Thursday, February 16, 2012

Somo la 7: Bwana wa Sabato

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Mwanzo 2, Kutoka 20, Kumbukumbu la Torati 5, Marko 15)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Juma lililopita tulijadiliana kwamba sheria ya Mungu inadhamiria kuwa mbaraka kwa wanadamu, sio kitu cha kutufanya tujikwae. Mojawapo ya mbaraka mkubwa wa sheria ni Sabato. Nilipokuwa kwenye shule ya sheria, mpambano ulikuwa mkali. Sio tu kuwa shule ya sheria ilihitajika mtu kusoma kwa bidii, bali pia wanafunzi walifahamu kuwa ubora wa kazi ambayo wangeipata baada ya kumaliza masomo ya shule ya sheria ulitegemea na nafasi yao kimasomo darasani. Baada ya kumaliza mwaka wa kwanza, shule ilikabiliana na shinikizo kubwa kwa kutotoa matokeo kulingana na nafasi aliyoishika mwanafunzi darasani! Nilikuwa na mahala pangu salama pa kujihifadhi, Sabato. Katika siku hiyo sikufanya kazi yoyote ya shule – na niliweza kupata pumziko bila kujisikia hatia! Kwa hakika nilijisikia vizuri sana. Mungu alibariki uaminifu wangu na akanipatia alama nzuri sana. Hetu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi kuhusu Sabato.

I. Alama za Sabato

A. Soma Mwanzo 2:1-3. Hapo awali tulijadili mafungu haya kwenye somo letu lililohusu utakatifu wa Mungu. Je, tulisema kitu gani kuhusiana na Sabato kuwa takatifu? (Kuwa takatifu ilimaanisha kuwa iliwekwa wakfu kinyume na siku nyingine zote. Ilibarikiwa. Utakatifu wake ulitokana na kitu kilichofanywa na Mungu, sio kitu chochote tulichokifanya sisi.)

B. Soma Marko 2:27. Je, unadhani ni kwa nini Mungu aliifanya Sabato? (Ilifanywa kwa ajili yetu. Kimsingi, ilifanywa kuwa siku ya pumziko kwa ajili yetu.)

C. Soma Kutoka 20:8-11. Je, ni sababu gani nyingine tunayoiona kwa Mungu kuifanya Sabato kuwa takatifu? (Ukumbusho wa uumbaji wa Mungu wa “mbingu na nchi.”)

D. Soma Kumbukumbu la Torati 5:12-15. Je, ni sababu gani tunayoiona hapa ya kuitunza Sabato? (Mungu aliwaokoa watu wake kutoka kwenye kutendewa kusikokuwa kwa haki. Kwa hiyo tunapaswa kuwatendea wale walio chini yetu mambo ya haki kwa kuwapatia pumziko la Sabato.)

1. Je, hiyo ndio sababu ya kutufanya tuamini kuwa Sabato ilifanywa kwa ajili ya Wayahudi pekee? (Hapana. Ulikuwa tu ni mfano wa “kuokoa.” Mungu aliingilia kati ili kuweza kuleta haki. Hivi leo Mungu anatuokoa kutoka kuwa watumwa wa dhambi na kifo.)

II. Sabato Inayofananishwa na Mpira wa Kimarekani

A. Soma Marko 15:33-34, Marko 15:37-39 na Marko 15:42-43. Je, Yesu alisulubiwa siku gani? (Ijumaa, kabla ya Sabato.)

B. Soma Marko 16:1-3 na Marko 16:5-9. Je, Yesu alifufuka kutoka kaburini siku gani? (Jumapili.)


1. Kwa nini ucheleweshaji huu? Hebu jiweke kwenye nafasi ya Mungu Baba. Ni punde tu Mwanao amepigwa hadi mauti kumkuta. Kabla Mwanao hajafa anakwambia, “Kwa nini umeniacha?” Kwa kuongezea, ni punde tu Mwanao ameshinda “Mpira wa Kimarekani (American Football)” wa hapa duniani – ameishinda dhambi na kuuleta ushindi katika Ufalme. Je, utachukua muda gani kumkumbatia Mwanao? Je, utachukua muda gani kusema, “Sijakuacha!” (Sitasubiri! Kwa hakika kabisa, sitasubiri.)

a. Je, kwa nini Mungu alifanya kile ambacho hakuna hata mtu mmoja angeweza kukifanya? (Mungu alisubiria kwa sababu ile ile ambayo alisherehekea uumbaji wa dunia katika siku ya Sabato. Alisubiria kwa sababu ile ile aliyosherehekea ukombozi wa watu wake kutoka Misri siku ya Sabato. Yesu alipumzika siku ya Sabato ikiwa ni kusherehekea kile alichokitimiza!)

