Sunday, November 6, 2011

Somo la 7: Njia ya Kuielekea Imani

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Wagalatia 3:21-25)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Juma lililopita tuliona changamoto ya mwanasheria: “Kama kuhesabiwa haki kwa imani ndio njia sahihi, je, ni kwa nini Mungu aliianzisha sheria pale Sinai miaka 430 baada ya mkataba wake wa kuhesabiwa haki kwa imani na Abrahamu? Tulipojaribu kufumbua (kufasiri) kile ambacho mwanasheria alikuwa akikihoji, tulifikia uamuzi kwamba mojawapo ya hoja inafahamika vizuri sana na wanasheria wa Marekani. Unapokuwa na sheria mbili zinazokinzana, sheria mpya inashika hatamu dhidi ya sheria ya zamani. Sinai ilikuja baada ya Abrahamu! Hata hivyo, ili kuweza kuishinda hii hoja, wanasheria walihitaji kitu zaidi ya muda tu, walihitaji ukinzani baina ya Sinai na kuhesabiwa haki kwa imani. Hebu tuzameni kwenye Biblia zetu ili tuweze kuchunguza mwendelezo wa hoja ya Paulo kuhusiana na huu mtafaruku/ukinzani!

I. Mtafaruku/Ukinzani

A. Soma Wagalatia 3:21. Je, kuna ukinzani kati ya sheria na kuhesabiwa haki kwa imani? (Paulo hasemi tu kwamba “hapana,” bali “kwa hakika kabisa hapana.”)

1. Je, umewahi kugundua kuwa mara nyingine watu huwa wanapiga kelele ili waweze kuficha makosa yao? Je, kuongea kwake kwa mkazo kwa kutumia maneno “kwa hakika kabisa hapana” ni njia ya kuficha udhaifu kwenye hoja yake?

2. Mara nyingine huwa hatuuoni msitu kwa sababu tunauangalia kwa ukaribu sana mti mmoja. Paulo anawezaje kusema kuwa hakuna ukinzani? Je, kwani haandiki hii barua kwa Wagalatia kwa sababu ya ukinzani? Kwani haikumpasa kumkemea Petro kwa sababu ya ukinzani/mtafaruku? (Angalia Wagalatia 2:11-14.) Je, kwani hatulijadili hili sasa hivi kwa sababu ya ukinzani/mtafaruku?

3. Ninaweza kufikiria kwa njia nyingi jinsi ambavyo sheria na neema zinatofautiana/zinapingana. Sheria inasema kuwa “tii la sivyo utakufa.” Neema inasema kuwa “amini na uishi.” Je, ni kwa njia gani Paulo anasema kuwa “kwa hakika kabisa” hazipingani? (Sheria haiwezi kutupatia uzima. Paulo anasema kuwa sheria haina chochote cha kutupatia haki. Kutupatia haki sio kusudi lake. Kama sheria ingeweza kutuokoa, basi wanasheria wangekuwa sahihi kuhusiana na ukinzani na kipaumbele cha sheria mpya.)

4. Hebu tupunguze mwendo kidogo kwa muda mfupi na kulitafakari hili. Je, kwani wanasheria hawadhani kwamba kusudi la sheria ni kutupatia wokovu? Kama unadhani kuwa ahadi na sheria vina kusudi moja, basi unapaswa kuendana na sheria, sawa? (Hii inatufanya tuchunguze umuhimu wa suala hili – je, sheria na ahadi vina lengo moja?)

II. Kusudi/Lengo

A. Soma Wagalatia 3:22-23. Paulo anasema kuwa sisi sote ni wafungwa. Je, wafungwa wanataka nini? (Uhuru. Heshima.)


1. Je, kwa nini hatutaki kuwapa wafungwa uhuru? (Kwa sababu hawaustahili.)

2. Je, kwa nini tunastahili kufungwa jela? (Kwa sababu ya dhambi.)

3. Unaonekana kuwa kwenye kundi zuri ajabu kwangu! Je, nani aliye mfungwa wa dhambi? Kila mmoja hapa. “Dunia yote.”)

4. Je, hivi punde tu hatujagundua kwamba hoja ya Paulo ya “hakuna ukinzani kwa hakika kabisa” ina makosa kwa uhakika kabisa? Kama sheria inatufanya kuwa wafungwa, na neema inatuweka huru, kwangu mimi hiyo inaonekana kuwa kama ukinzani mkubwa sana!

a. Kama tukiangalia lile swali la “lengo/kusudu” je, kusudi la vyote viwili, yaani sheria na neema, sio kubainisha kama tusalie kuwa wafungwa kwenye jela?

