Friday, October 28, 2011

Somo la 6: Kipaumbele (Umuhimu wa) cha Ahadi

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Wagalatia 3:15-20)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, umewahi kuwa kwenye hali ambapo imani yako inatiwa changamoto na mtu ambaye unadhani kuwa yuko sahihi? Mwanzoni unajisikia kukereka. Kisha unaanza kujisikia vibaya kwamba umekuwa ukikosea. Kisha unaangalia muktadha wote tena ili uwe na uhakika kwamba una mtizamo sahihi. Somo letu la Biblia juma hili linanikumbusha kuhusiana na suala hili. Paulo anatuambia kwa ujasiri kabisa kwamba Abrahamu aliokolewa kwa neema, sio kwa matendo. Lakini, baadaye wapinzani wa Paulo wanaibua hoja nzito: kama mpango wa wokovu ulikuwa ni kupitia imani pekee, kwa nini baadaye Mungu alitupatia Amri Kumi? Je, hiyo ina mantiki gani endapo Amri Kumi sio mpango wa Mungu wa sasa? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kukibaini kwamba nani yuko sahihi!

I. Hoja ya Mkataba

A. Juma lililopita tuliishia kwenye somo ambapo Paulo alibainisha kuwa uhusiano wa kuhesabiwa haki kwa imani aliokuwa nao Abrahamu kati yake na Mungu sasa unapatikana kwetu. Habari njema hii! Hebu tuendelee kwa kusoma Wagalatia 3:15. Je, Paulo analeta hoja ya aina gani? (Analeta hoja ya kisheria. Hii ni hoja iliyoelemea kwenye mkataba wa kisheria.)

1. Kwenu wana sheria, je, Paulo anahoji kitu gani? (Mikataba inatekelezwa kama jinsi ilivyoandikwa. Mkataba wa Abrahamu na Mungu (wokovu kwa njia ya imani pekee) ni makubaliano halali yanayotekelezeka.)

2. Je, nadharia ya kisheria ya Paulo iko sahihi? Je, inawezekana kuiweka pembeni mikataba ya kisheria? (Kwa ujumla, hapana. Sio ya kisheria. Kama una mkataba halali na mtu, unaweza kwenda mahakamani kuutekeleza mkataba wako.)

B. Soma Wagalatia 3:16-18. Utabaini kuwa sasa Paulo anakiita kile alichokipokea Paulo kuwa ni “ahadi.” Je, ahadi zinatekelezwa kisheria? (Ni hadi pale utakapozipa umuhimu. Hiyo inamaanisha “ni hadi pale utakapoahidi kubadilishana kitu cha thamani.” Kama ukiahidi kunipatia gari lako, nami nikaahidi kukupatia dola za Marekani 20,000, tuna mkataba unaotekelezeka na sio ahadi isiyotekelezeka.)

1. Je, kuna umuhimu gani, kama upo, ambao Abrahamu alimpatia Mungu?

2. Kwa uhakika kabisa, kuna mjadala mkubwa wa namna ambavyo Paulo anatafsiri ahadi ya Mungu kwa Abrahamu (angalia, kwa mfano, Mwanzo 12:3) na hususan neno “uzao.” “Nitauacha huo mjadala, kwa sababu Paulo anaielezea tena hoja yake kwa njia yenye kuleta ubishani kidogo kwenye mafungu ya 17-18. Je, ni kweli kwamba mkataba wa baadaye haubatilishi makubaliano ya awali? (Ndiyo. Kama wewe na mimi tumekubaliana masharti ya mkataba, unaweza kujitolea kubadili masharti, lakini sio lazima nikubali.)


3. Je, hoja ya kiteolojia ya Paulo ni ipi? (Hoja ni kwamba kama mkataba “uliojadiliwa” na Abrahamu ulikuwa kwamba kama aliamini atapata wokovu, basi Mungu hawezi kubadili huu mkataba baadaye kwa kusema kwamba lazima tuzitii amri ili kuweza kuupata wokovu.)

II. Hoja Kinyume na Mkataba

A. Soma Wagalatia 3:19. Hebu tusome “kwa undani zaidi (kupata maana iliyojificha)” na tujaribu kubaini, kwa mujibu wa ukanushi wa Paulo, kile ambacho wapinzani wa Paulo walikuwa wakikihoji. Je, unadhani hoja ya wapinzani wa Paulo iliyokuwa ikipinga hoja ya Paulo ilikuwa ni ipi? (Kama imani ndio ilikuwa makubaliano kati ya Mungu na wanadamu, basi je, ni kwa nini baadaye Mungu alitoa sheria yake?)