III. Sabato na Kanisa la Awali

A. Padre wa kanisa la awali, Ignatius wa Antiokia, kwenye barua yake kwa “Magnesians 9-10” anasema, “Kama wale waliokuzwa kupitia kwenye mfumo wa kale hivi sasa wana matumaini mapya, hawaitunzi tena Sabato, lakini wanaishi kwa kuishika/kuitunza Siku ya Bwana, ambapo maisha yetu yamechipushwa tena na Yeye na ufufuo Wake….. Ni upuuzi kumkiri Kristo Yesu, na kufanya mambo ya Kiyahudi. Kwa maana Ukristo haukuikumbatia dini ya Kiyahudi, bali dini ya Kiyahudi iliukumbatia Ukristo.”

1. Je, ni sababu ipi/zipi ambazo Ignatius anazitoa za kuabudu siku ya Jumapili? (Ufufuo wa Yesu siku ya Jumapili. Uhasama dhidi ya dini ya Kiyahudi.)

a. Je, Wayahudi walikuwa maarufu kwa kiwango gani kipindi ambacho Rumi iliiharibu Yerusalemu na hekalu mwaka wa 70 BK?

b. Je, dini ya Kiyahudi ina ugomvi na Ukristo? (Hii inatupatia mtazamo wa wazi kabisa wa sababu za kuitunza siku ya Jumapili hapo awali. Imejengwa kwenye hoja ya “kimantiki” ambayo sio bora zaidi kuliko mantiki ya Yesu kupumzika siku ya Sabato baada ya kuteswa kwake. Kwa kuongezea, ina upande wa pili wa chuki kubwa ya Wayahudi. Ilikuwa ni baada ya kujiingiza kwenye mjadala wa dhati wa kiteolojia na mmojawapo wa mafariki wangu wa Kiyahudi ndipo nilipoelimishwa kuhusu uhusiano wa karibu wa historia kati ya uhasama/chuki/uadui dhidi ya Wayahudi na ukataaji wa Sabato ya Kibiblia. Uhasama dhidi ya Wayahudi (mfikirie Musa, Petro, Paulo) hauna msingi wa kiteolojia, na hauna nafasi sahihi kwenye fikra zetu. Yesu alikuja kutimiliza, sio kutangua, unabii na matendo ya Agano la Kale. (Mathayo 5:17.)

B. Mfalme Konstatino wa Rumi katika mwaka wa 321 BK alitangaza rasmi Jumapili kuwa siku mpya ya mapumziko kwenye himaya yake. Hivi sasa ninasoma kitabu maarufu sana kuhusu historia ya Yerusalemu. Kinasema kuwa Konstatino alikuwa na matamanio mawili makubwa, uwezo/nguvu ya jua na Ukristo. Alitengeneza sarafu zenye sanamu ya msalaba na nyingine zenye sanamuya jua. Je, hii inapendekeza nini kwenye mtazamo wake wa ibada ya Jumapili? (Alitaka Wakristo wajumuishe ibada ya jua kwenye ibada zao za kidini.)


1. Baadhi ya Wakristo wanasema kuwa hawaijali Krismasi au Pasaka kwa sababu zina mizizi ya “kipagani.” Ninakataa hoja hizi kwa sababu ya umuhimu wa hizi sherehe za kidini kwa Wakristo hivi leo. Je, tunapaswa pia kuwa na mtazamo huo huo kuhusiana na ibada ya kila juma wa Sabato ya Jumapili? (Huo ungekuwa mtazamo wangu kama isingekuwa ni kwa ajili ya amri ya Biblia iliyo wazi kabisa na isiyoyumba kwamba siku ya saba ndio pekee iliyofanywa na Mungu kuwa takatifu. Krismasi na Pasaka kamwe hazikudhihirishwa kuwa takatifu katika Biblia, kwa hiyo nipo huru kudai umuhimu wao wa sasa kwa Wakristo wote waliopo duniani.)

IV. Siku Yetu ya Bwana

A. Jina la kawaida la Jumapili ni kuiita kuwa siku ya Bwana. Je, Yesu aliabudu siku ya Jumapili au alitoa ishara yoyote kuwa aliikana/aliikataa Sabato? Hebu tusome Mathayo 12:1-2. Kama Yesu alitaka kutoa ishara ya kubadili ibada kutoka Sabato kwenda kwenye siku nyingine, je, hii ingekuwa fursa nzuri sana kufanya hivyo?

