Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Mwanzo 3, Mambo ya Walawi 5, Warumi 1 & 5)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Chukulia kwamba wewe ni kibaka. Unafurahia kuwapiga watu vichwani mwao, na unafaidika kwa kuwaibia fedha. Fikiria tena mbadala ufuatao. Wa kwanza, kama polisi wakikukamata, basi watakutaka uombe msamaha kisha watakuachia. Wa pili ni kwamba, una mjomba tajiri sana ambaye pale unapokuwa umekamatwa anarekebisha mambo kwa gharama zake mwenyewe. Je, utaichukuliaje tabia yako ya kuwa kibaka? Hutalichukulia tatizo lako kwa dhati, si ndio? Hatuhitajiki kufikiria kwamba sisi ni vibaka, kwani kiukweli sisi sote ni vibaka kwa namna fulani. Dhambi zetu zinawagharimu watu wengine na kuwagharimu fedha. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kulitafakari tatizo letu na hitaji la Mkombozi!
I. “Ukibaka”/Ukabaji wa Kwanza
A. Katika kitabu cha Mwanzo sura ya 3 tunasoma kisa kinachoelezea jinsi ambavyo Adamu na Hawa walivyotenda dhambi. Hebu tukiangalie kisa hicho kwa kusoma Mwanzo 3:9-13. Je, ni mtazamo wa aina gani walio nao Adamu na Hawa kuhusu dhambi yao? (Wanalaumu wengine.)
B. Soma Mwanzo 3:14-15. Je, Mungu anamaanisha nini anapomwambia nyoka kuwa kichwa chake kitapondwa? (Mungu haongei na nyoka tu, anaongea na Shetani. Anamwambia Shetani kwamba atashindwa.)
1. Je, ushindi wa Mungu na kushindwa kwa Shetani vinahusisha kitu gani? (Ni punde tu Shetani alikuwa ameupata utii wa wanadamu. Ni punde tu alikuwa ameingiza dhambi duniani. Dhambi itapaswa kushindwa na utii wa wanadamu kurejeshwa.)
II. Upatanisho kwa Vibaka
A. Soma Mambo ya Walawi 5:5-6. Je, Mungu alitumia njia gani katika kukabiliana na tatizo la dhambi? (Kwamba dhambi lazima iungamwe, na mnyama achinjwe “ili kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi.”)
B. Soma Mambo ya Walawi 17:11. Je, unaweza kuelezea mantiki ya mfumo wa kafara? (Dhambi inamwelekeza mtu mautini. Matokeo na adhabu ya dhambi ni kifo. Mungu aliweka mpango ambao maisha ya kitu kingine yangeweza kulipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu.)
C. Soma Yohana 1:29. Je, Yohana Mbatizaji alisema nini kumhusu Yesu? (Kwamba alikuwa “Mwana-kondoo wa Mungu” ambaye “ataichukua dhambi ya ulimwengu!”)
1. Kama ungekuwa umekaa mahali pale ukimsikiliza Yohana, je, ungehitimisha nini kuhusu mfumo wa kafara na Yesu? (Kwamba mfumo wa kafara ulikuwa unajielekeza kwa Yesu. Ulikuwa ni aina ya unabii. Kwamba kama vile kondoo alivyomwaga damu yake ili kupatanisha dhambi, ndivyo ambavyo Yesu atamwaga damu yake ili apatanishe dhambi zetu.)
III. Matokeo ya Kubaka
A. Soma Luka 1:26-32. Linganisha jinsi ilivyokuwa kwa Yesu kule mbinguni na jinsi alivyokuwa alipokuja kuishi duniani kama mwana wa Mariamu?
1. Hebu niambie yale yote aliyoyaacha Yesu?
B. Soma Mathayo 27:27-31, Matendo 2:23-24, na Mathayo 27:39-42. Je, Yesu aliacha vitu gani?
C. Soma Warumi 5:6-8. Je, Yesu alikuwa akifanya kitu gani alipokufa pale msalabani (kitu cha aibu sana kwa Mungu)? (Alikufa kwa ajili ya dhambi zetu.)
