Friday, December 16, 2011

Somo la 13: Injili na Kanisa

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Wagalatia 6:1-10)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, kanisa linapaswa kukabilianaje na dhambi? Je, juhudi za kanisa lako zimefanikiwaje katika kipindi cha nyuma? Mara nyingi, ninaona mambo mawili yakitokea. Kwanza, watu walio wakosoaji wanakosoa dhambi (au zinazodhaniwa kuwa ni dhambi) za watu wengine. Pili, wadhambi wanajisikia kuwa dhambi zao ni “mambo yao wenyewe’ na hivyo kuwataka viongozi wa kanisa “wajali mambo yao wenyewe’ – wakimaanisha kuwa, “tafadhali achana na mimi.” Waathirika wa ukosoaji wanafedheheshwa, na wadhambi waliokubuhu wanarejea ndani ya ganda lao la dhambi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile inachotufundisha kuhusiana na hii mada!

I. Mtego wa Dhambi

A. Soma Wagalatia 6:1. Je, inamaanisha nini “kunaswa” dhambini? (Dhambi yako inawekwa hadharani pale ambapo wewe mwenyewe hukupanga ijulikane hadharani. Au, ulijiingiza dhambini wakati ambapo ungependelea kutembea na Mungu.)

1. Je, hii inahusika kwa wadhambi majasiri? (Kama unajivunia dhambi zako, je, “umenaswa” nayo?)

B. Lazima kutakuwa na kosa la kiuchapaji kwenye Biblia yangu. Lazima Paulo atakuwa alimaanisha kuandika “nyie ambao ni wakosoaji mnapaswa kurejezwa,” sio “nyie ambao ni wa kiroho” mnapaswa kurejezwa. Je, hauoni zaidi hiyo ya awali kuliko hii ya pili?

1. Kama suala la “kiroho” pekee ndilo lilonapaswa “kurejezwa kwa upole,” je, hii inatufundisha nini kuhusiana na mfumo wa kanisa? Je, tunapaswa kuwazuia washiriki wetu walio wakosoaji wasikemee dhambi za watu wengine?

2. Fikiria nyakati ambazo ulikemewa aidha dhambi yako ya kweli au dhambi yako iliyofikiriwa tu lakini haikuwa dhambi. Je, ni viongozi wa kiroho wa kanisa walikukemea? (Mara nyingi huwa ni wageni na washiriki wapya wanaonikemea kwa sababu hawakubaliani na mawazo yangu! Mke wangu wa kiroho anafanya kazi nzuri sana ya kuniweka kwenye msitari sahihi!)

3. Unapoona dhambi kwa watu wengine, je, umegundua kuwa mara nyingi hiyo huwa ni dhambi yako uliyoigundua?

a. Je, kwa kukosa kwako vigezo, unapaswa kuondolewa kwenye mchakato wa “kuwarejeza” watu wengine wanaojihusisha na dhambi hizo hizo/zile zile zinazokufanya upambane nazo?

C. Je, inamaanisha nini kumrejeza mtu “kwa upole?” Je, hii inajumuisha kumfuta mtu ushirika wa kanisa?

1. Soma Mathayo 18:15-17. Je, Yesu anauelezeaje “upole?”


a. Utabaini kuwa katika mfano wa Yesu sio viongozi wa “kiroho” kanisani, bali ni mwathirika wa dhambi anayekabiliana na mdhambi. Je, unalinganishaje ushauri wa Paulo na ule wa Yesu?