1. Je, wapinzani wa Paulo wanaleta hoja nzuri ajabu? (Tunaweza kulielewa hili kwa njia mbili. Hivi punde tu tumejadili uelewa wa aina moja - kama kweli tuna mkataba, kinyume na ahadi tu, tunaweza kutekeleza mkataba halisi dhidi ya Mungu. Njia ya pili ya kuliangalia hili ni kama sheria mpya. Kule Marekani, kama kuna sheria ya zamani na sheria mpya kabisa, na kuna ukinzani kati ya hizo sheria mbili, basi sheria mpya ndio inayotumika (ndio hutawala).)

2. Hebu tuangalie hii hoja ya pili – kwamba Mungu alitoa sheria baadaye (pale Sinai) iliyobadili sheria ya zamani (aliyopewa Abrahamu). Je, nadharia za kweli zipo sahihi kwa kiasi gani katika hii hoja iliyo kinyume?

a. Soma Mwanzo 2:2-3 na Kutoka 20:8-11. Je, amri ya Sabato ilianzia Sinai? (Hapana.)

b. Soma Mwanzo 4:8, Mwanzo 4:10-12 na Kutoka 20:13. Je, uzuiaji wa mauaji ulianzia Sinai? (Hapana.)

3. Je, wapinzani wa Paulo wana tatizo la kweli la wazi kabisa kuhusiana na hoja yao? (Ndiyo. Kama kile kilichotolewa pale Sinai kilikuwepo kabla Abrahamu hajazaliwa, basi hii hoja ina tatizo kubwa sana.)

4. Kumbuka kwamba lazima pawepo na ukinzani kati ya sheria ya zamani na mpya ili sheria mpya iweze kuchukua udhibiti. Je, kuna ukinzani kati ya haki kwa imani na sheria iliyotolewa pale Sinai?

a. Kama umejibu kuwa, “ndiyo,” je, dhambi zilisamehewaje katika mfumo wa patakatifu?

(1) Je, watu walitakiwa kupiga “push-ups” walipotenda dhambi?

(2) Je, walitakiwa kulipa faini?

(3) Je, walitakiwa kuahidi kutojihusisha na dhambi hiyo hiyo kwa kipindi cha mwaka mzima? (Hapana. Walitoa kondoo asiye na mawaa. Hii ilikuwa/ni sio “matendo.” Ilirejea makubaliano na Abrahamu na kuangalia mbele kile ambacho Yesu angekifanya ili aweze kutupatia neema kwa ajili yetu.)


5. Kama tunaweza kuona hizi dosari kwenye hoja za wapinzani wa Paulo, je, wana hoja yoyote yenye mantiki? (Lazima watakuwa wanahoji, “Kwa nini Mungu aliijali sana sheria mamia ya miaka baada ya kufanya makubaliano ya neema kati yake na Abrahamu?”)

a. Je, Mungu anatoa jibu gani kwa swali hili? (Wagalatia 3:19 – Kwa sababu ya kiasi cha dhambi (“uvunjaji wa sheria”).)

B. Hebu turejee nyuma kidogo. Je, unadhani wana wa Israeli walifahamuje kuhusiana na Mungu wao baada ya mamia ya miaka ya utumwa kule Misri? (Huenda hawakufahamu sana. Hii inafanya maoni ya Wagalatia 3:19 isemayo kuwa “makosa ya sheria (uvunjaji wa sheria)” ilete mantiki. Watu wa Mungu sio tu kwamba walikuwa wakitenda dhambi, bali pia hawakuwa na wazo lolote kuhusiana na kiwango cha Mungu cha tabia/mwenendo. Mungu alihitaji watu wake wajue kile alichokichukulia kuwa ni dhambi.)

1. Kama Mungu aliweka mkataba na Abrahamu kwamba aliokolewa kwa neema, pale sheria ya Mungu ilipofahamika na Abrahamu, je, hiyo inasema nini kuhusu uhusiano kati ya imani na sheria? (Inasisitiza wazo la kwamba makubaliano yetu na Mungu ni ya wokovu kwa imani, na sio kwa kuishika sheria. Lakini, pia inasema kitu muhimu kuhusu sheria.)