B. Soma Mathayo 12:3-5. Je, kuna wazo gani lililopo kuhusu utakatifu wa Sabato kwenye haya mafungu? (Analinganisha kula mikate ya wonyesho na wanafunzi wake kula siku ya Sabato – hakuna hata kimojawapo kilicho halali. Analinganisha makuhani kufanya kazi siku ya Sabato na wanafunzi wake “kufanya kazi” siku ya Sabato. Anasema kuwa “hawana hatia,” lakini sio kwa sababu ya tatizo lolote lililopo dhidi ya Sabato.)

C. Soma Mathayo 12:6-8. Kwa nini Daudi hakuwa na hatia, makuhani hekaluni hawakuwa na hatia, na wanafunzi wa Yesu hawakuwa na hatia kwa kuivunja Sabato? (Lengo kuu. Daudi kwa dhati kabisa alikuwa na haki ya kufanya hivi kwa kuwa alikuwa mtiwa mafuta wa Mungu. Makuhani walikuwa wakifanya kazi kwa ajili ya Mungu. Yesu alikuwa Mungu na wanafunzi wake walikuwa pamoja naye katika kuuendeleza Ufalme wa Mungu.)

1. Je, Yesu anamaanisha nini anaposema, “Nataka rehema, wala si sadaka?” (Soma Hosea 6:6. Dhana ya kutembea kwetu na Mungu sio kutoa wanyama sadaka (kutubu dhambi), ni kumpenda na kumtii Mungu. Washtaki wa wanafunzi walikuwa mbele za Mungu, lakini macho yao bado yalikuwa kwenye jambo dogo (lisilo la msingi). Yesu alikuwa hashushi umuhimu wa Sabato. Alikuwa akiwaelekeza wafuasi wake kujikita kwenye jambo la muhimu katika suala lolote lile.)

a. Je, watunzaji wa Sabato watalitumiaje somo hili hivi leo?

D. Soma Yohana 9:10-11 na Yohana 9:13-16. (Niliwahi kuwa na mshiriki wa darasa ambaye alimshutumu kwa nguvu zote Billy Graham kwa kutoitunza Sabato. Haya ndio mashtaka yaliyofanywa na baadhi ya Mafarisayo.)

E. Soma Yohana 9:35-41. Je, Yesu anamaanisha nini anaposema kuwa amekuja ili vipofu wapate kuona? (Kwa mara nyingine tena Yesu anazungumzia kuhusu kuwa na mtazamo sahihi juu ya Sabato na asili ya umuhimu wake. Graham aliwaongoa mamia kwa maelfu ya watu maishani mwake. Huenda zaidi ya mtu mwingine yeyote yule, alikuwa uso (kioo) cha Wakristo wa Kiprotestati kwa miongo kadhaa. Mshiriki mwenzangu wa darasa, ambaye huenda kamwe hajawahi kumwongoa mtu yeyote, hakujikita kwenye Ufalme wa Mungu. Yesu anatuita tujikite kuuendeleza Ufalme wa Mungu.)

F. Soma Mathayo 12:9-12. Je, Yesu anaukataa utakatifu wa Sabato? (Hapana.)


1. Je, Yesu anasema nini kuhusiana na Sabato? (Kwa mara nyingine, anasema kuwa tunatakiwa kuiangalia vizuri - zana ya kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Kuwaponya na kuwasaidia watu wengine kunaendana na Sabato.)

G. Soma Mathayo 12:13-14. Je, ingejalisha kitu chochote kwa yule mtu kama Yesu angesubiria hadi muda wa jua kuzama ili aweze kumponya? (Hapana.)

1. Je, kwa nini Yesu alimponya siku ya Sabato? (Kusisitiza dhana yake ya jinsi ambavyo Sabato inapaswa kueleweka.)

2. Kama Yesu alikuwa anakaribia kuifuta Sabato, kwa nini alifanya juhudi hizi za kubainisha jinsi Sabato inavyoingia kwenye mpambano kwa ajili ya Ufalme wa Mungu?