II. Kuubeba/Kuuchukua Mzigo

A. Soma Wagalatia 6:2. Je, Paulo amebadili mada?

1. Je, dhambi ni mzigo maishani mwetu? (Ndiyo.)

2. Je, tunawajibika (kama tuna vigezo vya kiroho) kubeba mizigo ya dhambi za watu wengine?

3. Je, “sheria ya Kristo” ina nini cha kujihusisha katika kubeba mizigo ya dhambi za watu wengine? (Utakumbuka kwamba juma lililopita tulijadili tofauti kati ya njia ya“kuhesabiwa haki wa imani” kwenye maisha ya kila siku, na njia ya “matendo na sheria” kwenye maisha ya kila siku. Njia ya imani inauliza, “Je, ninaweza kufanya kitu gani ili nimpendeze Mungu, mwenzi wangu na wale wanaonizunguka hivi leo?” Njia ya matendo inauliza, “Je, ni alama gani nyekundu zinajielekeza kwenye dhambi nilizozivuka hivi leo?” Njia moja inajielekeza kwenye kuwapenda watu wengine, njia ya pili inajielekeza kwako wewe binafsi na kwenye dhambi. Njia ya imani, njia ya sheria ya Kristo, inauliza “Je, nifanye nini ili niweze kuchukua/kubeba mizigo ya watu wengine?” Hii itajumuisha kuwasaidia waushinde mzigo wa dhambi.)

B. Je, ni umuhimu gani unaouhusianishwa na neno “kubeba?” (Kubeba kunaonekana kumaanisha zaidi tu ya msaada mdogo.)

1. Je, ninawezaje “kubeba/kuchukua” dhambi ya mtu mwingine? (Je, ni mara ngapi dhambi ya watu wengine inakuathiri vibaya sana? “Kubeba/kuchuhua” dhambi wakati unamrejeza mtu inamaanisha kuwa unaweza kuwa unateseka kutokana na dhambi ya mtu huyo.)

III. Majivuno Katika Ubebaji/Uchukuaji wa Mzigo

A. Hebu turudie tena kusoma sehemu ya mwisho ya Wagalatia 6:1. Chukulia kwamba unamsaidia mshiriki mwenzako wa kanisa aliyeelemewa na usemaji wa uongo. Je, Paulo anatuambia kuwa kama tukimsaidia mshiriki kama huyo, yumkini nasi tukaanza kuwa waongo?

B. Soma Wagalatia 6:3-5. Hivi punde tu Paulo ameniambia kuchukua/kubeba mizigo ya watu wengine. Sasa ananiambia kuwa nibebe furushi langu mwenyewe!

1. Je, ushauri wa Paulo ya kwamba tuwe waangalifu kuhusu kutojaribiwa unahusika hapa? (Vipande vya fumbo/kitendawili vinaungana! Kama tunamsaidia mwongo na dhambi yake, tunaweza kujaribiwa na majivuno na kudhani kuwa sisi ni wa hadhi ya juu. Tunaweza kujaribiwa kwa usengenyaji kwa kuwaambia watu wengine jinsi gani mtu fulani alivyo mtu mbaya. Tunahitajika “kubeba/kuchukua” mizigo yetu ya majivuno na usengenyaji.)

2. Paulo anatuambia kuwa “tuzipime kazi zetu wenyewe,” “acha majivuno,” na tuachane na masuala ya “kujilinganisha” na watu wengine. Je, anatuambia kuwa tufanye kitu gani? (Hatuwezi kujilinganisha na mwongo. Hatuwezi kuwa na majivuno kutokana na ukweli kwamba sisi sio waongo. Hatupaswi kupima kwa kutumia kipimo cha juu sana “wema” wetu. Tunapaswa kujilinganisha na Yesu, sio na watu wengine. Kumfanya Yesu kuwa kituo cha ulinganifu, kuwa makini na dhambi yetu weyewe, ni “kubeba/kuchukua” “furushi letu” wenyewe.)


C. Sasa basi tumekwishajadili mada hii, je, ni vigezo gani ambavyo kanisa linapaswa kuvitumia kwa “wanawaorejeza” wale walionaswa dhambini? (Hawa wanapaswa kuwa watakatifu wanyenyekevu walio na ufahamu/utambuzi wa dhambi zao wenyewe, wasio wasengeyaji, na walio wapole kwa sababu wanatambua kuwa Mungu amekuwa na upole na unyenyekevu kwao.)