2. Je, sheria ya Mungu ni muhimu kwake na kwetu? (Ndiyo. Ikiwa neema, bila rejea yoyote kwa sheria, ilikuwa ni mkataba kati ya Abrahamu na Mungu, basi Mungu asingekuwa na haja ya kuanzisha Amri Kumi (na sheria zote zilizosalia) pale Sinai kwa watu ambao hawakujua kitu chochote kuhusiana na sheria.)

C. Soma Warumi 3:19-20. Je, fungu hili linakubalianaje na hali ya watu wa Mungu pale Sinai? (Kwa hakika hiki ndicho tulichokuwa tukikijadili! Mungu anatumia sheria yake kutufanya tuwe na utambuzi wa dhambi zetu. Je, tunawezaje kuitambua dhambi bila sheria? Tungekuwa tunajivuna/tunajisifu kuhusu kuhesabiwa kwetu haki kama tusingekuwa na sheria ya kutunyamazisha.

D. Soma Warumi 3:21-24. Je, tunakuwaje wenye haki? (Kwa imani katika Yesu. Kwa kumwamini Yesu.)

E. Soma Warumi 3:25-26. Je, patakatifu pa Agano la Kale pana sehemu gani katika hili? (Paulo anatumia taswira ya mfumo wa kafara kuelezea kazi ya Yesu. Huu ndio umoja tunaouona pale Sinai, sio mtafaruku ambao ungehitaji kuusema “Mungu alianzisha sheria mpya pale Sinai iliyo juu ya makubaliano ya zamani ya neema na Abrahamu.”)

III. Mjumbe (Mpatanishi)

A. Hebu turejee kwenye Wagalatia 3. Soma tena sehemu ya mwisho ya Wagalatia 3:19 na uongezee Wagalatia 3:20. Tunaona neno jingine la kisheria: “mjumbe.” Je, mjumbe ni nani? (Sio mwanasheria anayewakilisha upande mmoja. Badala yake, mjumbe anapaswa kufanya kazi na pande zote mbili ili kufikia muafaka wa ugomvi/mgongano kati ya pande mbili. Kuzifanya pande zote mbili zifikie suluhisho/muafaka.)

1. Hii inamaanisha kuwa mjumbe (mpatanishi) pamona na malaika wanaiweka mbele sheria. Je, sheria inaenenda kama mjumbe kati ya Mungu na wanadamu?

a. Je, sheria imemfanyia nini Mungu?


b. Je, uelewa wetu wa sheria umetufanyia kitu gani? (Maoni mbalimbali yanatofautiana kuhusu kile ambacho fungu la 20 linamaanisha. Maoni ya jumla ni kwamba Musa anachukuliwa kama “mjumbe (mpatanishi).” Lakini, ninaona kwamba sheria inafanya kazi kama mjumbe nyakati mbili muhimu tofauti kutuweka pamoja na Mungu. Kwanza, sheria inatuonyesha upendo wa Mungu. Mungu alitufilia ili kutimiza matakwa ya sheria. Pili, sheria ni kiwango – kiwango tusichoweza kukifikia. Sheria inatufanya tuikubali kafara ya neema ya Yesu – ikiwa ni shukrani kwa Mungu, na kutokujiweza kwetu mbele ya sheria. Je, nini kinaweza kutuleta karibu na Mungu zaidi ya hicho?

c. Je, sheria inaathirije mtazamo wetu dhidi ya utii? (Yesu anasema, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Yohana 14:15. Kwa hakika huu ni ukweli mtupu! Kama tunaiheshimu kafara ya Yesu, tunaona kwamba sheria lazima itakuwa ni ya muhimu sana kwa Mungu. Vinginevyo, Mungu angeipuuza sheria na kumwokoa Yesu kutoka katika kifo cha kutisha. Upendo wa Mungu katika kukazia kutimiza matakwa kunatusaidia kuitikia kwa upendo kwa kudhamiria kwamba tutaishi, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, maisha yanayompendeza Mungu. Sasa tunaweza kuona (Wagalatia 3:20) kwa nini “Mungu ni mmoja,” kwenye mfumo wake kwa sababu wokovu ni “mmoja.”)

B. Rafiki, kama bado hujakubali kikamilifu kuhesabiwa haki kwa imani pekee, je, utaikubali sasa hivi? Kwa nini usimwombe Yesu akusamehe dhambi zako, na akuokoe kwa neema yake?

IV. Juma lijalo: Njia ya Kuielekea Imani.

0 comments:

Post a Comment