umeitengeneza sanamu hiyo.)

a. Je, hiyo ni sawa na kuwa na mapepo? (Shetani anataka tupuuze au tusiamini kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa hiyo, ni kweli, haya ni mapepo – hususan kwa vile yanatufanya tudai kuwa tunafanya kazi ya Mungu.)

C. Soma Wagalatia 3:2-5. Sawa, Paulo anasema kuwa, enyi watu wapumbavu, nina swali moja kwenu. Sasa tunaona kuwa lazima Paulo awe ni mwanasheria, kwa sababu “neno lake moja tu” linazaa maswali kadhaa! Maswali ambayo angependa kupata majibu ya kiuerevu!


1. Je, Roho Mtakatifu anakuja kwa kuitii sheria au kwa kuamini katika kile alichokisema Yesu?

a. Hebu ngoja niulize swali langu mwenyewe hapa. Je, Roho Mtakatifu yu maishani mwako? Kama sivyo, je, inawezekana ni kwa sababu unatumia njia mbaya?

2. Baada ya kumpata Roho Mtakatifu maishani mwako ili akuongoze, je, unadhani kwamba unaweza kufanya kazi nzuri ya kujiongoza mwenyewe?

3. Kama umeteswa kwa sababu ya imani yako, je, unataka kuitupilia mbali?

4. Je, unaona miujiza maishani mwako kwa sababu ya kuitii sheria, au kwa sababu ya uwezo wa Mungu unaofanya kazi kupitia kwenye imani?

a. Hebu ngoja niulize maswali kadhaa hapa. Je, unaiona miujiza maishani mwako? Kama sivyo, je, inawezekana ni kwa sababu unatumia njia mbaya?

b. Unapozungumza na watoto wako, je, unaizingatia zaidi sheria au unamzingatia Roho Mtakatifu?

(1) Kama una watoto walio katika umri wa kubalehe, jaribu kukaa nao na kuwauliza haya maswali na jinsi watakavyoyajibu na wanadhani kuwa wewe utajibuje.

(2) Kama hauoni miujiza maishani mwa wanao, je, ni kwa sababu umekuwa ukiivunja sheria badala ya uwezo na neema ya Mungu? (Najua kwamba nimekuwa nikiwaambia wanangu mara zote kwamba “wawe watiifu!” Baba yangu alikuwa akisema “Ninyi ni wana wa Don Cameron, mwenende kama yeye!”)

5. Maswali manne yaliyopita niliyoyanukuu kutoka kwa Paulo ni maswali yasiyohitaji majibu – ikimaanisha kwamba ni maswali ya wazi kabisa yakiwa na majibu ya dhahiri. Mtu anayeuliza swali lisilohitaji jibu hahitaji jibu lako, anakutaka wewe uone dhana ya dhahiri kabisa. Je, dhana ya wazi ya Paulo ni ipi? (Uwezo wa Mungu, na kutoishika sheria, ndio chanzo cha maisha mazuri ya Mkristo.)

D. Hebu tusimame kidogo na kupitia hoja za Paulo za kuhesabiwa haki kwa imani. Hoja yake katika sura ya kwanza ni kwamba Yesu alimpatia yeye ujumbe wa kuhesabiwa haki kwa imani pekee moja kwa moja. Madai yake katika sura ya pili ni kwamba viongozi wa kanisa walikubaliana naye, ingawaje kuuweka ujumbe wake kivitendo ilichukua muda, na baadhi yao, kama vile Petro, mara kadhaa walitoka nje ya msitari. Hoja yake mwanzoni mwa sura ya tatu ni kuangalia jinsi Mungu anavyofanya kazi maishani mwetu wenyewe.

II. Mfano wa Ibrahimu

A. Soma Mwanzo 12:1-3. Je, wajibu wa Abramu katika historia ya sayari yetu ni upi? (Yeye ndiye mwanzo wa kundi maalum la watu ambao kupitia kwao Mungu alikuwa amepanga kuwabariki watu wote wa dunia.)


B. Soma Wagalatia 3:6. Je, kwa nini Mungu anamgeukia Paulo kama mfano? (Paulo anasema kwamba tangu mwanzo kabisa mwa mahusiano maalum ya Mungu na kundi maalum la watu (kwa lengo la kuhamasisha mapenzi ya Mungu), kuhesabiwa haki kwa imani ndio ilikuwa kanuni.)

C. Hebu tuangalie kisa hiki kidogo. Soma Mwanzo 15:1-6. Je, hiki ni kisa kuhusu Uungu (Umungu)? Kuhusu haki? (Mungu alimwambia Abramu (Mwanzo12:3) kwamba ndiye atakayekuwa chombo ambacho kupitia kwacho dunia yote itabarikiwa. Sehemu ya mustakabali kwa ajili ya hili ilikuwa (Mwanzo 12:2) kwamba Abramu atakuwa na wazao wengi. Kama Mungu alikwambia kuwa utakuwa na kanisa kubwa kabisa kupita yote katika maeneo yanayokuzunguka, na kanisa hilo kubwa ndilo litakuwa chanzo cha mibaraka kwa ajili ya jamii inalolizunguka, je, ungefanyaje?? (Ningeanzisha kanisa!)