IV. Wakufunzi Wenye Mbaraka

A. Soma Wagalatia 6:6. Hapa ndipo utakaponikaribisha chakula cha usiku! (Hapa anamaanisha kumtoa mtu out – yaani kumpa ofa! Zingatia: Mwandishi huyu ni Mhadhiri (Profesa)). – mkazo (emphasis) ni wangu.

1. Je, ushauri huu unaelekezwa kwa nani? (Paulo anazungumza na wale walionaswa dhambini ambao wamefaidika kutokana na wale wanaowarejeza kwa upole na kubeba/kuchukua mizigo yao.)

a. Je, wadhambi waliorejezwa wanapaswa kufanya nini? (Wanapaswa kuwa mbaraka kwa wale waliowarejeza.)

b. Je, umewahi kuhusika katika kumrejeza mdhambi na kuishia kupata adhabu kutokana na urejezaji huo? (Miaka mingi iliyopita, wenzi fulani waliniomba kuwasaidia kwa sababu walikuwa wakipitia wakati mgumu sana kwenye ndoa yao. Dhambi ilihusika. Nilikutana nao, na nikajitolea kuwa yeyote kati yao aishi nyumbani kwangu kwa muda hadi hapo ambapo wangeweza kuishi pamoja tena. Ilitokea kuwa nilishutumiwa kwa “kufungamana” na mwenzi aliyekuja kuishi nyumbani kwangu kwa muda – ingawaje wenza hao walikubaliana wao wenyewe kuwa nani aje kuishi nasi (mimi pamoja na mke wangu!))

V. Malipo

A. Soma Wagalatia 6:7-8. Kwa nini Paulo anamrejea Mungu kudhihakiwa kwenye sheria ya malipo? (Kama Mungu ndiye mmiliki wa dunia, basi tunapaswa kuwa na uwezo wa kuzitegemea kanuni fulani fulani. Mojawapo ya kanuni hizi ni kanuni ya “malipo.” Kutafuta kuwasaidia watu wengine kunaleta msaada kwako. Kuwadhuru watu wengine kunaleta madhara kwako.)

1. Je, hii inahusianaje na wazo la kumrejeza mtu aliyenaswa dhambini? (Inakupa hoja kwenye jaribu lako la kurejesha! Lakini, wazo la msingi ni kwamba kuonyesha upendo na wema kwa watu wengine kutatupa thawabu.)

B. Soma Wagalatia 6:9. Je, kwa nini tunaonywa kuhusu “kuchoka?” (Ingawaje Mungu yupo kwenye umiliki, dhambi na uhuru wa uchaguzi vinatawala. Mara nyingine malipo yanacheleweshwa. Mara nyingine hatutapewa malipo hadi tutakapofika mbinguni.)

1. Kwenye somo letu la Wagalatia, tumenyumbulisha umuhimu wa “neema.” Je, huu mfululizo wa mafungu unatufundisha nini kuhusu umuhimu wa matendo? (Neema inatupatia wokovu, lakini matendo yana thawabu – thawabu chanya na hasi. Paulo anataja kwa mahsusi thawabu inayotusubiri mbinguni kutokana na matendo yetu mema!)

C. Angalia tena Wagalatia 6:8. Je, nini kilicho cha muhimu kuhusu njia ambayo Paulo anaelezea upandaji sahihi? (Hebu baini njia ya neema: kupanda “kwa kumpendeza Roho.” Utume wetu ni kumpenda Mungu na kuwapenda wale wanaotuzunguka.)

D. Soma Wagalatia 6:10. Kwa nini Paulo anatofautisha kati ya jamaa ya waaminio na watu wengine? (Tuna wajibu mkubwa kwa wale wanaoamini.)


E. Rafiki, je, utaliweka lengo lako ili uwe wa kiroho zaidi ili kwamba uweze kusaidia kubeba/kuchukua mzigo wa dhambi wa watu wengine? Kama umetambua kuwa wewe u mkosoaji zaidi kuliko mtu wa kiroho, je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie utoke kwenye ukosoaji hadi kuwa mtu wa kiroho?

VI. Juma lijalo: Kujivunia Msalaba.

0 comments:

Post a Comment