B. Hebu tuangalie mfano wa kivitendo. Tuseme kwamba sheria A inatuambia kuwa kama tuna hatia kwenye kodi zetu, tunaweza kuepuka adhabu yoyote kama tukilipa kodi zetu au tukijiunga na kanisa. Sheria B inasema kuwa kwa wale wasiolipa kodi zao, basi adhabu yao ni kwamba wanatakiwa kwenda gerezani. Je, hizo sheria mbili zinakinzana? Enyi wanasheria, je, mahakama itaitupilia mbali sheria ya kwanza? (Hapana, hutaitupilia mbali sheria ya awali. Badala yake, nitasema kwamba hizo sheria mbili zinaweza kuhuwianishwa kwa kutamka kwamba sheria ya awali ilisababisha vitu visivyofuata sheria kwenye kanuni ya jumla.)

C. Angalia tena Wagalatia 3:23. Sisi ni wafungwa kwenye mahabusu. Imani inakuja kututembelea. Je, hii kauli ya “imani hii ilikuja” inamaanisha nini? Je, inamaanisha kwamba ulipata na kuendeleza imani ya namna fulani hivi? (Wagalatia 3:22 inarejea “imani ya Yesu Kristo,” lakini hapa inaonekana kuwa rejea ni kwa Yesu. Yesu (“imani hii”) alipokuja, basi uvunjaji wa mahabusu uliwezekana.)

III. Mtazamo Mpana

A. Utakumbuka kwamba juma lililopita tulichunguza usahihi wa ukweli wa hoja inayohusiana na muda ya mwanasheria: kwamba sheria ilikuja baada ya ahadi kwa Abrahamu. Tuligundua kwamba hii haikuwa kweli kwenye Amri Kumi. Amri ya Sabato na amri ya mauaji zilifahamika kwa wazi kabisa tangu wakati wa Adam na Hawa. Je, ilikuwa tu sheria inayohusiana na kafara (sheria ya “mapokeo”) ndio ilikuja baadaye?

1. Soma Mwanzo 4:3-5. Je, hii inasema nini kuhusiana na mapokeo? (Mapokeo yalikuwepo. Juma lililopita tulikiangalia kisa hiki katika kujifunza kwamba sheria ya maadili tayari ilikuwepo. Sasa tunaona kwamba kisa hiki kinahusisha sheria zote mbili, yaani ya maadili na ya mapokeo!)

2. Soma Mwanzo 7:1-3 na Mwanzo 7:7-9. Je, kwa nini tunaona rejea ya wanyama walio safi na wanyama wasio safi zamani kabisa kabla ya Walawi 11 na rejea yake kwa wanyama ambao “sio wasafi kimapokeo” (Walawi 11:4)?

3. Je, inawezekana kwamba wanasheria wamekosea, na kwamba sheria ya maadili na sheria ya mapokeo ilikuwepo tangu mwanzo kabisa? Kama hivyo ndivyo, je, ni kwa nini Mungu anafanya hivyo?


a. Paulo anasema kwamba Mungu ana lengo tofauti kwenye sheria kuliko vile anavyofanya kwenye neema. Je, hiyo inakubaliana na wazo la sheria ya maadili na mapokeo iliyokuwepo tangu mwanzo? (“Kwa hakika kabisa!” Hii inaonyesha kwamba Mungu alidhani kuwa sheria hizi mbili zilikuwa na malengo tofauti.)

IV. Mwangamizaji/Mpondaji

A. Soma Wagalatia 3:24. Hebu tangalie kwa makini kauli isemayo kuwa “sheria iliwekwa kuwa kiongozi.” Baadhi ya tafsiri za Biblia zinasema sheria ilikuwa “mwalimu mkuu.” Nimesoma maoni kadhaa yanayosema kuwa Uyunani inamrejea mtumwa ambaye ni kiongozi wa wana wa bwana wake. Ni kama vile “yaya” hivi leo. Utabaini kuwa Paulo anatuita majina kadhaa hapa. Tayari ameshatuita kuwa wafungwa. Sasa anaongezea “watoto wasio na akili,” “watoto wadogo wanaohitaji maelekezo ya watu wazima.” Je, huyo ni wewe?