1. Kwa nini hilo halitendeki kwa Abramu? (Huenda Abramu anafanyia kazi suala la kupata mtoto. Lakini, suala la msingi ni kwamba Abramu lazima kwanza amwamini Mungu ili kufanya jambo hilo litokee. Lazima atambue kwamba hii ni kazi ya Mungu na wajibu wa Mungu. Abramu hana uwezo wake binafsi kufanya jambo hilo. Kwa hakika, pale ambapo Abramu na Sarai wanafanya mpango wa kutekeleza suala hili kwa uwezo wao wenyewe (Mwanzo 16), inakuwa balaa -yaani mambo yanakuwa magumu/yanaharibika.)

2. Je, kisa hiki cha Abramu kinatusaidia tuelewe vizuri zaidi suala la kuhesabiwa haki kwa imani? (Mungu hatwambii tulale kwenye maisha yetu ya Ukristo. Anatuambia tuwe na imani naye. Hii ni kazi yake. Ni Roho wake. Hatuwezi kuifanya sisi wenyewe.)

D. Soma Wagalatia 3:7-9. Je, Ibrahimu, baba wa watu wa jamii ya Kiyahudi, ni baba yetu pia? (Hii ndio hoja ya Paulo iliyounganishwa. Mungu wa Agano la Kale ana hii njia isiyobadilika kwa wanadamu. Mtazamo wa watu wake maalum umepanuka – Mungu asifiwe kwa kuwaunganisha watu wa mataifa na watu wake maalum – lakini mpango wa msingi haujabadilika!)

III. Laana

A. Soma Wagalatia 3:10. Sijui wewe unasemaje, lakini mimi huwa ninakuwa na wasiwasi pale watu wanapoanza kutoa laana. Je, kwa nini watunza sheria sana hawakosei tu? Kwa nini wanalaaniwa? (Soma Kumbukumbu la Torati 27:26. Kama kuitunza Sabato, kuachana na vitendo vya wizi, mauaji, tamaa, na uzinzi ndivyo msingi wako wa wokovu, basi wewe umelaaniwa. Kwa nini? Kwa sababu huwezi kuyafanya mambo haya. Kama ukisema kwamba kufanya jambo lolote kati ya haya ni muhimu kwa ajili ya wokovu, basi umejihukumu wewe mwenyewe!)

B. Soma Wagalatia 3:11-12. Je, wenye haki wanaishi kutokana na utii wa sheria? (Hapana. Wanaishi kwa haki kwa imani.)

C. Yote haya yananifanya nitahayari. Sitaki kulaaniwa, lakini ninaiangalia sheria kwa ukaribu sana. Kumbukumbu la Torati 6:8 inasema “zifunge [amri] juu ya mkono wako.” Hivi karibuni nimeanza kuvaa kikuku/bangili mkononi mwangu ambayo ina Amri Kumi. Soma Wagalatia 3:13. Je, ni kwa nini ni lazima tusiegemee kwenye utii wa sheria ili tuweze kuokolewa? (Yesu tayari alikwishafanya hivyo kwa ajili yetu. Yesu alilaaniwa ili kwamba tusiweze kulaaniwa kwa kushindwa kwetu kuitii sheria. Sio hivyo tu, Yesu alilipa adhabu kwa ajili ya laana yake – na kwa hiyo kwa ajili ya laana yetu.)

IV. Utaratibu Mpya na wa Zamani


A. Soma Wagalatia 3:14. Je, tunapaswa kuwa na wasiwasi kuhusiana na kutunza sheria (ikijumuisha Amri Kumi)? (Hapana. Badala yake, lazima tuwe na Roho Mtakatifu anayeishi maishani mwetu!)

1. Kama wewe pia unatahayari sasa hivi, basi utabaini kwamba hali iyo hiyo inamkabili Ibrahimu. Je, Ibrahimu anapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu kuwa na wazao wengi? Je, alipaswa kuwa na wasiwasi kuhusu Yesu kuzaliwa kutoka katika mmojawapo wa wazao wake? (Hapana! Kile ambacho Mungu alimtaka Abrahamu afanye ni kumtumainia yeye. Kumwamini yeye.)

2. Je, kuna kitu chochote kilichobadilika kwenye uhusiano kati ya wanadamu na Mungu? (Hakuna kilichobadilika tangu enzi za Ibrahimu! Ibrahimu aliamini katika ahadi – ambayo ilijumuisha Yesu kuja kuchukua nafasi yetu. Tunaamini kwamba ahadi imetimizwa na tunaipokea/tunaikubali zawadi hiyo kwa imani.)

B. Rafiki, je, utakaa mbali na laana, na kuitegemea haki pekee inayokujia kwa imani katika Yesu?

V. Juma lijalo: Kipaumbele (Umuhimu) cha Ahadi.

1 comments:

  1. Nimefurahi sana kukumbana na Blogu inayotukuza lugha ya Kiswahili. Nadhani mada zinazoongelewa ni za kuvutia na raha sana kuona Kiswahili kinatukuzwa. Hongera sana.
    Ila sijaelewa kwanini neno "Lesoni" linatumiwa kuiita Blogu muhimu kama hii badala ya "Somo" , "Darasa" au "Mafunzo" ambayo ni maneno sahihi ya Kiswahili. "Lesoni" inatokana na "Lesson" la Kiingereza. Hakuna haja ya kuazima maneno ya kigeni ilhali Kiswahili kinajitosheleza kimsamiati.
    Au je kuna hazina nyingine iliyojificha ambayo sikuiona?

    ReplyDelete