H. Rafiki, Sabato ni ukumbusho wa kile ambacho Yesu amekifanya kwa ajili yetu – Alituumba, alituokoa kutoka dhambini, alikufa kwa ajili yetu na alifufuka kwa ajili yetu. Kamwe hatutakiwi kuacha kusherehekea siku takatifu aliyotupatia na kamwe haijabadilika. Lakini, lazima pia tuwe na mtazamo sahihi juu ya Sabato katika kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Je, utakubali hivi leo kuitunza Sabato kama sehemu ya kazi yako ya kuuendeleza ufalme wa Mungu?

V. Juma lijalo: Utunzaji wa Viumbe

Wednesday, February 8, 2012

Somo la 6: Mungu Mtoaji wa Sheria

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Kutok 19 & 20, Mathayo 22, Isaya 48)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Somo lililopita tulijifunza kitabu cha Wagalatia, somo ambalo lilitupatia mtazamo wa “sheria dhidi ya neema.” Mtazamo huo utatupotosha isipokuwa tu kama tutafungua macho yetu kwenye mtazamo mpana zaidi. Hebu angalia hapa duniani kwenye nchi zinazoongozwa kwa sheria na uzilinganishe na nchi zinazoongozwa na chochote kile ambacho mtawala anaamua kwa muda huo. Nchi ambazo zinaongozwa kwa “utawala wa sheria” zina mafanikio zaidi na zina uhuru zaidi. Uhuru wa kidini, uhuru wetu wa msingi sana, unapatikana tu kwenye nchi zinazoongozwa chini ya utawala wa sheria. Kama wazo lako la “neema” lina dhana ya kwamba unafanya jambo lolote unalodhani kuwa ni zuri kulifanya kwa wakati huo, basi hapo utakuwa umekosea kabisa dhana ya sheria ya Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuweze kujifunza zaidi kuhusu sheria ya Mungu.

I. Utoaji (“Ofa”)

A. Soma Kutoka 19:3-6. Je, Mungu anatoa ofa ya kitu gani? (Anatoa ofa ya mkataba. Yaani kama watu “watatunza agano langu” watakuwa watu maalum kwa Mungu.)

1. Unadhani Mungu alikuwa anamaanisha nini aliposema kuwa watu watakuwa “ufalme wa makuhani?” (Je, makuhani wanafanya nini? Wao ni wawakilishi wa mungu wao. Mungu anatupatia mahusiano maalum endapo tutamtii.)

2. Kwa nini watu watake kukubali ofa hii? (Kama Mungu alivyokwishawaelezea, alikuwa na uwezo mkubwa kabisa wa kushughulikia matatizo yote waliyokabiliana nayo.)

B. Soma Kutoka 19:7-8. Je, watu waliikubali ofa ya Mungu?

II. Muhtasari

A. Soma Mathayo 22:37- 40. Yesu aliposema kuwa “Torati na Manabii” “inaning’inia” kwenye hizi amri mbili, je, alimaanisha nini? (Hizo ndizo msingi na umuhimu wa sheria.)

1. Angalia wajibu wetu kwa Mungu. Je, ni sehemu yetu gani ambayo Mungu anaitaka? (Yote.)

2. Yesu anaporejea “moyo,” “roho” na “akili,” je, unadhani kuwa anamaanisha nini? Je, hivi vitu vitatu ni tofauti?

3. Je, ni kwa jinsi gani amri ya pili (mpende jirani yako) ina utofauti kwa muktadha wa kujitoa kwayo na ile ya kwanza (mpende Mungu wako)? (Hatuambiwi kuwapenda majirani zetu kikamilifu kabisa, bali tuwapende kama tunavyojipenda wenyewe.)

a. Je, unajipenda kwa kiwango gani?

b. Je, ni sahihi kujipenda wewe mwenyewe? (Ama kwa hakika kabisa!)


B. Je, unadhani kuwa Yesu anaanzisha njia mpya ya kuiangalia sheria? (Soma Kumbukumbu la Torati 10:12. Yesu haanzishi kitu kipya.)

III. Amri Kumi za Mungu - Upendo kwa Mungu

A. Soma Kutoka 19:16-19. Utabaini kuwa hii ni tofauti na njia ambayo Yesu aliutangaza msingi wa sheria kwenye Mathayo 22. Kwa nini Mungu aliwatisha watu? (Alitaka kusisitizia umuhimu wa sheria. Pia alitaka (ukisoma mafungu yanayofuatia) kuwaweka watu mbali ili kwamba wasijaribu kumwona na wafe.)

B. Soma Kutoka 20:1-2. Je, Mungu angeongezea kitu gani kwenye wasifu wake hivi leo? (Mimi ni Bwana Mungu wako niliyekuokoa kutoka katika mauti ya milele.)