1. Likiwa kama suala la kivitendo, je, lengo la mtoto kwenda shule ni lipi, kulelewa na yaya au kufundishwa?

2. Je, ulijifunza nini shuleni? Je, ulijifunza nini kutoka kwa “yaya” wako (tuchukulie kuwa ulikuwa na yaya) au wazazi wako (tuchukulie kuwa hukuwa na yaya)? (Nilijifunza mambo mawili shuleni. Kwanza, nilijifunza mambo chanya ambayo nitayahitaji nitakapokuwa mkubwa. Pili, nilijifunza mambo hasi kunihusu mimi. Kwa kadri nilivyoendelea kwenda shule, ndivyo nilivyojiona kuwa bubu zaidi.)

a. Kama, kutokana na vile tulivyobaini, Mungu alitupatia ahadi ya neema na matakwa ya sheria zikiwa pamoja katika kipindi cha historia ya wanadamu, je, lengo la sheria kwa mwalimu mkuu, yaya, mkuu wa gereza ni lipi? (Sio tu kutufundisha kiwango cha ukamilifu wa Mungu, bali kupondaponda kiburi/majivuno yetu. Kutufundisha kuwa sisi sio watu werevu sana na wenye utii mkubwa kupindukia. Kutufundisha kwamba uanadamu kwa ujumla, na hususan wewe, huwezi kuishika sheria ya Mungu.)

b. Soma Mathayo 5:27-28. Je, Yesu na Paulo wako kwenye njia moja? (Yesu anatupatia mtazamo wa wajibu wa kweli wa sheria ambao unatuondolea kiburi/majivuno yetu.)

B. Utabaini kwamba Wagalatia 3:24 inasema kuwa sheria “inatuelekeza kwa Kristo.” (Ukweli kwamba tunafungwa jela kwa dhambi inatufanya tutafute nji ya kutokea. Ukweli kwamba kiburi/majivuno yetu yamekwisha, na kwamba tunatambua kuwa tunahitaji neema, kunatufanya tuitafute neema. Yesu ndiye njia ya kutuondoa dhambini. Kwa hiyo, wajibu wa sheria ni kutuelekeza kwa Yesu na ahadi yake ya neema.)

V. Uhuru

A. Soma Wagalatia 3:25. “imani imekuja” – ikimaanisha kuwa Yesu alikuja duniani, akaishi na kufa kwa ajili yetu (kwa niaba yetu), na akafufuka kwenye uzima wa milele ili kwamba tuweze kuokolewa. Sheria imekuongoza, mfungwa wa dhambi uliyepondwapondwa, hadi kwenye hiki chanzo kikubwa cha uhuru ulichokikubali kwa imani. Je, tupo pamoja hadi kufikia hapo?

1. Hebu tufuatilie mantiki ya Paulo inayofuatia. Watoto wanapokua, je hawapo tena chini ya uangalizi wa walimu wao wa shule ya awali/msingi, mayaya wao au wakufunzi wao? (Hapana.)

a. Je, ni aina gani ya tabia utakayoitarajia? (Tabia ya kisomi! Hiyo ndio sababu tunawapeleka shule.)


2. Je, nini kinatokea kama mtoto mkubwa anakiuka kanuni za shule, yaya au mkufunzi? (Hakitokei kitu chochote – kinachohusiana na nidhamu iliyofundishwa shuleni, na yaya au mkufunzi. Lakini, isipokuwa tu kama hawa walimu hawakuwa na umuhimu wowote, kukiuka kanuni kunaweza kuwa na matokeo ya kivitendo.)

3. Je, tupo chini ya uangalizi wowote sasa? (Kama tuko sahihi kwamba mara zote Mungu alikuwa na sheria na neema mbele za macho ya wanadamu, hiyo inamaanisha mambo kadhaa:

a. Mara zote imekuwa ni lengo la Mungu kwa sisi kuelewa kiwango chake, ambacho kinapondaponda mawazo yetu yenye kiburi ili tuweze kufikia kiwango chake; na,

b. Kutuelekeza kwenye ahadi yake ya neema (ambayo imeshatimizwa). Kuielewa taswira kamili ndio “uangalizi” wetu wa sasa. Sote tunaelewa kiwango cha Mungu kwa ajili ya maisha yetu, na tunataka kufanya jambo lolote kwa ajili yake kwa sababu ya zawadi yake ya neema.)

B. Rafiki, je, umejawa kiburi kiasi kwamba unaweza kuupata wokovu? Yaani kitu unachoweza kukifanya kitamfanya Mungu akuzawadie thawabu ya milele? Kwa nini usikiri kiburi/majivuno yako hivi leo, na uingie kwenye mahusiano yenye kubadili maisha ukiwa na Mungu?

VI. Juma lijalo: Kutoka Utumwani Hadi Kuwa Warithi.

0 comments:

Post a Comment