1. Je, ungefanya kile alichokifanya Yesu kama ungekuwa yeye?
2. Je, mtazamo wa Yesu ulikuwa upi? (Haukuwa kwamba tungeweza kufanya kitu chochote kwa ajili yake. Hatukuwa na “uwezo wowote.” Haikuwa kwamba tulikuwa na ustahili wowote. Tulikuwa “wadhambi.” Ilikuwa ni kwa sababu ya upendo tu.)
D. Soma Warumi 5:9. Je, Mungu anawezaje kutughadhibikia na wakati huo huo kutupenda? (Hasira ya Mungu i dhidi ya dhambi zetu.)
1. Kwenye mfululizo wetu wa masomo uliopita, nilipendekeza kwamba tunapaswa kuonyesha matendo yetu kwa kusema kuwa, “Je, hii itampendeza Mungu? Je, hii itamfurahisha mwenza wangu?” Je, ghadhabu ya Mungu inaingilianaje na hili suala?
2. Je, inaleta mantiki kwa Mungu kuighadhabikia dhambi? (Kweli kabisa. Dhambi iliichafua/iliiharibu mbingu. Dhambi iliuharibu Uumbaji wa Mungu hapa duniani. Dhambi ilisababisha Yesu aingie kwenye suala kubwa la kafara na mateso. Mungu anapaswa kuchukia dhambi.)
E. Soma Warumi 5:1-2. Je, hii ni aina gani ya amani? (Mungu anachukia dhambi. Tunapohesabiwa haki kwa imani (yaani pale ambapo haki ya Yesu inapokuwa haki yetu), hii inashughulikia tatizo sugu ambalo Mungu analichukia.)
F. Je, hii inapendekeza kuwa tunapaswa kuwa na mtazamo wa aina gani dhidi ya dhambi? Mtazamo wa aina gani dhidi ya Mungu? (Kwa vile dhambi ingetuua kama Yesu asingeingilia kati, basi tunatakiwa kuichukulia kwa dhati. Ukweli kwamba tuliepuka kulipa adhabu ya dhambi haiifanyi dhambi kuwa na umuhimu wa chini. Ukweli kwamba Yesu aliacha vyote, na kufa kifo cha kutisha kwa ajili yetu unapaswa kutufanya kumshukuru milele!)
IV. Mtazamo wa Kibaka
A. Soma Warumi 1:16. Paulo anapoandika kuwa haionei haya injili, je, hiyo inakuambia kitu gani? (Kwamba kuna sababu ya kuwa na haya. Kama ulikuwa na mwanamke mrembo sana au mume mzuri sana, je, kamwe usingesema, “Sioni haya jinsi ambavyo mwenza wangu anavyoonekana?” Hapatakuwepo na sababu ya ukanaji.)
1. Je, kuna sababu gani iliyopo ya kuionea aibu injili? (Angalia kile kinachofuatia ambacho Paulo anakisema, “ni uweza wa Mungu.” Hiyo ndio alama/ishara yetu. Mungu wetu alikufa. Alisulubishwa na serikali. Hii inaonekana kuonyesha upungufu wa uwezo kwa upande wa Mungu, na hili ni suala la aibu.)
2. Je, usulubishaji unaonyeshaje uweza wa Mungu? Je, huu ni uweza wa aina gani? (Uweza wa Mungu ni upendo. Uweza wa Mungu ni kujitoa kafara yeye mwenyewe. Mungu alijeruhiwa ili kwamba tuweze kuokolewa. Kinachoonekana kuwa ni maelezo ya upungufu wa uweza kimsingi ni uthibitisho wa uweza wa upendo wa Mungu.)