1. Je, haya ni madai makubwa zaidi kuliko yale ya awali?

C. Soma Kutoka 20:3. Je, hii inapendekeza nini kuhusiana na Mtoaji wetu wa sheria? (Kwamba anahitaji utii wetu uwe wa kwanza kabisa.)

D. Soma Kutoka 20:4-6. Ni kwa nini hii amri ya pili ni ya muhimu ukizingatia kuwa tayari tunayo ile amri ya kwanza? (Hii inahusiana na heshima/hadhi/utu wa Mungu. Mungu hataki kushushwa na kuonekana kuwa kama “kitu fulani hivi” – hususan, sio kuwa kama kitu alichokiumba, au kitu kilichofanywa/kilichotengenezwa na kimojawapo cha uumbaji wake.)

1. Je, ninapindisha maneno ya Mungu? Anasema kuwa ana “wivu” na nilipendekeza kuwa hiyo ndio ilikuwa hadhi yake. Je, vitu hivi viwili vinatofautiana? (Yesu anaionea wivu nafasi yake – hadhi yake.)

2. Nini kinatokea kwa kumpa Mungu kile anachokistahili? (Mibaraka! Mibaraka hadi kwa watoto wetu.)

E. Je, unawezaje kuzielezea kwa ufupi hizi amri mbili za kwanza? (Zinaakisi somo letu la juma lililopita – zinaonyesha kuwa Mungu ni mtakatifu, amewekwa wakfu, na ni wa kipekee.)

F. Soma Kutoka 20:7. Je, ni kitu gani cha kwanza kabisa kinakujia akilini unapoisoma amri hii? (Kuapa.)

1. Je, unadhani kuwa ni tatizo gani lililopo ambalo Mungu analielezea? Je, ni kwa jinsi gani kuapa ni tatizo kubwa kwenye hilo tatizo lililoelezewa? (Kwa mara nyingine tena, ni utu/hadhi, utukufu wa Mungu, ndilo lililo suala la msingi.)

2. Je, utakuwa unakiuka amri hii kwa wewe kudai kuwa Mkristo na kufanya mambo ambayo yatampa Mungu sifa mbaya? (Nadhani hili ni tatizo kubwa zaidi kuliko kuapa. Watu wanafikiria kwa uchache kuhusiana na kuapa, kwa sababu kwa ujumla wale wanaoapa sio watu wanaodai kuwa wawakilishi wa Mungu. Ni wale wanaodai kuwa wawakilishi, na wale wanaofanya uovu, ndio wanaolitumia vibaya jina lake.)

IV. Amri Kumi – Kipindi cha Mpito

A. Soma Kutoka 20:8-11. Je, hii amri ya nne inahusu kumpenda Mungu au inahusu kuwapenda wanadamu wenzetu? (Inamheshimu Mungu kwa kuwa Muumba wetu, lakini wanadamu wote (hadi waajiriwa wetu) wanafurahia pumziko hili la kila juma.)

V. Amri Kumi - Upendo kwa Jirani


A. Soma Kutoka 20:12. Je, kwa nini heshima kwa wazazi wetu inahusishwa na urefu wa maisha yetu? Je, Mungu anatuambia kuwa “atatushambulia/atatupiga” kwa kutowaheshimu wazazi? (Kwa ujumla wazazi wana busara. Kama tukijifunza kutoka kwao maisha yetu yatakuwa bora na marefu. Kuwapenda wazazi wetu, kama kuwapenda wenzi wetu, ndio njia ya kujipenda sisi wenyewe.)

B. Soma Kutoka 20:13-16. Je, ni kitu gani kinachofanana kinachoonekana kwenye hizi amri zote? (Soma Warumi 13:8-10. Upendo wa watu wengine. Tunapotoa/tunapochukua kutoka kwa watu kitu chao cha haki, tunaonyesha ubinafsi na upungufu wa upendo.)

1. Je, ni kitu gani alichotutendea Yesu? (Alikufa badala yetu. Aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu.)

a. Je, amri hizi zinaakisije kile alichotutendea Yesu? (Msingi wa injili ni kujitoa sisi wenyewe kwa ajili ya watu wengine. Matendo yaliyoelezewa kwenye hizi amri yanachukua vitu kutoka kwa watu wengine kwa faida yetu. Amri hizo ni kinyume cha injili.)

C. Soma Kutoka 20:17. Je, hii inahusianaje na amri nne ambazo tumejifunza hivi punde? (Hii ni sehemu ya mtazamo wa amri zilizotangulia. Ukijiepusha kutaka vitu vya jirani yako, kama ukiridhika na kitu chako, basi hutachukua kitu chochote cha jirani yako.)

1. Je, upendo kwa jirani yako unaingiaje kwenye hii amri ya mwisho?

2. Je, hizi kanuni za Kibiblia zinapaswa kujihusisha na sera za kodi za kitaifa?

3. Kama umesema kuwa ndiyo, Marekani inapokuwa inaingia kwenye miezi ya mwisho ya uchaguzi wa urais, kuna mjadala mkubwa kuhusu kuongeza kodi ya ziada kwa matajiri. Je, huu ni ukiukwaji wa amri ya kumi? Je, huu ni wivu na matamanio?

VI. Amri Kumi za Neema

A. Soma Isaya 48:17. Je, haya ni maelezo ya Amri Kumi? (Haya ni sehemu ya maelekezo ya Mungu “ya jinsi ambavyo unapaswa kuenenda.”)

B. Soma Isaya 48:18-19. Je, matokeo ya kuitii sheria ya Mungu ni yapi? (Amani. Haki. Hadhi. Familia. Haya ndio mambo yote tunayoyataka. Mungu anatufundisha kuwa sheria yake haipo kwa ajili ya kutukosesha. Haipo kwa ajili ya kutuhukumu/kutushutumu. Mungu alitupatia sheria yake kwa sababu anatupenda na anafahamu vizuri zaidi kuwa ni mtazamo na matendo ya aina gani yatakuwa mbaraka maishani mwetu.)

VII. Juma lijalo: Bwana wa Sabato

Wednesday, February 1, 2012

Somo la 5: Utakatifu wa Mungu

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(1 Petro 1, Mwanzo 2, Ayubu 42, Luka 5)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Biblia inatuambia kwa kurudia rudia kuwa Mungu ni mtakatifu. Je, hiyo inamaanisha nini? Hili sio suala linalomaanisha kufurahisha akili zetu tu, kwa sababu Mungu anatuamuru kwenye Agano la Kale na Agano Jipya la Biblia kuwa tuwe watakatifu kama jisi Mungu alivyo mtakatifu. (1 Petro 1:15-16; Mambo ya Walawi 11:44.) Kama hatuelewi kile kinachomaanishwa kwa Mungu kuwa mtakatifu, hatuwezi kuelewa lengo la muhimu maishani mwetu. Hetu tuone tunavyoweza kulibaini hili kwa mara nyingine tena kwa kuzama kwenye somo letu la Biblia!

I. Wakati (Muda) Mtakatifu

A. Soma Mwanzo 2:2-3. Hii inatuambia kuwa Mungu “aliifanya” Sabato kuwa takatifu. Je, muktadha huu unapendekeza kuwa utakatifu unamaanisha nini? (Kwanza kabisa, utakatifu unatoka kwa Mungu. Yeye ndiye mwanzilishi wake. Pili, kuwa takatifu ni kuwa tofauti na siku nyinginezo. Utabaini kuwa utakatifu na mibaraka vinaonekana kufanana. Siku takatifu ni siku iliyowekwa wakfu dhidi ya siku nyinginezo, siku maalum, siku iliyobarikiwa.)

B. Soma Zaburi 86:8-10. Je, ni kipengele gani cha utakatifu wa Mungu kinachofanana na Sabato? (Mungu amewekwa wakfu. Hakuna mungu kama Bwana wetu. Yeye peke yake ndiye mkuu na mzuri ajabu.)

C. Soma Kutoka 20:11. Je, uhusiano iliopo kati ya huu muda mtakatifu na Uumbaji ni upi? (Ni sherehe, ukumbusho wa uwezo wa ubunifu wa Mungu.)

1. Kama haya mawazo kuhusu utakatifu wa Mungu pia yanahusika kwetu kwa namna fulani hivi, je, ni sehemu gani ya kitendawili cha utakatifu tunachoweza kukifahamu? (Utakatifu unatoka kwa Mungu pekee. Inamaanisha kuwa tumewekwa wakfu na kubarikiwa pia. Inamaanisha kuwa maisha yetu yanapaswa kuwa kama usherehekeaji wa uwezo wa Mungu na ubunifu wa Mungu.)

D. Soma 1 Samweli 2:2. Tunapozama kwenye mjadala kuhusiana na utakatifu wa Mungu na lengo la utakatifu wetu, je, hii inatufundisha kitu gani cha muhimu? (Hatuwezi kufikia kiwango cha Mungu cha utakatifu. Hakuna hata mtu mmoja aliye kama yeye! Habari njema ni kwamba hatupaswi kukata tamaa pale ambapo utakatifu wetu mara kwa mara unaonekana kuwa kwenye matatizo.)

E. Soma Kutoka 20:8-10. Je, ni kwa namna gani kuacha kufanya kazi kuna cha kujihusianisha na muda mtakatifu? (Ni wakati wa kujielekeza kwenye kile alichokiumba Mungu, sio vile tunavyovifanya. Hii inaonyesha kuwa utakatifu unatoka kwa Mungu, sio kwetu. Hatutengenezi/hatufanyi muda mtakatifu kwa kufanya jambo fulani.)

1. Je, ni kipande gani kingine cha kitendawili kinaimarishwa na suala hili kuhusiana na sisi kuwa watakatifu? (Hatuwezi kujifanya wenyewe kuwa watakatifu.)

II. Akili Takatifu


A. Soma 1 Petro 1:13-16. Je, tumefanya makosa? Petro anatuambia tuwe watakatifu katika yote tuyatendayo. Je, hiyo inamaanisha kuwa tunaweza kuufanya/ku-uumba utakatifu?

1. Angalia tena 1 Petro 1:13. Je, ni “tendo” gani linafanyika hapa? (Hakuna tendo lolote. Petro anatuambia tu kuwa tujielekeze kwenye zawadi ya neema ya Mungu. Zingatia/kuwa msikivu. Neema (utakatifu?) tunayoipokea “tunapewa,” hatuipati kwa juhudi zetu.)

2. Vipi kuhusu 1 Petro 1:14, ambapo tunaambiwa kuwa “watiifu?” (Tunapojielekeza kwa Bwana wetu, tunajifunza zaidi kuhusiana na mapenzi yake. Kimsingi Petro anasema, “Mmejifunza, kwa hiyo msiishi kufuatana na matamanio yenu maovu.”)

B. Soma 1 Petro 1:17-19. Je, matendo ni sehemu ya kuishi maisha matakaifu? (Ndiyo. Wakati ambapo hatuwezi kujifanya wenyewe kuwa watakatifu, Mungu anatutaraji tuishi maisha yanayoendana na kuwa watakatifu. Lengo la kwanza ni kuzingatia mapenzi ya Mungu. “Je, ninaweza kufanya jambo gani hivi leo ili kuuendeleza Ufalme wa Mungu, badala ya kukiendeleza chanzo cha dhambi?”)

1. Je, kuishi kama “wageni” na “kwa hofu yenye utii” kuna nini cha kujihusisha na lengo letu la utakatifu? (Hatutakiwi kuridhika sana na maisha ya hapa. Sisi sio sehemu ya hii dunia. Sisi ni sehemu ya Ufalme wa Mungu. Kwa hiyo, “tunamhofu” (ikimaabisha heshima, inayohusiana na Mungu). Hatujihusishi na dunia ila kuuendeleza Ufalme wa Mungu.)

2. Je, ni tofauti gani iliyopo ya kwamba tunafidiwa na kafara ya Yesu mwenyewe, badala ya malipo ya fedha? (Inafanya jinsi tunavyoishi maisha yetu yawe ya mtu binafsi. Yesu alilipa gharama kwa ajili ya dhambi zetu kwa kuyatoa maisha yake. Haliwezi kuwa suala la binafsi zaidi ya hapo. Tunahitajika kulichukua lengo la utakatifu na kulifanya kuwa suala la mtu binafsi.)

C. Soma 1 Petro 1:20-21. Je, ni hoja gani unayoiona hapa kuhusiana na neema? (“Tunaamini katika Mungu” kupitia “kwake” – kupitia kwa kile Yesu alichotutendea pale msalabani na katika ufufuo wake.)

D. Soma 1 Petro 1:22. Kwa wazi kabisa hii inaonyesha kuwa kile ambacho nimekuwa nikikifundisha ni makosa, sawa? Kinasema kwamba “tumejitakasa roho zetu kwa kuitii kweli.” Je, ni nini kinachoweza kuwa wazi zaidi ya hicho?

1. Angalia sehemu iliyosalia ya hili fungu. Je, unaweza kusaga meno yako na kumpenda mtu ambaye unamwona kabisa kuwa hapendeki? Vipi kuhusu “upendo wa dhati” kutoka moyoni? (Sote tunafahamu kuwa upendo wa dhati wa “ndugu” unatoka tu kwenye moyo uliobadilishwa na Mungu. Moyo unaotambua kuwa Mungu alikufa kifo cha kutisha kwa ajili yetu, ni moyo unaojibu kwa shukrani na upendo. Upendo wa ndugu ni mwitikio kwa Mungu. Kwa hiyo Mungu, na sio mapenzi ya mwanadamu, ndicho chanzo cha upendo. Hata hivyo, ni kweli kwamba “tabia” ya utii (kinyume na “tabia” ya kutokutii) inasaidia katika njia ya kuuelekea utukufu.)

III. Utukufu Linganishi


A. Sehemu kubwa ya kitabu cha Ayubu kinajumuisha maneno ya Ayubu akijitangazia kutokua na hatia ilhali marafiki zake wanasisitiza kuwa anaadhibiwa kutokana na dhambi zake. Suala la kuvutia linakuja pale ambapo Ayubu anatangaza kuwa anataka awe na Mungu chumbani na amfanye ajibu baadhi ya maswali yake kuhusu usawa na haki. Katika kitabu cha Ayubu sura za 40 & 41 Mungu anamtokea Ayubu na anamwambia kuwa watakuwa na “uendeshaji wa mashtaka,” lakini hali itakuwa ni kwamba Ayubu ndiye atakayekuwa akijibu maswali. Hebu tusome Ayubu 42:1-3. Je, jibu la awali la Ayubu kwa Mungu ni lipi? (Nilijibu nikiwa mpumbavu. Sikuelewa uwezo na utukufu wa Mungu.)

B. Soma Ayubu 42:4-6. Je, utukufu na utakatifu wa Mungu vinatenda kitu gani kwa Ayubu? (Kutubu kwa unyenyekevu. Uelewa wa kwamba hatupo kwenye nafasi ya kuhoji haki na asili ya Mungu.)

1. Je, hii inakubalianaje na mjadala wetu wa awali kuhusiana na kile kinachomaanishwa kwa kuwa mtakatifu? (Kuwa mtakatifu ni “kuwekwa wakfu.” Mungu “amewekwa wakfu” kutoka kwetu. Kamwe hatuwezi kuwa na tumaini la kuweza kuufikia utakatifu wa Mungu. Tunapokea zawadi ya utakatifu anayotupatia na kudhamiria kutembea kwenye njia inayotuelekeza kwenye utakatifu. Kutembea katika njia hiyo hakutegemeani na suala la kama tunaelewa matatizo yote maishani. Kile tunachokielewa ni kwamba Mungu wetu ni mkuu, mwenye upendo na mtakatifu.)

C. Soma Luka 5:1-5. Hebu jiweke kwenye nafasi ya Petro. Je, mawazo yako kuhusu amri ya Yesu ni yapi? (Walikuwa wamekwisha safisha zana zao na vifaa vyao. Yesu anawataka wachafue zana zao ili kwamba waje waifanye kazi hiyo tena. Wanavua samaki usiku, na walikuwa wametia juhudi kubwa sana usiku kucha. Yesu anawaambia kufanya kazi ya ziada. Wao ni wataalam wa uvuvi, Yesu ni mhubiri. Wao wana maarifa makubwa kuhusiana na suala hili.)

D. Soma Luka 5:6-8. Kwa nini hii inaonyesha kuwa Petro ni mdhambi? Alimtii Yesu? (Petro anatambua kuwa yeye sio mwerevu ambaye anajiendekeza kwa Yesu tu. Anatambua kuwa yupo mbele ya nguvu ya ulimwengu. Kitu kitakatifu kimekutana na kisicho kitakatifu na kitiifu, na utakatifu unahitaji utenganifu!)

E. Soma Luka 5:10 (sehemu ya mwisho). Je, kwa nini Yesu asiogope? (Kwa sababu yupo kwenye utume wake kuwapatanisha Mungu Mtakatifu na wanadamu wadhambi. Safari yetu ya kuuelekea utakatifu ni ya “kuwavua watu,” kuuendeleza Ufalme wa Mungu.)

F. Rafiki, je, utaufanya utakatifu kuwa lengo lako hivi leo? Je, malengo, maazimio, matamanio na matendo yako, yatajielekeza katika kuuendeleza Ufalme wa Mungu? Je, utafanya uchaguzi huo sasa hivi?

IV. Juma lijalo: Mungu Mtoaji wa Sheria.