B. Soma Warumi 1:17. Je, haki ya Mungu inayofunuliwa kwenye injili ni ipi – injili ambayo kwa juu juu ni ya aibu? (Kinachofunuliwa ni kwamba Mungu anaishinda dhambi kwa upendo. Hii “haki” inaishinda dhambi. Inatutoa kutoka kuwa watumwa hadi kuwa watu wenye haki.)
1. Je, tunaipataje hii haki? (Inaonekana kuwa kinyume sana na njia za ulimwengu. Lazima tuikubali kwa imani.)
C. Soma Yohana 3:16-18. Je, msingi wa upendo ni kujitoa kafara mwenyewe? (Ndiyo.)
1. Kwa nini Munghu alipaswa kujeruhiwa? (Kumbuka kwamba dhambi inasababisha kifo. Tunapaswa kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Biblia inatuambia kuwa Mungu alikubali kwa hiari “kushindwa,” alikubali kufa kwa hiari kwa ajili yetu kwa sababu alitupenda. Hii inaonyesha kuwa Mungu sio mbinafsi. Kwamba alitupendelea sisi zaidi ukilinganisha na hadhi yake au starehe yake.)
V. Ghadhabu ya Mungu
A. Soma Warumi 1:18-19. Je, Mungu hana furaha? (Ameghadhabika!)
1. Je, Mungu ana sababu ya kutokuwa na furaha? (Hebu angalia mafungu ya Biblia ambayo tumeyapitia hivi punde. Mungu alikwenda mbali sana (alichukua hatua ndefu na za kushangaza) katika mchakato wa kutuokoa. Aliacha kila kitu ili aweze kuwaokoa wale waliomkataa.)
Je, unajisikiaje pale ambapo wale uliowapenda na kuwajali wanapokukataa?
2. Je, ghadhabu ya Mungu inajionyesha dhidi ya nani? (Dhidi ya wale wasio na Mungu na waovu.)
3. Je, sababu ya ghadhabu ya Mungu ni ipi? (Hawa watu wanaukandamiza ukweli.)
B. Soma Warumi 1:20. Je, hawa wakandamizaji wa ukweli wana kisingizio? (Hapana. Asili na uweza wa Mungu vi dhahiri tangu uumbaji. Tunaweza kuona kuwa Mungu yupo na tunaweza kuona kuwa tatizo la dhambi lipo.)
C. Soma Warumi 1:21-22. Je, ni kwa njia gani unaweza kukandamiza ukweli wa Mungu? (Njia nyingi, lakini Mungu anaonyesha njia mbili. Kwa kukana au kugeuza/kubadili kile ambacho Yesu ametutendea. Kwa kukana na kuwakilisha vibaya upendo wa Mungu. Kwa kutokumtukuza Mungu au kwa kutokumshukuru yeye.)
Hebu turejee kwenye lile suala la “haya/aibu.” Kama tunafedheheshwa kuhusu Mungu wetu na ujumbe wetu, je, sisi tu waovu? (Tunaukandamiza ukweli kwa kutompatia Mungu utukufu na kutokuwa na shukrani kwa kile alichotutendea pale msalabani.)
Rafiki, tulianza kwa kukiri kuwa sisi ni vibaka. Kwa sababu kamwe hatukutakiwa kulipa gharama, inawezekana tusizichukulie njia zetu za kiovu kwa dhati. Kisa cha injili kinatusaidia kuzichukulia njia zetu za kiovu kwa dhati. Kinatufunulia upendo mkubwa wa Mungu usio na ubinafsi na njia zetu za kibinafsi. Je, utadhamiria hivi leo kutenda kile kinachompendeza Mungu? Kuonyesha uelewa wako wa kafara yake na upendo wake kwa kugeuka na kuyaacha yale mambo yaliyomsababishia Yesu maumivu makali? Kwa kumpa Mungu utukufu kwa kile ambacho amekutendea?
Juma lijalo: Mungu wa Neema na Hukumu.
Friday, January 13, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment